Mama anaomba ushauri, ndoa imemtatiza

HABARI wanajukwaa, naombeni ushauri wenu...

Mimi ninaitwa Aisha wa Magomeni Mapipa jijini Dar es Salaam, natambua mawazo ya wengi yanaweza kunipa mwanga wa maisha. Nimefunga ndoa na mwanaume mwenye watoto wanne wawili wa kike na wawili wa kiume. Mama yao alifariki kwa ajali ya gari aliwaacha wadogo wakiwa shule ya msingi.

Na mimi niliolewa nikiwa na mtoto mmoja wa kike ambae kiumri analingana na mtoto wake wa tatu.Kiukweli mwanzoni iliniwia vigumu sana kukubali ombi lake hasa nikifikiria kulea watoto wa mama mwingine kwamba watanikubalije na vipi kuhusu huyu nilie naye?.

Baada ya muda kupita na kukolea kimapenzi nilikubaliana nae, tukafunga ndoa tukaunganisha familia wote wakawa kitu kimoja. Mungu akabariki tukajaliwa kupata mtoto mmoja. Kiukweli niliwapenda sana hawa watoto, niliwalea kama wangu.

Nilijitahidi kadri ya uwezo wangu kuwafanya wasijione wakiwa. Kama zawadi nikiwa natoa nilitoa mezani bila kubagua, sikupenda kuweka makundi na hili shahidi ni Mungu pekee. Watoto watatu wapo chuo kikuu na mmoja wa kwake yupo kidato cha sita.

Katika ndoa yangu kulikuwa na migongano upande wa tendo la ndoa, kabla ya ndoa tukiwa kwenye stori za mapenzi niliwahi kumweleza mwenzangu kuwa mimi sio mtundu sana upande huo, hivyo ningependa yeye awe mwalimu kwangu, kwani tangu mwanaume wa kwanza anidanganye na kunipa ujauzito sikuwahi tena kuwa na mwanaume.
Aliniambia sawa. Tulipoingia kwenye ndoa mwenzangu alianza kubadilika wakati mwingine alikaa hata miezi 8-10 bila kutaka tendo.Nikimuuliza husema amechoka au hajisikii.

Hata huo muda anaokaa mpaka mimi nimchokoze na hii nikutokana na kushindwa kuvumilia. Kuna wakati aliamua kuniambia ukweli kuwa sijui mapenzi, niliumia ila nilikubali kuwa ni kweli sijui ila anisaidie kujua.

Hakufanya hivo. Ilifikia wakati nikaona ngoja nikae nisimsumbue ila nilijiuliza nitaishi hivi mpaka lini na kusaliti ndoa siwezi. Nilimuomba Mungu sana anipe uvumilivu ila pia Mungu aseme na mimi juu ya hii ndoa.

Mungu ni mwaminifu. Baada ya maombi ya zaidi ya mwaka mke wa shemeji yangu alileta malalamiko kuwa mume wangu amekua akimsubua sana kimapenzi ikiwa ni pamoja na kumtumia picha za ngono.

Niliziona, hakuishia hapo akasema hata hawa wadada wa kazi huwa anatembea nao. Nilipowabana waliopo na walioondoka walikubali na kunipa ushahidi. Mbaya zaidi hata huyu mwanangu alishamtaka kimapenzi sina uhakika kama alifanikiwa au la.

Ninaumia sana sana. Mtaani ndoa yangu imekua mfano wa kuigwa hilo ni kutokana na jinsi tunavoonekana kwa watu. Lakini hii yote inatokana na jinsi nisivopenda watu wajue mambo ya ndani. Ninampenda, nina mheshimu, ninamjali.Siruhusu nguo au chakula cha mume wangu afanye mwingine nikiwepo.

Hata kama tumegombana nisingependa yoyote ajue, nilijitahidi sana, kuwa mtiifu na mnyenyekevu kwake. Hii ni kutokana na malezi niliyolelewa. Hata kama amesafiri watoto watajua baba anarudi kwa kuwa wataniona jinsi ninavokua 'busy' jikoni na kuandaa juisi na matunda.

1 Comments

Previous Post Next Post

International news