Jukwaa la Kumi la Biashara Zanzibar, Rais Shein asisitiza mambo muhimu

ZANZIBAR,Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Ali Mohamed Shein amesema Serikali ya Awamu ya Saba imejitayarisha kikamilifu kufanikisha dhana ya uchumi wa Bahari, ikiwa ni utekelezaji wa Mpango mkuu wa Maendeleo wa Dira Mpya ya 2020-2050, unaofungamana na Ajenda na Mikakati ya Kimataifa.

Dkt.Shein amesema hayo katika ufunguzi wa Jukwaa la Kumi la Biashara Zanzibar, lililofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul-wakil ,Kikwajuni jijini hapa.

Amesema, kwa sasa Serikali inashughulikia dhamira ya ujenzi wa Bandari mpya ya Mpigaduri na Bandari ya Mafuta na Gesi katika eneo la Mangapwani, huku tayari ikiwa imeshaanzisha Kampuni ya Uvuvi Zanzibar (ZAFICO), kupitia Sheria namba 15 ya mwaka 2013 ya Usajili wa Makampuni Zanzibar.

Alisema, katika kufanikisha dhamira hiyo, pia Serikali imefanikisha ununuzi wa boti mpya ya kisasa ya uvuvi ‘Sehewa I’ huku boti nyingine ya Sehewa II’ ikiwa inaendelea kutengenezwa.

Aidha, alisema Serikali inaendelea na ujenzi wa soko la samaki na Bandari ya uvuvi eneo la Malindi pamoja na uimarishaji wa sekta ya usafiri wa bahari na utalii kwa ushirikiano na sekta binafsi, akibainisha shughuli hizo kuwa na mahusiano ya karibu na sekta za uvuvi na sehemu ya sekta ya utalii.

Dkt.Shein alieleza kuwa lengo la Serikali ni kuongeza maeneo ya shughuli za Uchumi wa Bahari na kuziunganisha katika mfumo mmoja madhubuti, na kusema tayari imeunda Kamati ya Wataalamu yenye wajumbe kutoka sekta mbalimbali ili kufanikisha dhamira hiyo.

Vile vile alisema, Serikali inatarjia kuanzisha Idara ya Shughuli za Uchumi wa Bahari, wakati ambapo Tume ya Mipango imepewa jukumu la kuandaa mkakati wa utekelezaji wa shughuli za Uchumi wa Bahari.

“Katika juhudi za kuendesha uchumi wa Bahari kupitia mfumo huo mpya, Serikali imeangalia utekelezaji wa baadhi ya nchi zilizofanya vyema na kupata mafanikio ya kuridhisha,"alisema.

Alizitaja nchi hizo kuwa ni pamoja na Mauritius, Sychelles, pamoja na Afrika Kusini, akibainisha mfumo huo umegawiwa katika maeneo makuu manne kama inavyotambulika Kimataifa.

Aliyataja maeneo hayo kuwa ni Uvuvi na Mazao ya baharini, nishati mbadala na Upatikanaji wa mafuta na Gesi Asilia katika maeneo ya Bahari pamoja na Utalii wa Fukwe za Bahari.
Akigusia kauli maudhui ya Jukwaa la mkutano wa Baraza la Biashara la mwaka huu isemayo ‘Ushirikishwaji katika kuleta maendeleo endelevu kupitia uchumi wa Bahari’, Dk. Shein alisema ujumbe huo ni mzuri kwa wakati uliopo, kwani unakwenda sambamba na wito anaoutowa wenye lengo la kupanua zaidi shughuli za kiuchumi nchini kwa kuangali fursa nyingine zilizopo, ambazo tayari zimeanza kushughulikia huku kukiwa na uwezekano wa kupata ufanisi zaidi.

Alisema, maudhui ya ujumbe huo yanabeba maana halisi ya uchumi wa bahari, inayolenga kuishirikisha jamii katika matumizi ya fursa za maendeleo endelevu ya kiuchumi yapatikanayo katika rasilimali za baharini kwa kuzingatia ubunifu wa fursa na mitindo imara ya kibiashara inayokwenda na wakati.

