Business Start Up Centre yasikia kilio cha wabunifu, wavumbuzi Tanzania

Kituo cha Biashara Zinazochipukia (IAA Business Start Up Centre) kilichopo Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kinatarajia kufanya tamasha kubwa la ubunifu na uvumbuzi liitwalo Arusha Innovation Summit mwezi Novemba, mwaka huu, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Tamasha hilo linalowalenga wadau wa ubunifu na uvumbuzi litatoa nafasi ya mijadala mbalimbali yenye lengo la kukuza ubunifu na uvumbuzi nchini.

Pamoja na mijadala, tamasha hilo litakuwa kilele cha mashindano ya uvumbuzi na ubunifu yaitwayo Arusha Innovation Challenge yanayoshindanisha vijana mbalimbali toka nchini Tanzania waliofanya ubunifu na uvumbuzi wa vitu mbalimbali.

Akizungumza na vyombo vya habari katika chuo hicho cha Uhasibu, msimamizi wa kituo hicho,Pamela Chogo amesema, mchakato wa vijana kushiriki kwenye mashindano ulianza Septemba 24,2020 kwa kuwawezesha vijana wanaopenda kushiriki kutuma maombi yao kwa njia ya mtandao kupitia tovuti ya www.startup.iaa.ac.tz.
Amefafanua kwamba, utaratibu wa jinsi ya kushiriki umeelezewa kwa undani kupitia tovuti hiyo.

Bi.Pamela amesema kwamba,kupitia tamasha na shindano hilo, wanaendelea kuhamasisha vijana kujiajiri kupitia ubunifu na ugunduzi wanaoweza kuufanya.

Kwa upande wake Mratibu wa Mashindano hayo,Sunday Massawe amesema kuwa washiriki wanaopaswa kushiriki mashindano hayo ni vijana kuanzia miaka 16 hadi 30 ambapo itawarahisishia vijana wenye ubunifu kuonyesha vipaji vyao ili kuweza kutambulika na jamii.

Amesema kuwa, wameamua kuwashirikisha vijana wote Tanzania walio vyuoni na walio nje ya vyuo na wa jinsia zote.

Amesisitiza kwamba, usajili umeshaanza na utafungwa Oktobs 23,mwaka huu na baada ya usajili kutakuwa na mchujo kwa hatua mbalimbali na mwisho kupatikana kwa mshindi. 

Mashindano hayo yamegawanyika katika makundi mawili ikiwa ni kundi la uvumbuzi kwenye Tehama (ICT Innovations) na kundi la uvumbuzi kwenye kitu cha kijamii au kibiashara (Social and business Innovations ).

Mwisho wa mchakato utatoa washindi watatu katika kila kundi ambao watapata zawadi.

Sunday amesisitiza kwamba, mashindano ni ya vijana wote na sio wasomi tu huku wanawake wakipewa kipaumbele.

Kwa upande wake mdau wa mashindano hayo ambayo ni Unisplash,Happy Mdenye amesema kuwa wamepata nafasi ya kuwa wadau ambapo watawafikia jamii kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii. 

Amesema,wataendelea kutoa taarifa za kuweza kushiriki na kuwakumbusha vigezo na masharti, pamoja na kuendelea kutoa elimu mbalimbali.

Amewataka vijana kuwa na mazoea ya kutumia fursa zinazojitokeza ili kuweza kujifunza masuala mbalimbali ya kuwajenga katika maisha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news