Bodi ya Wakurugenzi TANESCO yaacha neema Kijiji cha Kakeneno

WANANCHI wa Kijiji cha Kakeneno wilayani Chato mkoani Geita wamepongeza Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco, Dkt.Alexander Kyaruzi kwa kupeleka huduma ya umeme katika kijiji hicho baada ya kuagiza kuunganishiwa umeme ndani ya siku moja kwa kaya mbalimbali, anaripoti ROBERT KALOKOLA kutoka GEITA.
Akizungumza kwa niaba ya wa wananchi wa kijiji hicho mwenyekiti wa kijiji,Masumbuko Thomas amesema kuwa, wakazi wa Kakeneno walikuwa wanapata usumbufu mkubwa wa kupata huduma mbalimbali kama kusaga mahindi,lakini baada ya Tanesco kupeleka umeme kupitia REA maisha yameanza kubadilika.

Mwenyekiti wa kijiji amesema kuwa, kaya 23 zimenufaika na umeme huo huku kaya 20 zikiwa zinasubiri kuunganishiwa huduma hiyo baada ya kujiandaa kwa ajili ya kulipia.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco, Dkt. Alexander Kyaruzi ameagiza kaya zote hizo ambazo ziko tayari kulipia zifanye hivyo na kufungiwa umeme mara moja.



Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi ya Tanesco Dkt.Alexander Kyaruzi (wa kwanza kushoto) akitazama moja ya nguzo za umeme wa REA katika Kijiji cha Kakeneno wilayani Chato,akiwa na wajumbe wa bodi hiyo pamoja na wataalamu wa Tanesco na REA.(Picha na Robert Kalokola/Diramakini).

Masumbuko Thomas ametaja baadhi ya taasisi zilizounganishiwa umeme huo kuwa ni makanisa katika kijiji hicho na baadhi ya kaya.

Amesema kuwa,hadi sasa kuna wananchi 20 ambao wako tayari kwa ajili ya kuunganishiwa umeme ili waendelee na shughuli zao za kiuchumi.

Deus Emmanuel ambaye ni mmiliki wa mashine mbili za kukoboa na kusaga nafaka ameieleza Diramakini kuwa, kabla ya umeme wa REA alikuwa anatumia mafuta ya dizeli ambayo yalikuwa yanampa hasara, lakini sasa hivi anategemea kufanya kazi kwa faida baada ya kuunganishiwa umeme.

Ameongeza kuwa, kutumia umeme mashine inakoboa au kusaga nafaka nyingi zaidi kwa muda mfupi kuliko kutumia mafuta.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco,Dkt. Alexander Kyaruzi amesema umeme una faida nyingi za kiuchumi kwa wananchi.

Amesema, wananchi wakiwa na umeme ni rahisi hata watoto wao kujisomea,wenye mashine za kusaga kusaga unga,mafundi samani kuranda mbao na hata kuchomelea vyuma.

Dkt.Alexander Kyaruzi ameelekeza wataalam wa Tanesco na REA pamoja mkandarasi wa mradi huo katika Kijiji cha Kakeneno kuunganisha umeme kwa wananchi hao kwa muda mfupi.

Meneja wa Miradi ya Tanesco, Mhandisi Emmanuel Manilambona amemhakikishia Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco, Dkt. Alexander Kyaruzi kuwa, watamsimamia mkandarasi wa mradi huo ili huduma ifike kwa wakati kwa wananchi hao.

Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco ikiongozwa na mwenyekiti wake,Dkt. Alexander Kyaruzi iko mkoani Geita kwa ajili ya kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na shirika hilo.

Baadhi ya miradi ambayo imeshakaguliwa na bodi hiyo ni ujenzi wa kituo cha kupozea na kusambaza umeme cha Mpomvu Mjini Geita ( substation) , ujenzi wa ofisi ya mkoa ya Tanesco ,Stoo ya mkoa ya Tanesco pamoja na mradi wa kusambaza umeme vijijini ( REA) katika kijiji cha Kakeneno wilayani Chato.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news