CCM yatoboa siri Mara; Samwel Kiboye, Prof. Muhongo,Shaibu Ngatiche wataja wanavyokwenda kufunga hesabu Oktoba 28

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Musoma Vijijini kimezindua kampeni zake za kuomba kura na kunadi sera za chama hicho kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu,anaripoti AMOS LUFUNGULO kutoka MARA.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Samwel Kiboye akionesha Ilani ya Uchaguzi leo Septemba 11, 2020 katika uzinduzi wa kampeni za uchaguzi Wilaya ya Musoma Vijijini, kulia kwake ni Mgombea Ubunge Jimbo la Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo. Picha na Amos Lufungulo/Diramakini.

Aidha, chama kimewaomba wananchi katika Jimbo la Musoma Vijijini kumchagua Mgombea Ubunge wao, Prof. Sospeter Muhongo,madiwani na Rais Dkt.John Maguli ili kiweze kuendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo jimboni humo.

Uzinduzi wa kampeni hizo umefanyika katika Kijiji cha Bwaikwitururu Kata ya Kiriba Wilaya ya Musoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama hicho akiwemo Katibu wa CCM Mkoa wa Mara, Shaibu Ngatiche,wagombea Ubunge Viti Maalumu Mkoa pamoja na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mara, Samwel Kiboye (Namba Tatu).
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Samwel Kiboye akimnadi Mgombea Ubunge Jimbo la Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo. Picha na Amos Lufungulo/Diramakini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hizo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Samwel Kiboye (Namba Tatu) amewahimiza wananchi wa jimbo hilo kumchagua Prof.Muhongo kutokana na kazi nzuri za maendeleo zilizofanyika katika jimbo hilo ikiwemo kubooresha huduma za kijamii elimu, afya na huduma za maji kwa ufanisi mkubwa.

Mafanikio ambayo yamewezekana kutoka na ushirikiano mkubwa chini ya uongozi wa Rais John Magufuli ambaye amewatumikia wananchi kwa moyo wa kujitoa kwa dhamana aliyepewa na Watanzania.
 

"Kazi alizofanya Rais Magufuli ni kubwa sana, barabara zimejengwa, elimu bure imetolewa na hata katika Mkoa wa Mara tumejengewa hospitali kubwa ya rufaa ambayo ni ya mfano itakayotoa matibabu ya kawaida na ya kibingwa, pia fedha za ujenzi wa uwanja wa Ndege Musoma zimetolewa, niombe wananchi wa Musoma Vijijini tumchague Magufuli na Prof.Muhongo kwa miaka mingine mitano, niombe watu wachache wanaobeza juhudi za Rais Magufuli muache mara moja kwa sababu kazi alizofanya zimeiheshimisha nchi kimataifa,"amesema Kiboye.
Kiboye ametoa onyo kali kwa baadhi ya wanachama wachache watakaobainika kukihujumu chama hicho katika kipindi hiki Cha Uchaguzi Mkuu, kwani hakitasita kumchukulia hatua kali za kisheria, kwani kufanya hivyo ni kukwamisha maendeleo ya wananchi na kizazi kijacho,huku akisisitiza umoja , mshikamano na uimara thabiti ili kushinda majimbo yote ya Mkoa wa Mara.

Naye Mgombea Ubunge Jimbo la Musoma Vijijini, Prof.Muhongo amesema kuwa , zipo baadhi ya changamoto zinazowakabili ikiwemo tatizo la watoto kukaa chini, ambapo amewaomba madiwani wote ifikapo mwezi Julai 2021 kila diwani ahakikishe katika kata yake hakuna changamoto hiyo.

Mgombea Ubunge Jimbo la Musoma Vijijini,Prof. Sospeter Muhongo akizungumza mbele ya wananchi na wagombea udiwani kata za Wilaya ya Musoma Vijini leo Septemba 11, 2020 katika uzinduzi wa kampeni za chama hicho Kata ya Kiriba. Picha na Amos Lufungulo/Diramakini.

Pia amesisitiza kwamba, atahakikisha anatanguliza mbele maslahi ya wananchi badala ya mtu mmoja mmoja pamoja na kushughulikia huduma za maji kupitia mradi mkubwa unaotekelezwa na Serikali wa Maziwa Makuu.

Mradi ambao utakuwa mwarobaini wa kutatua tatizo hilo pamoja na miradi mingine mikubwa ya maji itakayotekelezwa vijijini vyote ambavyo bado havitafikiwa katika jimbo hilo.

"Tuna sekondari 20, na shule za msingi 111 katika jimbo letu katika sekondari hizi hakuna hata sekondari moja yenye maabara ya kuridhisha, kwa hiyo haya ndiyo majukumu ambayo madiwani mkichaguliwa tuhakikishe yanatatuliwa, ajenda yetu kubwa iwe maendeleo, upande wa afya tunajenga zahanati 14, zote tuzimalize ndiyo shauku yetu.

"Pia mimi mwenyewe nimeamua kuwafanya wananchi waachane na jembe la mkono, ndiyo maana nimekuwa nikitoa plau, lengo ni kuboresha kilimo kiwe na tija, nitaendelea kufanya hivyo. Sambamba na kuweka maslahi ya jamii mbele siyo ya mtu mmoja mmoja,"amesema Profesa Muhongo.

Prof.Muhongo ameongeza kuwa, ipo miradi mbalimbali ambayo itatekelezwa ndani ya miaka mitano ndani ya jimbo hilo ikiwemo miradi ya ujenzi wa viwanda vidogo vidogo, kuboresha mazingira, kuwekeza katika kilimo cha tija, upanuzi wa kilimo cha umwagiliaji, uimarishaji huduma za majosho, zana bora za uvuvi, usalama wa wavuvi, ujenzi wa maabara na maktaba shuleni pamoja na kuimarisha uhakika wa masoko ili kufikia pato la shilingi 250,000 kwa mwezi kila mwananchi sawa na shilingi milioni tatu kwa mwaka.

Katibu wa CCM Mkoa wa Mara, Shaibu Ngatiche (kulia), kushoto kwake ni Mgombea Ubunge Jimbo la Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo wakifuatilia hotuba ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara Samwel Kiboye (hayupo pichani) katika uzinduzi wa kampeni zilizofanyika Kata ya Kiriba Wilaya ya Musoma. Picha na Amos Lufungulo/Diramakini.

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mara, Shaibu Ngatiche amesema, kutokana na mafanikio makubwa yaliyofanywa na Serikali ya Rais Magufuli kwa miaka mitano wananchi wana kila sababu ya kukichagua chama hicho katika majimbo yote ya Mkoa wa Mara na kata zote za Mkoa wa Mara katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu ili kiweze kuendeleza kuwaletea maendeleo wananchi.huku akibainisha kuwa tayari kata 32 wagombea wa udiwani wamepita bila kupingwa.

"Mkoa wa Mara una kata 178 na tayari kata 32 madiwani wamepita bila kupingwa, Serikali imetekeleza miradi mingi katika miaka mitano iliyopita, ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya Watanzania na Musoma Vijijini, mathalani Jimbo la Musoma Vijijini zahanati zimejengwa, shule za msingi, sekondari, umeme umepelekwa karibuni vijiji vyote vya jimbo hili, pamoja na kuimarisha upatikanaji wa madawati shuleni chini ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ambapo Mbunge alikuwa Prof. Muhongo na Rais ni John Magufuli,"amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news