Rais Dkt.Shein alieleza kuwa, Serikali inaendelea kuandaa miradi migine muhimu ukiwemo mradi wa “Boosting Inclusive Growth of Zanzibar (BIGZ), utakaofuata baada ya kukamilika mradi wa kuimarisha Huduma za Jamii Mijini (ZUSP).

“Jitihada hizo zinalenga kuyafikia mafanikio zaidi ya kiuchumi, kukiwa na matarajio makubwa zitazaa matunda yenye tija iwapo sekta binafsi itazidisha ushirikiano wake na Serikali katika kubuni na kuweka miradi mizuri yenye faida kwa pande zote,"alisema.
Alisema, Serikali imeamua kushirikiana, kufanyakazi na sekta binafsi na kuisaidia sekta hiyo na ili iwe na nguvu na uwezo katika kufanikisha dhamira ya kuimarisha uchumi wa nchi, kwa kuamini kuwa ‘Private sector is the Engine of Growth’.

“Serikali itafanya kila juhudi kuhakikisha sekta binafsi inakuwa imara, yenye nguvu na kutoa mchango mkubwa katika kuimarisha uchumi wa Zanzibar,"alisema.

Alisema, bado kuna nafasi kwa sekta binafsi ya kuongeza juhudi za ushirikiano na serikali katika kuzitumia fursa kadhaa za biashara, elimu, afya, utalii na nyinginezo zilizopo nchini ili kuongeza ajira.

Alisema, hatua hiyo itawaongezea kipato vijana pamoja na kukuza uchumi wa nchi, akitoa mfano katika sekta ya elimu ambako kuna fani nyingi za teknolojia na ufundi ambazo bado hazijashughulikiwa.

Alisema, sekta ya ufundi inaweza kuanzisha taasisi za ufundi mchanganyiko yaani ‘polytechnic’kwa njia ya ubia na kuwafunza vijana kazi mbalimbali zenye manufaa kwao na jamii kwa ujumla.

Akinasibisha na umuhimu wa jambo hilo, Dkt.Shein alisema, Serikali imeanzisha michepuo maalum katika skuli zainazoanzia ngazi ya sekondari Unguja na Pemba.

Aidha, alisema amefarijika mno na hatua zilizochukuliwa za marekebisho ya uendeshaji wa shughuli za Jumuiya ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima Zanzibar, na kusisitiza umuhimu wa kuongeza juhudi katika kutekelezaji wajibu wao ili ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi uweze kupata ufanisi mkubwa.

Katika hatua nyingine, Dkt.Shein aliwataka wafanyabiashara na wawekezaji nchini kuwekeza katika yanja mpya, ili kupanua wigo wa maeneo ya uwekezaji pamoja na kuongeza fursa za ajira kwa vijana.

Alisema, ipo haja kwa wadau hao kupanua zaidi shughuli za kibiashara badala ya watu wengi kwa pamoja kukumbatia aina moja ya mradi.

Alisema, kila panapokuwa na wigo mpana wa huduma na bidhaa, sekta ya biashara hushamiri na kuendelea kukua.

Akitoa mfano wa sekta zenye fursa zaidi na ambazo hazijafikiwa ipasavyo, alisema wadau wana wajibu wa kuongeza ushirikiano katika shughuli za kilimo na mifugo ambazo zinaweza kuharaksiha azma ya Serikali ya kuwa na viwanda vidogo vidogo na vya kati.

“Hivi sasa kuna bidhaa zinazotokana na kilimo na mifugo ambazo zinatulazimu tuziagize kutoka nje ya Zanzibar, kwa vile kiwango kinachopatikana nchini hakitoshi,”alisema.
Alisema, ili kuwa na uwezo wa kuviendesha viwanda hivyo kwa faida ni lazima kuhakikisha unakuwepo uwezo wa kuvipatia malighafi za bidhaa zinazopatikana humu nchini.

Aidha, alisema katika sekta ya afya kuna fani nyingine ambazo bado huduma zake hzipatikani, mbali na Serikali kununua vifaa na zana muhimu na za kisasa za kutolea matibabu, hivyo kuwepo ulazima wa kuwapeleka nje ya nchi.

