Dkt.Hassan Abbasi:Ukitugusa na uongo wako tutakujibu;hatuna mizaha na Beberu, kazi yetu ni kutekeleza tu

Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Katibu Mkuu wa  Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt.Hassan Abbasi Said. 
 

Akaulizwa beberu ni nani? Akajibu: "Beberu hana rangi wala utaifa, beberu ni mtu, taasisi au taifa lolote ambalo tukiwa hatuna hospitali, barabara, madaraja, ndege na vingine muhimu kwa maendeleo wanatubeza; tukianza kuvijenga na kuvifanyia kazi wananuna na kujaribu kuhujumu na kuvibeza bila hoja; mtu wa namna hii awe Mtanzania au si Mtanzania ni beberu tu,"

Majibu hayo yanatokana na tabia za baadhi ya Watanzania ambao wameendeleza tamaduni za kuviona vitu vinavyotekelezwa na Serikali kuwa, havina tija yoyote huku wakati mwingine wakiamua kushirikiana na watu wa nje kutafuta kila mbinu kuhakikisha wanakwamisha juhudi hizo, Mwandishi Diramakini amebaini.

Ameyabaini hayo Septemba 23, 2020 wakati Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Katibu Mkuu wa  Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt.Hassan Abbasi Said akifanya mahojiano na Kituo cha Redio cha Times Fm kilichopo nchini Tanzania.

Kabla ya hapo, Dkt.Abbasi aliyataja mambo 10 ambayo yanatoa majibu sahihi juu ya kauli za upotoshaji ambazo mara nyingi zimekuwa zikiienezwa na watu hao ambao kwa sababu zao binafsi wamekuwa wakishirikiana na Mabeberu wenzao kukwamisha juhudi za maendeleo nchini. miongoni  mwa mambo hayo ni;

1. Wakati wanasiasa wakiendelea na kampeni za uchaguzi, Serikali bado ipo na kazi mbalimbali zinaendelea kama ilivyopangwa, sheria za nchi zipo na wasemaji wa nchi wapo, ukitugusa na uongo wako tutakujibu;

2. Miradi mbalimbali mikubwa na midogo inayolenga kuboresha maisha ya Watanzania inaendelea vyema na tutaendelea kutoa takwimu za kila mara kuhusu utekelezaji;

3. Kuhusu faida za ndege hili tumeshalieleza sana kwamba ndege ni ajira, hivyo zimeshaingiza zaidi ya ajira 400 za moja kwa moja, ndege ni mapato hivyo zimeshaongeza mapato ya Shirika na Serikali kutoka shilingi Bilioni 2.5 kwa mwezi hadi shilingi Bilioni 15 kwa mwezi na kodi zaidi zinalipwa zinazokwenda kuhudumia wananchi;

4. Kuhusu madai kwamba ndege zilinunuliwa bila uwazi wala bajeti yake haijulikani Dkt. Abbasi alihoji wanaotoa madai hayo kama wanaishi Tanzania au vipi?.

 Amesema, ununuzi ulikuwa kwa mujibu wa kifungu kipya cha 65A cha Sheria ya Ununuzi wa Umma (marekebisho ya 2016) ambayo inaruhusu, kwa nia ya kupata bei bora na thamani ya fedha, taasisi ya ununuzi kununua moja kwa moja kutoka kwa mtengenezaji wa bidhaa husika badala ya mawakala wanaopandisha bei;

5. "Kama kuna mtu alikuwa na wakala wake mfukoni katika ununuzi wa hizi ndege imekula kwao, Serikali imenunua moja kwa moja kutoka kwa watengenezaji wanaojulikana Kimataifa kama Boeing na Bombardia na sheria inaruhusu hivyo na ilipata bei ya chini kuliko hata zile zilizoainishwa kwenye tovuti zao,"amesema.

6. Kwamba ndege hizi haijulikani zinanunuliwa kwa fedha kutoka wapi, Dkt.Abbasi amesema, Watanzania waendelee kuwakataa wanaotoa hoja hizo dhaifu kwa kuwa ni matapeli wasiojua lolote linaloendelea nchini;

7. Akimwaga ushahidi wa bajeti za mwaka 2016/17, 2017/18 na 2019/20 kutoka Fungu 2006 na mradi namba 4294 (Acquisition of New Aircrafts-ATCL), Dkt Abbasi amesema kwa miaka takribani minne mfululizo Serikali imekuwa ikitenga wastani wa shilingi Bilioni 500 kwa mwaka na zinajadiliwa na zinapitishwa na Bunge kupitia fungu hilo, akashangaa wanaodai kuwa fedha za ndege hazijulikani zinatoka wapi kama ni watu wanaoishi Tanzania au ndio wamekuja nchini juzi kushangaa maendeleo yetu?.

8. Akaulizwa hoja kama hiyo kuhusu usiri katika ujenzi wa reli ya SGR na Mradi wa Umeme Rufiji na fedha zinakotoka Dkt. Abbasi akaainisha vipande vyote vya ujenzi wa reli na Mradi wa Umeme kuwa vilishindanisha wataalamu wa ndani na nje. 

Akatoa mfano mradi wa SGR Dar kwenda Moro walijitokeza washindani zaidi ya 40, Moro kwenda Makutupora walijitokeza washindani takribani 36 na sasa akawaalika "wenye watu wao" waache kupiga kelele bali wawalete washiriki zabuni iliyotangazwa Agosti, mwaka huu ya ujenzi wa SGR kwa kipande cha Mwanza-Isaka. 

Kuhusu mradi wa Umeme Rufiji amesema, zabuni ilitangazwa wazi na takribani makampuni manne yalishiriki kutoka mataifa ya Afrika, Ulaya na Asia;

9. Aidha, Dkt.Abbasi alizidi kusisitiza kuwa fedha zote za miradi hii zipo kwenye bajeti na zinapitishwa na Bunge kila mwaka huku akitaja mradi wa Rufiji kuwa mpaka sasa shilingi Trilioni 1.432 zimeshatolewa;

"Kuna wageni wengi nchini kwa sasa kwa hiyo tuwavumilie, mtu anahoji hela za SGR hazijulikani zinatoka wapi, nataka tuamini yeye ndiye hajulikani ametoka wapi na anataka nini, anayehoji hii akasome fungu 2005, mradi namba 4281 kwenye Sekta ya Uchukuzi aone kila mwaka Bunge liliidhinisha shilingi ngapi kwa miradi ya SGR kuanzia mwaka 2017/18,"amesema na kuwataka Watanzania kuwapuuza waropokaji wanaoumizwa na maendeleo yanayotokea.

10. Akasisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea kutekeleza mambo makubwa yenye mwangwi mkubwa katika kuwanufaisha Watanzania na kuwataka Wananchi kuendelea kutimiza wajibu wao na kuwakataa mabeberu na mawakala wao.

No comments

Powered by Blogger.