BREAKING NEWS:Matatani kwa kukutwa akimchuna mbwa kwa ajili ya kuuza kitoweo

Mwanaume ambaye inadaiwa ni raia wa Uganda amekamatwa muda mfupi uliopita mjini Nimule baada ya kumuua mbwa na kuanza kumchinja kwa ajili ya kuwauzia nyama wananchi Sudan Kusini, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Kwa mujibu wa chanzo cha taarifa hii kutoka mjini Nimule kimeieleza Diramakini kuwa, mtuhumiwa huyo amechukuliwa na vyombo vya usalama kwa mahojiano zaidi.
Mtuhumiwa huyo ambaye inadaiwa anaendelea kuhojiwa katika Kituo cha Polisi Nimule nchini Sudan Kusini awali alikaririwa akisema kuwa, amefanya biashara hiyo kwa muda mrefu kwa ajili ya kujipatia kipato cha kujikimu kimaisha.

Amesema kuwa, "Siwezi kusema sasa ni kwa muida gani ambao nimefanya biashara hii ya kuuza nyama ya mbwa,"alidai mtuhumiwa huyo kabla ya kupelekwa katika kituo hicho.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi wa Nimule wamesema kuwa, huenda biashara hiyo huwa wanaifanya pia kwa kushirikiana na wenye mabucha ambao mara nyingi wamekuwa wakifanya biashara za kuuza nyama kwa njia za kimagendo.

Jitihada zaidi za Diramakini kupata ufafanuzi wa kina juu ya matukio yanayofanana na hayo katika mji wa Nimule uliopo Kaunti ya Magwi, Equatoria ya Mashariki nchini Sudan Kusini zinaendelea.
Matukio kama hayo inadaiwa yamekuwa yakijitokeza katika mji huo ambao unapakana na Mji wa Gulu nchini Uganda ambao unafikika kwa barabara kwa kutembea kilomita 120 kutoka Uganda, hivyo matukio ya biashara haramu huwa yanafanyika mara kwa mara kutokana na kukosekana kwa mifumo imara ya usalama nchini humo.

Inadaiwa, watu wengi huwa wanatoka Uganda kwenda mjini humo kufanya biashara mbalimbali kwa ajili ya kujiingizia kipato huku wengine wakifanya zile haramu ambazo zitawapatia fedha za haraka haraka.


No comments

Powered by Blogger.