CHAMA CHA WANAWAKE WAFANYABIASHARA TANZANIA (TWCC) CHAZINDUA TUZO ZA WANAWAKE WENYE VIWANDA NA BIASHARA NCHINI

*Lengo ni kutambua na kuheshimu wanawake waliofanikiwa na wale wanaochipukia katika sekta za viwanda na biashara

*Kujenga imani juu ya ujasiriamali na kuhamasisha wanawake wa vizazi vijavyo kuwekeza na kujishughulisha katika shughuli za viwanda na biashara

*Kusheherekea mafanikio wanayoyapata wanawake katika sekta za viwanda na biashara

CHAMA cha Wanawake wenye Viwanda na Biashara (Tanzania Women Chamber of Commerce -TWCC) kimezindua tuzo za wanawake waliofanya vizuri zaidi kwa mwaka 2020 katika sekta za viwanda na biashara, anaripoti MWANDISHI WETU kutoka DIRAMAKINI.

Tuzo hizi zimezinduliwa na Mwenyekiti wa TWCC,Jacquiline Maleko katika Hoteli ya Seashells iliyopo jijini Dar es Salaam. 
 Mwenyekiti Taifa, Jacqueline Maleko (wa pili kutoka kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa TWCC,Bi.Mwajuma Hamza (mwenye kitenge cha rangirangi kushoto) wakizindua rasmi tunzo hiyo.

Katika salamu zake za uzinduzi, Bi.Maleko amesema tuzo hizi zinalenga kuonesha mchango wa mwanamke mjasiriamali katika kukuza uchumi wa nchi na kuchochea maendeleo ya jamii. 

Ameongeza kuwa, wanawake ni nguzo muhimu sana katika maendeleo ya jamii yoyote na kwamba wanawake wana uwezo wa kufanya mapinduzi makubwa katika sekta ya viwanda na biashara endapo wataaminiwa na kupewa nafasi ya kufanya hivyo.

Aidha, Bi. Maleko ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha mazingira ya biashara nchini ambapo wanawake wengi wameweza kuanzisha biashara na viwanda vidogo ambavyo vimewaongezea kipato, kuzalisha ajira pamoja kuchangia katika kukua kwa uchumi wa nchi. 

Ameongeza kuwa,juhudi zinazofanywa na Serikali kwa sasa katika kuboresha mazingira ya biashara zinatia moyo na kuwaomba wadau wote kushirikiana na serikali hasa katika kutekeleza mpango wa uboreshaji wa mazingira ya biashara yaani “The Blueprint for Regulatory Reforms to Improve the Business Environment”.

Mchakato wa upatikanaji wa washindi wa tuzo unaratibiwa na kamati maalum inayoundwa na wajumbe kutoka taasisi za serikali na sekta binafsi. 
Mwenyekiti  Bi.Jacqueline Maleko akilezea kuhusu tunzo.

Ili kuweza kushiriki katika tuzo hizi wanawake wanatakiwa kujaza fomu maalumu ambazo kwa sasa zinapatikana bure katika tovuti ya TWCC www.twcc-tz.org, Ofisi za serikali za mikoa, halmashauri, ofisi za TWCC mikoa mbalimbali, SIDO na ofisi zote za TCCIA. 

Zoezi la kusajili washiriki wa tuzo litaendelea kwa kipindi cha mwezi mmoja na litafungwa Oktoba 9, 2020. 

Sherehe za utoaji wa tuzo kwa washindi zinatarajiwa kufanyika Novemba 28,2020 jijini Dar es Salaam. 

Utoaji wa tuzo hizo utaambatana na uzinduzi wa Jarida la Wanawake 100 Wajasiriamali waliothubutu (Tanzania Inspire & Impact Women Book) kitachotumika kutangaza kazi mbalimbali za wanawake wajasiriamali nchini.

Tuzo za mwaka huu zinafadhiliwa na TradeMark East Africa (TMEA) chini ya mradi wa kujengea wanawake uwezo wa kufanya biashara ‘’Capacity Building Project for Women Traders and entrepreneurs’’. 
Baadhi ya wanawake wajasiriamali na wanachama wa TWCC waliohudhuria uzinduzi wa tunzo hiyo.

TMEA wamekuwa wakifadhili TWCC toka mwaka 2016 kujenga uwezo wa wanawake kuuza bidhaa ndani ya Jumuiya ya Afrika mashariki. Kupitia mradi huu TMEA imeshafikia zaidi ya wanawake 3000 na ina mpango wa kufikia jumla ya wanawake 10,000 kupitia TWCC ifikapo mwaka 2023. 

TMEA imetenga zaidi ya shillingi bilioni mbili kufanikisha mradi huu wa kujengea uwezo wanawake wa Tanzania kufanya biashara.

No comments

Powered by Blogger.