TAKUKURU yarejesha milioni 600/- zilizofanyiwa ubadhirifu malipo ya korosho

“Nimewaita kwa mara nyingine tena ili kupitia kwenu, tuujulishe umma kazi ya uchunguzi iliyofanywa na TAKUKURU Mkoa wa Mtwara kuhusu taarifa tuliyopokea tarehe 14 Machi 2020 kutoka chanzo cha siri.

"Kwamba kuna wizi na ubadhirifu mkubwa wa fedha za Serikali uliodaiwa kufanywa katika malipo ya korosho za msimu wa 2018/2019 ambao Serikali ilinunua korosho kwa wakulima.

“Taarifa ilieleza kuwa kuna fedha za Serikali zilizotolewa kwa ajili ya malipo ya wakulima wa korosho, lakini sehemu ya fedha hizo zilifanyiwa ubadhilifu na watu wasio waaminifu na kusababisha wakulima kutopata fedha zao;

Hayo yamebainishwa na Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Mtwara, Enock P.Ngailo wakati akitioa taarifa kuhusiana na hatua hiyo kwa umma.

“Uchunguzi wa awali dhidi ya tuhuma hii ulifanyika na kubaini kwamba baadhi ya watumishi wa Serikali walioaminiwa na kupewa jukumu la kuwa kwenye timu ya uhakiki na timu ya malipo ya korosho katika msimu wa 2018/2019 walikula njama na kufanya wizi na ubadhirifu wa fedha za Serikali kwa kuingiza katika nyaraka za malipo majina na akaunti za watu ambao hawakuuza korosho kwenye msimu huo na kisha kulipa fedha na wengine wakulima halali kwa kuwazidishia fedha ambazo baadae ziliwarudia watumishi hao.

“TAKUKURU Mkoa wa Mtwara ilifanya uchunguzi wa kina kwa kuishirikisha Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Tanzania (CPB) iliyokuwa na jukumu la kusimamia malipo hayo. Hadi sasa uchunguzi umebaini yafuatayo:-

i) Kiasi cha fedha shilingi 922,702,132.65 zililipwa kwa watu ambao hawakuuza korosho

ii) Kiasi cha fedha shilingi 533,809,490.01 zililipwa zidifu kwa wakulima waliouza korosho

iii) Hivyo jumla ya fedha za Serikali zilizolipwa kwa wasio stahili ni shilingi 1,456,511,622.67

Katika uchunguzi huu tulibaini kuwa fedha zilizolipwa kwa watu ambao hawakustahili zilikwenda kuwanufaisha baadhi ya watumishi wa Serikali waliohusika katika timu za uhakiki wa malipo hayo, baadhi ya wafanyabiashara, baadhi ya wakulima na baadhi ya maafisa wa benki waliohusika kuchakata malipo ya msimu huo.

“Kufuatia yaliyobainika katika uchunguzi huu, zoezi la kuwatafuta watuhumiwa, kuwahoji kwa kina na kuwabana ili warejeshe fedha hizo Serikalini lilifanyika na linaendelea kufanyika. Hadi sasa takwimu za fedha zilizookolewa ni kama ifuatavyo:-

a) Kiasi cha fedha zilizookolewa kupitia TAKUKURU Mkoa wa Mtwara ni shilingi 600,000,000

b) Kiasi cha fedha zilizookolewa kupitia CPB ni shilingi 147,941,718.99

c) Hivyo jumla ya fedha za Serikali zilizookolewa ni shilingi 747,941,718.99

Zoezi linaloendelea kwa sasa ni kufuatilia miamala katika baadhi ya akaunti za kwenye tuhuma hii, kuwatafuta watuhumiwa walionufaika na fedha hizo, kuwahoji kwa kina na kuwabana ili warejeshe fedha hizo Serikalini ili zikatumike kuwalipa wakulima ambao bado wanaidai Serikali.

“Wizi na ubadhirifu huo wa fedha za Serikali ulisababisha madhara makubwa kwa wakulima halali waliostahili fedha hizo na wengi wameshindwa kukidhi kuhudumia mashamba yao, kutatua shida zao za kifamilia na kupelekea kuilaumu Serikali yao kwamba imewadhulumu korosho zao.

“Tunapenda wananchi wa Mkoa wa Mtwara wafahamu kwamba, Serikali ililipa fedha zote za kununulia korosho za msimu wa 2018/2019 lakini baadhi ya watumishi na watu wasio waaminifu ndio waliokwamisha malipo hayo kwa manufaa yao binafsi.

“TAKUKURU Mkoa wa Mtwara ipo imara kuwafuatilia wale wote waliojihusisha na ubadhirifu huu ili warejeshe fedha walizoiba. Hatua kali dhidi ya wote ambao watakaidi agizo la kurejesha fedha walizochukua zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria ikiwa ni pamoja na kutaifisha mali za watuhumiwa kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashitaka.

“Kufuatia mafanikio haya ya TAKUKURU Mkoa wa Mtwara, leo tunayo furaha kuikabidhi Serikali kupitia Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Tanzania (CPB) fedha shilingi 600,000,000 zilizookolewa katika awamu hii ya kwanza ili zikatumike kuwalipa wakulima waliosalia.

“TAKUKURU Mkoa wa Mtwara imeelekeza nguvu zake katika kuhakikisha fedha shilingi 708,569,903.68 zilizobaki mikononi mwa watuhumiwa hadi sasa zinarejeshwa Serikalini na hatua kali za kisheria zinachukuliwa dhidi yao.

“TAKUKURU inaendelea kuwasihi wananchi wa mkoa wa Mtwara popote pale walipo, waendelee kutupatia taarifa za wale wote wanaojihusisha na vitendo vya rushwa ili tuhakikishe kwamba hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi ya wale wote wasiolitakia mema Taifa letu.

“Taarifa zinaweza kufikishwa kwetu kwa njia ya simu ya dharura 113 ambayo ni bure, pia Mwananchi anaweza kufika katika ofisi zetu zilizoko katika kila Mkoa, kila Wilaya na hata katika Vituo Maalum ambavyo vina mkusanyiko wa shughuli nyingi za kuichumi.

“TAKUKURU Mkoa wa Mtwara inatoa wito kwa Maafisa Ushirika ngazi ya Halmashauri, Viongozi Ushirika ngazi ya Mkoa, Wadau mbalimbali wa Ushirika na Bodi za Mazao kila mmoja kusimamia ipasavyo Sheria na Kanuni ili kuhakikisha ushirika unajengwa katika misingi imara na kuondoa matatizo ya rushwa na ubadhirifu wa mali unaoathiri wanachama wakiwemo wakulima wa korosho.

"Aidha, TAKUKURU Mkoa wa Mtwara inawaasa wananchi wote wa Mtwara kujiepusha na vitendo vya rushwa katika uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka huu wa 2020 na wahakikishe wanatumia vizuri kura zao ili kuwapata viongozi bora na wenye malengo mema na Taifa letu,"amefafanua Hayo yamebainishwa na Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Mtwara, Enock P.Ngailo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news