Aliyekuwa mgombea Ubunge wa CHADEMA ajivua, Majaliwa awaeleza wana Kyerwa sababu za kumchagua Dkt.Magufuli

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa Kyerwa wamchague Dkt. John Pombe Magufuli kwa sababu anatoka katika chama ambacho kina mikakati inayotokana na mawazo ya wananchi.

"Dkt.Magufuli anatoka kwenye chama ambacho kina utaratibu katika kuendesha nchi, chama ambacho kinaratibu kero za wananchi, ambacho kinasikiliza wananchi mpaka ngazi ya chini,"amesema.

Ametoa wito huo leo Septemba 29, 2020 wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Nkwenda, akiwa njiani kuelekea Isingiro wilayani Kyerwa, mkoani Kagera.

"Tumemjaribu na amefanya mambo makubwa katika wizara alizoziongoza na ndiyo maana namleta kwenu Dkt. Magufuli na kumuombea miaka mingine mitano ili alete maendeleo zaidi."

Mheshimiwa Majaliwa ambaye yuko mkoani Kagera kumuombea kura mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. Magufuli alitumia fursa hiyo kumnadi mgombea ubunge wa jimbo la Kyerwa, Bw. Innocent Bilakwate, mgombea udiwani wa kata ya Nkwenda, Bw. Edward Katunzi na wagombea wa CCM wa kata za jirani.

Amesema CCM ni chama kinachoongozwa na Ilani ya Uchaguzi na kuna mambo yamethibitika katika ilani inayoishia 2020. "Leo tunaleta kitabu kingine cha Ilani ya 2020 - 2025. Kama tuliweza kufanya makubwa ndani ya miaka mitano na kile kitabu kidogo, je huko tuendako itakuwaje?"

Akiwa Isingiro kwenye mkutano wa hadhara, Mheshimiwa Majaliwa alisema Serikali ilibadilisha sheria tangu mwaka 2017 na ikazuia uuzaji wa madini ya bati nje ya nchi kwa kutumia njia za panya.

"Sheria inatutaka tutenge ekari kadhaa kwa ajili ya wachimbaji wadogo. Leo hii ekari 38,000 zimetolewa kwa wachimbaji wadogo wa madini mbalimbali. Pia tumeanzisha masoko ya madini 26 na vituo vidogo 28 vya kuuzia madini," alisema.

Akifafanua kuhusu vitambulisho vya Taifa, Mheshimiwa Majaliwa alisema Tanzania ni nchi ya amani na wengi wanatamani kuja kuishi nchini.

Alisema wilaya za Kyerwa, Karagwe na Missenyi ni za mipakani kwa hiyo zina changamoto za uhamijai na masuala ya kiraia. "Ndiyo maana Serikali inakuwa makini katika uhakiki. Tutaimarisha usimamizi ili kila Mtanzania apate kitambulisho.”

Pia amewaonya maafisa wanaohusika na utaoaji vitambulisho vya uraia ambao wanapokea hongo na kuwapa vitambulisho hivyo watu wasiostahili.

Wakati huohuo, Mheshimiwa Majaliwa amempokea aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo la Karagwe kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. Princepius Rwazo ambaye ameamua kurejea CCM.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Bw. Rwazo alisema alikuwa mgombea ubunge kwenye uchaguzi mkuu uliopita na aliisumbua sana CCM lakini sasa ameamua kurejea kwani ameona mazuri yanayofanywa na Chama hicho.

"CCM imejibu kiu zetu, kimekuwa kama chama cha upinzani, na wapinzani sasa wamelala. Nimerudi CCM, sihitaji cheo chochote, shida yangu ni kujiunga na watu wanaochapa kazi. Nitamuunga mkono Dkt. Magufuli na ndugu yangu Bashungwa," alisema na kushangiliwa. Mheshimiwa Majaliwa anaendelea za ziara yake katika wilaya za Karagwe na Missenyi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

1 Comments

  1. Alikuwa mbunge au alikuwa mgombea?yaan Bila kuitaja chadema hamuuzi habari

    ReplyDelete
Previous Post Next Post

International news