Amsha Amsha ya Uhuru FM yawaibukia wafanyabiashara wadogo Moshi, wasema Oktoba 28 upinzani wataisoma namba

WAFANYABIASHARA ndogo ndogo wa Soko la Samaki la Manyema mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, wamesema vyama vya upinzani mwaka huu 2020, havina nafasi tena vijiandae kufungisha virago, kwani havijawasaidia chochote wananchi na badala yake safari hii watawachagua wagombea wa Chama Cha Mapinduzi kupitia Uchaguzi Mkuu Oktoba 28,mwaka huu, anaripoti PIUS NTIGA kutoka MOSHI.

Wakizungumza na Amsha Amsha ya Uhuru FM katika Soko la Manyema, wafanyabiashara hao wamesema walifanya makosa kwa muda mrefu kukumbatia upinzani mkoani Kilimanjaro hususani Moshi, lakini safari hii Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli imeleta mafanikio makubwa mkoani huo, hivyo Oktoba 28, mwaka huu wataichagua CCM kwa kura nyingi.
Mwenyekiti wa Soko la Manyema, Ismael Mkwinda, amesema licha ya soko hilo kutokuwa na huduma ya choo, wamesema wanaimani kubwa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi itawajengea huduma hiyo.

Kina mama akiwemo Hamisa Ali pamoja na Bibi Mariam Mussa wamesema kupitia vitambulisho vya wajasiriamali na mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na halmashauri, wamesema imewasaidia kwa kiasi kikubwa kukuza vipato vyao na hivyo wanaimani na CCM na kwamba mwaka huu hawatafa ya makosa.

Wamesema mazingira ya kazi yao katika Soko hilo ambalo lipo katika Jimbo lililokuwa linaongozwa na Upinzani sio mazuri na wamesema Mgombea Ubunge wa CCM katika Jimbo la Moshi Mjini, Priscus Tarimo watampigia kura nyingi ili alete mafanikio makubwa Moshi.
Kuhusu ujio wa Treni ya Mizigo na Abiria katika Mkoa wa Kilimanjaro na Arusha, wamesema walikosa huduma hiyo kwa kipindi kirefu cha zaidi ya miaka 30, hivyo hatua hiyo iliyosaidia kupunguza gharama za usafiri wa abiria na mizigo, inawapa mtumaini ya kuipenda Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli, ambayo imeleta maajabu makubwa kwa muda mfupi.

Aidha, sekta ya elimu bila malipo, miundombinu ya barabara, huduma ya maji pamoja na vitambulisho vya wajasiriamali, wamesema wanampenda Rais Magufuli kwa kuwa habagui na maendeleo hayana chama hakuwabagua wananchi wa Moshi licha ya kuchagua upinzani, na hawatarudia makosa hayo.
Wakati huo huo, wananchi wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, wamesema iwe mvua, iwe jua, mwaka huu Jimbo la Same Mashariki linarudi CCM, kauli ambayo iliungwa mkono na Katibu wa CCM Wilaya ya Same, Mama Victoria Mahende.

Katika mahojiano na Uhuru Fm wananchi hao wamesema, jimbo hilo la Same Mashariki ambalo lilikuwa chini ya upinzani, safari hii CCM imemleta mgombea ambaye ni Mama Anna Kilango Malecela, hivyo watamchagua ili aharakishe maendeleo ya Wanasame.

Kuhusu zao la tangawizi ambalo linalimwa kwa wingi Same, Katibu wa CCM Wilaya ya Same amesema kupitia serikali ya CCM wakulima wa zao hilo watapewa mitaji ya kilimo kupitia zao hilo la Tangawizi.
Aidha,kuhusu sekta ya afya amesema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli imepeleka kiasi cha shilingi Bilioni mbili ambazo zimetumika kufanya ukarabati wa Hospitali ya Wilaya ya Same, hivyo wananchi wanapongeza hatua hivyo na kuwa na imani na CCM.

No comments

Powered by Blogger.