Wafanyabiashara saba wenye ukwasi wa mabilioni zenye viashiria vya magendo, utoroshaji madini mikononi mwa TAKUKURU

Wafanyabiashara maarufu saba wa madini ya Tanzanite jijini Arusha wanashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) kwa tuhuma za kufanya biashara ya vito ya madini hayo kwa njia ya magendo na utoroshwaji nje ya nchi,anaripoti Mwandishi Diramakini.

Sambamba na ukwepaji kodi bila kuzingatia sheria,kanuni,taratibu pamoja na miongozo iliyopo katika biashara ya vito na madini hapa nchini.Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU,Brigedia John Mbungo amewataja wafanyabishara hao kuwa ni pamoja na Joel Mollel (Saitoti), Meneja wa kampuni ya kuuuza na kununua madini ya Gem and Rock Venture ya jijini Arusha na mke wake, Caren Mollel ambaye ni Mtanzania mwenye asili ya Asia.

Pia yumo Rakesh Kumar Gokhroo anayemiliki kampuni ya kuuza na kununua madini ya Colour Clarity  ya jijini Arusha.

Wengine ni pamoja na Daud Saimalie Lairumbe ambaye ni Wakili wa Kampuni ya Gem and Rock Venture kutoka kampuni ya Uwakili ya Northen Law Chambers Advocates & Legal Cunsultants ya jijini Arusha,George Paul Kivuyo (Lekoo) mchimbaji na mfanyabiashara wa madini na mshiriki wa kibiashara wa Saitoti.

Mkurugenzi huyo amewataja wengine ni pamoja na Naiman Emmanuel Mollel mchimbaji wa madini ya Tanzanite katika mgodi uliopo Mirerani unaomilikiwa na Kampuni ya Gems & Rock Venture ya jijini Arusha pamoja na Ezekiel Amon Laizer mchimbaji na mfanyabiashara wa madini na mshirika wa kibiashara wa Saitoti wa jijini Arusha.

Amesema kuwa, uchunguzi wa awali umebaini kuwa, wafanyabiashara Saitoti na Gokhroo kwa kushirikiana na wenzao hao watano wanatuhumiwa kufanya uchimbaji,ununuzi na usafirishaji haramu wa madini ya Tanzanite kutoka katika migodi ya madini hayo yaliyopo huko Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara bila ya kufuata sheria,kanuni na taratibu.
 
Brigedia Mbungo amesema kuwa, tuhuma zilizochunguzwa na zinazoendelea kuchunguzwa ni pamoja na watuhumiwa wote wamekuwa wakitumia rushwa kuwashawishi baadhi ya watendaji wa Serikali ili kufanikisha azma yao ya kupunguza thamani ya madini husika hivyo kuikosesha Serikali mapato kwa madini husika kupewa thamani ndogo.
 
Amesema, wafanyabiasha hao wamekuwa wakipata madini bila kufuata sheria,kanuni na taratibu wamekuwa wakiyauza nje ya nchi kinyume na taratibu na hivyo kuendelea kuikosesha serikali mapato stahiki.
 
Pia wamekuwa wakikwepa kulipa kodi halali ya serikali,wamewawezesha wafanyabiashara hao na wabia wao kutumia fedha hizo na kujijengea ukwasi mkubwa uliowawezesha kununua majengo ya kifahari na magari ya kifahari na kuanzisha biashara mbalimbali jijini Arusha pamoja na maeneo mengine nchini.
 
Amesema kuwa, ukwasi huo ambao uchunguzi unaendelea kuubaini na ambao unatuhumiwa kupatikana kwa njia zisizo halali,unakadiriwa kufikia shilingi bilioni 7.2 .

TAKUKURU imebaini kuwa ,mali kadhaa zinazomilikiwa na watuhumiwa ambazo taasisi hiyo inaendelea kuzifanyia uchunguzi kwani Saitoti ana mali na biashara katika maeneo mbalimbali jijini Arusha zenye thamani ya zaidi ya sh.bilioni 4.7,mke wake anamiliki nyumba na magari yenye thamani ya zaidi ya sh.milioni 610.

Brigedia Mbungo amesema Saitoti na mke wake Caren wanamiliki kampuni ya Azo Africa ambayo inamiliki mgodi,magari na mali nyingine zenye thamani ya sh.milioni 177.5 na kwa ujumla Saitoti anamiliki mali zenye thamani ya zaidi ya sh bilioni 5.5. 

Amesema mtuhumiwa Naiman Emmanuel Mollel anamiliki nyumba na magari yenye thamani ya zaidi ya sh.milioni 574,mfanyabiashara Gohkroo anamiliki magari,fedha taslimu pamoja na madini yenye thamani ya sh.milioni 895,mfanyabiashara Lekoo anatuhumiwa kumiliki nyumba na magari yenye thamani ya sh.milioni 227.
 
Amesema, watuhumiwa wote wanachunguzwa na tayari uchunguzi wake unaendelea vizuri na TAKUKURU kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali na watapelekwa katika vyombo vya sheria.

Amesema, endapo watatiwa hatiani,adhabu stahiki zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na utaifishwaji wa mali zao zilizotokana na ufanyaji wa biashara za madini ya vito kwa njia zilizo kinyume na sheria.
 
Brigedia Mbungo amewataka wafanyabiashara wa madini ya vito nchini kuwa serikali iko macho sana na haitakuwa na simile au huruma kwa yeyote atayekiuka sheria na kanuni za kufanya biashara ya madini hapa nchini.

No comments

Powered by Blogger.