Amber Rutty, mpenzi wake, aliyesambaza picha jela kwa michezo michafu

Leo Septemba 25, 2020 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imemuhukumu Msanii Rutyfiya Abubakary (Amber Rutty), mpenzi wake, Said Bakary na James Charles (James Delicious) kulipa faini ya shilingi milioni 11 ama kwenda jela miaka mitano,anaripoti Mwandishi Diramakini.
Uamuzi huo umetolewa baada ya watuhumiwa hao kutiwa hatiani kwa makosa matatu ikiwemo kufanya mapenzi kinyume na maumbile huku wakishindwa kulipa faini hiyo kwa leo, hivyo wamepelekwa gerezani na endapo kama watalipa wataachiwa huru.

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Godfrey Isaya baada ya Mahakama hiyo kujiridhisha bila kuachwa kwa ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka. “Nimezingatia hoja za pande zote mbili na athari za makosa haya, ni kweli washitakiwa wote ni vijana na wanategemewa, nimeona mshitakiwa wa kwanza anajutia.
"Mshtakiwa wa kwanza, wa pili na watatu ni wakosaji wa kwanza, kutokana na mazingira ya kesi hii, adhabu yake ni miaka 30 kila kosa ambapo nikiwafunga mtapotea kabisa. Hivyo, kwa mazingira mliyoyasema na lengo la adhabu ni kujirudi, mshitakiwa wa kwanza utalipa shilingi milioni tatu ama jela miaka mitano, mshitakiwa wa pili utalipa faini ya shilingi milioni tatu ama jela miaka mitano na mshitakiwa wa tatu faini shilingi milioni tano ama jela miaka mitano, adhabu zitaenda sambamba,”Hakimu Mkazi Mfawidhi, Godfrey Isaya.

Kabla ya adhabu hiyo, Wakili wa Serikali, Faraja Nguka aliieleza Mahakama kwamba,hakuna rekodi za makosa ya nyuma juu ya washitakiwa hao.

Amesema, pia kutokana na makosa waliyotiwa nayo hatiani ni makosa ambayo yamezuiliwa hata na vitabu vitakatifu na yana madhara makubwa kwa jamii na hayana tiba, "tunaomba Mahakama iwape adhabu stahiki ili iwe fundisho kwa wengine,”amebainisha.

Wakati huo huo, katika utetezi Ambe Rutty amesema kwamba, anaiomba Mahakama impunguzie adhabu kwa ana watoto wanaomtegemea.

Amber Rutty amesema, mmoja kati ya watoto hao ana matatizo ya pumu na ana wazazi wake ambao wanamtegemea huku akibainisha kuwa, yeye mwenyewe anasumbuliwa na ugonjwa wa Kifua Kikuu.

Kwa upande wa Mshitakiwa Said Bakary ameiomba Mahakama isimpe adhabu kali kwani yeye ni mtoto mkubwa anayetegemea kwa familia ya watoto watatu.

"Mama yangu amezeeka na ninasumbuliwa na TB, natumia vidonge, Mahakama yako inionee huruma,”amesema Said Bakary mbele ya Mahakama hiyo.

Naye Mshitakiwa James Charles (James Delicious) kupitia Wakili wake amesema, “Naomba Mahakama itoe adhabu ndogo kwa sababu hajawahi kutiwa hatiani wala rekodi ya jinai.

"Pia alionyesha ushirikiano tangu shauri lilipofunguliwa mahakamani. Pia ni mtu aliyeonyesha utii na wito uliotolewa na RC aliutii na kufika Polisi. Pia mshitakiwa ni kijana mwenye umri mdogo, familia yake inamtegemea, pia ana mzazi mmoja,”amesema Wakili wake.

Aidha, katika hukumu hiyo, Hakimu Isaya amesema upande wa mashitaka ulikuwa na mashahidi 10, huku upande wa utetezi wakijitetea washitakiwa wenyewe.

Amesema, katika hukumu hiyo hoja kuu zilikuwa saba ikiwemo kama mshitakiwa Ambe Rutty ndiye aliyeonekana katika video ya ngono ama lah!, pia kama mshitakiwa huyo ameingiliwa kinyume na maumbile ama lah!, pia kama mshitakiwa Said alimuingilia kinyume Ambe Rutty .

Hakimu Isaya amesema kuwa, baadhi ya hoja hazikuwa na shaka ikiwemo iliyomuhusu mshitakiwa Ambe Rutty ambaye alipelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam na kufanyiwa vipimo sehemu ya nyuma na kubaini kuna tatizo.

Hata hivyo,katika kesi hiyo kosa la kufanya mapenzi kinyume na maumbile lilikuwa linamkabili Amber Rutty, ambapo anadaiwa amelitenda kati ama baada ya Oktoba 25, 2018 ambapo alimruhusu Said Bakary kumuingilia kinyume na maumbile, kosa ambalo amelikana.

Pia kosa lingine la kufanya mapenzi kinyume na maumbile linamkabili mshtakiwa wa pili Said Bakary ambapo anadaiwa kati ama baada ya Oktoba 25,2018 jijini Dar es Salaam alifanya mapenzi na Amber Rutty kinyume na maumbile ambapo amesema si kweli.

Kosa la tatu la kuchapisha video ama picha za ngono, ambapo linamkabili James Charles (James Delicious) akidaiwa kati ya Oktoba 25,2018 alisambaza video za ngono kupitia magroup ya Whatsapp jambo ambalo ni kinyume cha sheria na uvunjivu wa maadili.

No comments

Powered by Blogger.