Balozi Ibuge:Miundombinu imara ni chachu ya mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Kamishna wa Polisi Thobias Andeng'enye alipowasili katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa kwa ajili ya kujitambulisha kabla hajaanza ziara ya ukaguzi wa miradi ya miundombinu inayoratibiwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki. (WMNUAM).

Utekelezaji wa miradi ya miundombinu chini ya Mtandao wa Miradi ya Barabara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (East Africa Road Network Project-EARNP), yenye dhamira ya kuunganisha nchi wanachama za jumuiya hiyo, kwa lengo la kuongeza kasi ya biashara inaendelea kushika kasi kwenye maeneo mbalimbali ya mipaka baina ya nchi hizo, anaripoti Mwandishi Maalum Diramakini.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge anafanya ziara katika Mkoa wa Kigoma kuanzia jana Septemba 28 na leo Septemba 29, 2020, kukagua baadhi ya miradi hiyo inayounganisha Tanzania na Burundi.

Ziara hiyo inakuja muda mfupi baada ya ziara ya Rais wa Burundi,Evariste Ndayishimiye aliyoifanya nchini katika Mkoa wa Kigoma Septemba 18, 2020.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe,Kanali Michael Ngayalina pamoja na ujumbe wao wakikagua eneo litakalojengwa kituo cha Kutoa Huduma kwa Pamoja Mpakani mwa Tanzania na Burundi katika miji ya Manyovu/Mugina. (WMNUAM).

Rais Ndayishimiye na mwenyeji wake,Dkt.John Pombe Magufuli waliazimia kukuza biashara kati ya nchi zao kwa kuimarisha miundombinu mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara, reli na meli za kisasa.

Balozi Ibuge alitembelea mradi wa barabara kutoka Nyakanazi hadi Kasulu hadi Manyovu wenye urefu wa kilomita 310 ambao unahusisha pia ujenzi wa Kituo cha Huduma kwa Pamoja cha Manyovu/Mugina na Daraja la Mto Malagarasi.

Ujenzi huo ambao kwa kipande cha Nyakanazi-Kibondo/Kabingo chenye urefu wa kilomita 50 umeanza kutekelezwa kwa fedha za Serikali ya Tanzania.

Kipande kilichobakia cha kilomita 260 kutoka Kabingo-Kasulu hadi Manyovu, Mkandarasi yupo tayari kwenye eneo la ujenzi na anaendelea na shughuli za awali.

Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia Mipango na Miundombinu, Mhandisi Steven Mlote (kulia) akiwasikiliza wakandarasi kutoka China wanaojenga barabara inayounganisha Tanzania na Burundi kutoka Kasulu hadi Kibondo.

Gharama za ujenzi wa barabara hiyo ya kilomita 260 ni Dola za Marekani milioni 256.2 ambazo ni mkopo nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).

Aidha, Serikali ya Tanzania imetoa fedha zaidi ya Shilingi bilioni 13 kwa ajili ya kuwafidia watakaopitiwa na barabara hiyo ambapo waathirika zaidi ya aslimia 93 wamehalipwa fidia zao na asilimia saba iliyosalia watalipwa hivi karibuni, baada ya wao kufanya marekebisho ya kasoro zilizojitokeza.

Balozi Ibuge alifurahishwa na maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo ambapo alitumia fursa hiyo kuwasihi wakandarasi waendani na kasi na ari ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dkt. Magufuli ya kuhakikisha kuwa barabara hiyo inakamilishwa mapema kabla ya muda uliowekwa wa miaka mitatu.

Alisema, ujenzi wa miundombinu hiyo inasaidia kuongeza kasi ya muingiliano wa watu baina ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo ni moja ya Sera Kuu ya nchi hizo.

Aliendelea kueleza kuwa sio tu, ujenzi wa miundombinu hiyo utarahisisha biashara ya bidhaa na huduma baina ya nchi za jumuiya, bali pia utaongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa kwa sababu ya uhakika wa soko katika nchi wanachama.

Balozi Ibuge alitumia fursa ya ziara hiyo kutembelea Kambi ya Wakimbizi ya Nduta na kuongea na Mkuu wa Kambi hiyo kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo zoezi la kuwarejesha wakimbizi kwa hiyari katika nchi zao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news