DC Isabela Chilumba akabidhi cheti cha usajili chama kipya cha Msingi cha Ushirika wa Mazao Kimbango, awashauri wakulima

MKUU wa Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma,Isabela Chilumba amekabidhi Cheti cha Usajili wa Chama Kipya cha Msingi cha Ushirika wa Mazao Kimbango, anaripoti MWANDISHI DIRAMAKINI.

Chama ambacho kimesogeza karibu huduma ya kuuza mazao kwa wakulima wa Kijiji cha Kimbango Kata ya Luhangarasi wilayani Nyasa.

Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Isabela Chilumba akiwakabidhi Cheti cha Usajili viongozi wa Kimbango Amcos katikaViwanja vya Ofisi ya Serikali ya Kijiji cha Kimbango Kata ya Luhangarasi wilayani Nyasa Septemba 15, 2020. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Nyasa,Jimson Mhagama. (Picha na Ofisi ya DED Nyasa).

Makabidhiano yamefanyika katika Viwanja vya Ofisi ya Serikali ya Kijiji cha Kimbango wilayani hapa.

Akikabidhi Cheti cha Usajili, Mkuu huyo amewataka wananchi wa kijiji hicho na Wilaya ya Nyasa kwa ujumla, hususani vijana, kuongeza uzalishaji wa zao la kahawa, kwa kuwa ardhi ipo ya kutosha inayostawisha zao la kahawa ili kuongeza kipato ngazi ya kaya na Taifa kwa ujumla.

Chilumba amefafanua kuwa, wananchi wa Kijiji cha Kimbango wamefurahia kupewa Cheti cha Usajili wa Chama cha Ushirika cha Msingi, ambacho ilikuwa ni kero ya wananchi wa kijiji hicho kwa kuwa, awali walikuwa wanasafirisha mazao yao umbali mrefu.

Pia walikuwa wakiuza kwenye Chama cha Luhangarasi Amcos, lakini kwa sasa watakuwa wanauza katika chama chao ambacho kimepata usajili.

Ameongeza kuwa, wasifurahie kupata usajili tu peke yake bali waongeze uzalishaji wa zao hilo, kwa kuongeza mashamba mapya na kupanda mbegu bora za kisasa, ambazo huzalisha mazao mengi na kwa muda mfupi.

Badala ya kusubiri mashamba ya kurithi peke yake. Amewaagiza watendaji wa kata na kijiji kuhakikisha kila mkulima anaongeza uzalishaji wa zao la kahawa kwa kila msimu wa kilimo.

“Ndugu wakulima nimewaona leo mnafurahia kupewa cheti cha Usajili wa Chama chenu, lakini furaha hiyo isiishie hapa bali iwe fursa kwenu ya kuongeza uzalishaji wa zao la kahawa hapa kijini kwenu na Wilaya ya Nyasa kwa ujumla, hasa vijana kila kijana anatakiwa kuwa na angalau hekari mbili kwa kufanya hivi hata chama chenu cha ushirika kitakuwa na nguvu kwa kuwa kitakuwa na mazao mengi,”amesema.

Aidha, ametoa wito kwa viongozi wa chama hicho kuwa waaminifu na waadilifu katika kutekeleza majukumu yao kwa kulinda na kutunza fedha na mali ya chama ili wananchi wakipende chama chao, na kuongeza uzalishaji wa zao hilo.

Pia amewatahadharisha kuwa Serikali wilayani hapa ipo makini na itawachukulia hatua za kisheria viongozi wa vyama vya ushirika watakaohusika na wizi au upotevu wa fedha za wakulima.

Kwa upande wao wanachama na wakulima wa mazao katika kijiji hicho wamempongeza Rais John Pombe Magufuli kwa kuwawezesha wakulima kuuza mazao yao katika Vyama vya Ushirika ambavyo vinawakomboa kiuchumi na kuwaunganisha na huduma za kibenki kwa kuwa awali walikuwa hata benki hawakujui.

Aidha wamemwambia Mkuu wa Wilaya kuwa, wataongeza uzalishaji wa zao la kahawa ili waweze kuongeza uchumi wa kaya na Taifa kwa ujumla wake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news