Mgombea Ubunge Dkt.Angeline Mabula asema Bilioni 276/- zinakwenda kufuta kero ya maji Ilemela

Zaidi ya shilingi bilioni 276 zinatarajiwa kumaliza adha na kero ya maji ndani ya jimbo la Ilemela na majimbo jirani yakiwemo Nyamagana na Magu, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Hayo yamesemwa na mgombea ubunge jimbo la Ilemela kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Angeline Mabula wakati akizungumza na maelfu ya wananchi na wanachama wa chama hicho waliojitokeza kwenye mkutano wake wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya Kangae 'A' Kata ya Nyakato.

Amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt.John Magufuli imetoa fedha hizo kwa ajili ya kutatua kero ya muda mrefu ya ukosefu wa maji kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza hususani jimbo la Ilemela. 

"Dkt.Magufuli amewekeza zaidi ya sh.bilioni 276 kumaliza kero ya maji kwa Ilemela na majirani zake wa Nyamagana na Magu,"amesema Dkt.Mabula.

Aidha, Dkt.Mabula ameongeza kuwa wakati anaingia madarakani mwaka 2015 jimbo la Ilemela kupitia manispaa lilikuwa na uwezo wa kukopesha jumla ya shilingi milioni 216 na mpaka mwaka huu 2020 wamefanikiwa kuongeza fedha za mikopo kwa vijana,akina mama na watu wenye ulemavu kufika shilingi bilioni moja na milioni 431.

Pia amesema,sheria imetungwa kwa ajili ya kusimamia utoaji wa fedha hizo tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambapo mikopo hiyo ilikuwa ikitolewa kwa utashi wa watu wachache kupelekea baadhi ya watu kutonufaika nayo.

Akimkaribisha mgombea huyo, Meneja kampeni Kazungu Safari Idebe amesema kuwa, zipo sababu zaidi ya milioni juu ya kwa nini wananchi hao wakichague Chama Cha Mapinduzi na wagombea wake ikiwemo ujenzi wa miradi ya kimkakati ya upanuzi wa uwanja wa ndege, ununuzi wa ndege mpya, ujenzi wa meli na vivuko ndani ya Ziwa Victoria na maziwa mengine, ujenzi wa mradi wa reli ya kisasa na mradi wa ufuaji wa umeme wa Mwalimu Nyerere.

Nae Mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Ilemela, Nelson Mesha akawaomba wananchi waliojitokeza katika mkutano huo kukiamini tena chama chake na kuwachagua Dkt.John Magufuli kwa nafasi ya Urais, Dkt Angeline Mabula kwa nafasi ya ubunge huku nafasi ya udiwani akiomba wapewe madiwani wote wanaogombea kwa tiketi ya chama hicho.

No comments

Powered by Blogger.