Rais Dkt. Shein aliwasisitiza wajumbe umuhimu wa kulipa kodi kwa maendeleo ya nchi na kufanya shughuli zao kwa kuziingatia sheria za nchi, maadili na utamamduni wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

“Ni wajibu wetu sote kuhakikisha tunaendesha biashra kwa kuzingatia usafi wa miji yetu pamoja na uhifadhi wa mazingira katika sekta za kiuchumi na kijamii, ikiwemo maeneo yetu ya bahari,” alisema.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein akihutubia wakati akilifungua Jukwaa la Kumi la Biashara Zanzibar, lililofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni jijini Zanzibar. (Picha na Ikulu).

Aidha, alisema ufumbuzi wa changamoto mbalimbali za uendeshaji biashara kwa haraka zitaondoa vikwazo vinavyokwamisha maendeleo ya biashara humu nchini.

Alitoa pongezi kwa wawekezaji walioko maeneo ya Chumbe, Mnemba pamoja na Misali kwa kuendelea kuyahifadhi maeneo ya bahari, na hivyo kuwezesha kuwepo ongezeko la viumbe katika maeneo hayo.

Vile vile, alitoa pongezi kwa juhudi zinazofanywa na sekta binafsi katika kuimarisha ushirikianao na serikali kwa ajili ya kukuza maendeleo ya nchi, hatua iliyofanikisha upatikanaji wa ajira kwa vijana kupitia sekta hiyo, sambamba na kuimarisha sekta za elimu, utalii, afya na ujenzi wa Mji wa kisasa katika eneo la Fumba na Nyamanzi.

Mapema, Waziri wa Biashara na Viwanda Amina Saluma Ali alisema Zanzibar ina fursa kubwa katika kufanikisha dhana ya uchumi wa Bahari, kwa kuzingatia uwepo wa rasilimali za kutosha katika bahari na fukwe.

Aliwataka wajumbe kutumia vyema Baraza la Biashara lililoundwa kwa mujibu wa sheria ili kuimarisha mfumo wa kibiashara kati ya Serikali na sekta binafsi.

Nae Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, anayeshughulikia mazingira, Mussa Hassan Zungu aliipongeza Serikali kwa kukusanya vyema kodi , hivyo kuiwezesha nchi kupiga hatua kubwa ya maendeleo kupitia fedha zake za ndani.

Alisema, changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika uendeshaji wa shughuli za kibiashara, zitaweza kupatiwa ufumbuzi pamoja na kuondokana usumbufu, hususan katika maeneo ya Bandari pale panapokuwa na dhamira ya kweli ya kufanya hivyo.

Aidha, Waziri wa Viwanda na Biashara wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Innocent Bashungwa alisema, kuna kasi kubwa ya maendeleo iliyofikiwa Zanzibar katika uongozi wa Serikali ya Awamu ya Saba iliyo chini ya Rais Dkt. Ali Mohamed Shein, akitoa mfano wa mafanikio hayo katika Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume na Bandari ya Malindi.

Alisema, kuna fursa kubwa za kiuchumi kupitia Bandari ya Malindi na kuzitolea mfano wa nchi za Mauritius na Singapore ambazo zimefanikiwa sana kiuchumi, zikiwa na mazingira yanayofanana na Zanzibar.

Kwa upande wake, Rais wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima, Tawfiq Salim Turki akitoa salamu za jumuiya hiyo aliipongeza Serikali kwa kufanikisha uaandaji wa sheria ya Jukwaa la Biashara, sambamba na kufanikisha utendaji kazi wa Bandari ya Zanzibar kwa saa 24.

Alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuvitunza vivutio vya utalii vilivyoko katika maeneo ya Bahari, ikiwa ni hatua muhimu katika kufanikisha dhana ya Uchumi wa Bahari.
 
Katika mkutano huo, mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwemo Uchumi wa Buluu, miradi ya ubia baina ya sekta ya umma na sekta binafsi pamoja na miradi ya serikali
.
Mada nyingine zilizowasilishwa ambapo wajumbe walipata fursa ya kuzijadili ikiwemo Jukumu la Wawekezaji katika kuishirikisha jamii pamoja na tathimini ya mfumo wa usimamizi wa utoaji wa leseni za biashara.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news