Dkt.Shein:Urais sio asali kila mtu ailambe, Urais ni kazi na Dkt.Mwinyi kazi hiyo anaiweza

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Ali Mohamed Shein amesema kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimewaletea kiongozi mchapakazi na mwenye uwezo kuwa kuwa Rais wa Zanzibar ambaye ni Dkt.Hussein Ali Hassan Mwinyi, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Dkt.Shein ameyasema hayo leo Septemba 27,2020 katika mkutano wa Kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) huko Gando, Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba, ambao ulihudhuriwa na maelfu ya wanaCCM.

Amesema, sifa za Dkt.Mwinyi za nidhamu, uhodari wa kazi, kuwajali watu wote na ubobevu wa uongozi, sifa hizo hana mgombea mwingine yeyote kwa nafasi yoyote kutoka vyama vya upinzani.

Rais Dkt.Shein ameeleza kuwa, Dkt.Mwinyi ni kiongozi anaejali shida za watu na ambaye ameweza kushika nafasi mbalimbali katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Ali Mohamed Shein akihutubia wananchi wa Wilaya ya Wete Pemba na kumuombea kura Mgombea wa Urais wa Zanzibar, Dkt.Hussein Mwinyi na Rais wa Tanzania, Dkt.John Magufuli na wabunge, wawakilishi na madiwani mkutano uliofanyika Uwanja wa Mpira Gando leo Septemba 27,2020.(IKULU).

"Kazi iliyofanywa na mikutano yote ya CCM na kisha kupatikana kwa mgombea huyu Dkt.Hussien Mwinyi haikukosea, maana uchapakazi wake unaonekana kila pale anapokabidhiwa madaraka,’ameeleza.

Hata hivyo, Rais Dkt.Shein ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar amesema kuwa, yeye anayajua vyema majukumu ya urais kutokana na ugumu wake, na jinsi anavyomfahamu Dkt. Mwinyi, basi anaweza kuifanya kazi hiyo bila wasiwasi.

“Urais sio asali kama kila mtu ailambe, Urais ni kazi na Dkt.Mwinyi kazi hiyo anaiweza,"amesisitiza Dkt.Shein.

Aidha, ameeleza kuwa, Dkt.Mwinyi ndiye mgombea pekee ambaye anafaa kwa asilimia 100 kuwa rais wa Zanzibar, hasa kwa busara zake na utii wa kazi.

"Dkt. Mwinyi anafaa kwa asilimia 100 kuwa rais, maana mimi nauwelewa sana na sijaona kiongozi mwingine anaeuweza baada ya mgombea aliyetuliwa na CCM,’’amefafanua.

Hivyo, Rais Dkt.Shein amewataka wananchi na wanaCCM kumpigia kura Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Mgombea wake Mwenza, Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani wote wa CCM.

Mwanachama wa Chama cha ACT-Wazalendo, Bi.Rahma Sheha Hamad akitangaza kukihama Chama cha ACT- Wazalendo wakati wa Mkutano wa Kampeni ya CCM kumnadi Mgombea Urais wa Zanzibar, Dkt.Hussein Mwinyi uliofanyika katika uwanja wa Mpira Gando Wilaya ya Wete Pemba.(IKULU).

Amesema kuwa, dhamira ya CCM kila siku ni kuona wananchi wake wanaishi kwa amani na utulivu, hivyo ili hilo litekelezeke ni kuwapigia kura wagombea wa chama hicho cha CCM.

Sambamba na hayo, Rais Dkt. Shein amesema kuwa, Dkt.Hussein Mwinyi ndiye kiongozi pekee anayegombea nafasi ya Urais wa Zanzibar kuwa Rais wa Zanzibar anayeweza kuyalinda, kuyatetea na kuyadumisha Mapinduzi ya Januari 12, 1964 pamoja na kuutunza Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

“Siku ya tarehe 28, Oktoba mwaka huu, siku hiyo ya kupiga kura ikifika, muhakikishe hamfanyi makosa, na muwapigie kura rais John Pombe Magufuli, Dkt.Hussein Mwinyi, wabunge, wawakilishi na madiwani wetu wote,’’amesisitiza.

Naye Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema, iwapo wananchi wa Zanzibar watampa ridhaa ya kushika nafasi hiyo, atahakikisha, anasimamia uwajibikaji na watakoshindwa atawawajibisha, ili mafanikio ya kweli yapatikane.

Dkt. Mwinyi amesema, hayo ndio kipaumbele chake cha kwanza mara atapomaliza kuapishwa, kwani mambo hayo ni miongoni mwa yanadhoofisha kwa kiasi kikubwa maendeleo ya jamii.

Mgombea huyo wa urais, aliyasema hayo Jimbo la Gando wilaya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba, alipokuwa akizugumza na mamia ya wana CCM na wananchi wengine, kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni wa chama hicho.

Ameongeza kuwa, serikali atakayoiongoza hatapenda hata kidogo kuona ndani yake kuna watendaji wasiopenda kuwajibika, kwani wanakuwa kikwazo kufikia maendeleo yaliokusudiwa.

Amesema kuwa, jambo hilo ni adui mkubwa wa kufikia maendeleo ya Zanzibar, na kuendelea kudumaa kwa baadhi ya sekta, jambo ambalo halikubaliki na atalisimamia kwa dhati.

“Mkinichagua kuwa Rais wa Zanzibar, pamoja na mambo kadhaa ambayo ntawafanyia, lakini suala la uwajibikaji ndio kipaumbele cha kwanza, na akitokezea mtendaji kushindwa kuwajibika, nitamuwajibisha,’’amesisitiza.

Aidha, Mgombea huyo wa Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dkt.Hussein Ali Mwinyi, amewaahidi wananchi wa Zanzibar kama akipata ridhaa, atahakikisha anaimarisha miundombinu ya barabara, ili iwe ya kisasa zaidi.

Amesema, barabara ambazo ataanza nazo kwa kisiwani Pemba, ni ile ya Chake Chake-Wete yenye urefu wa kilomita 21, Finya-Kicha yenye urefu wa kilomita 8.8 na zile ndani ya mji wa Wete zenye urefu wa kilomita 9.

Amesema kuwa, ili Zanzibar ipige hatua kubwa kwenye maendeleo ya sekta ya utalii, viwanda, uvuvi inategemea sana uwepo wa barabara za kisasa, katika maeneo yote ya Unguja na Pemba.

Amesema, ingawa tayari Rais wa Zanzibar Dkt.Ali Mohamed Shein anaemaliza muda wake, ameitekeleza kwa kiwango kikubwa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 ambapo na y ye ameahidi kuitekeleza vyema ile ya 2020-2025.

“Kila mmoja ni shahidi kuwa, Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 Dkt.Shein, ameitekeleza kwa asilimia 100, karibu kila sekta na mimi mkinichagua, nitazidi kuziimarisha na kuendeleza,’’amefafanua

Mgombea Ubunge Jimbo la Gando, Salum Mussa omar akiwaombea kura wagombea wenzake katika mkutano wa kampeni za CCM uliofanyika leo Uwanja wa Mpira wa Gando Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba. (IKULU).

Pia, Mgombea huyo amewaahidi wananchi kuwa atawafanyia, ni kupiga vita suala la udhalilishaji pamoja na dawa za kulevya, ambapo amesema matatizo hayo amekuwa akielezwa kila anapopita katika kapeni zake za urais anazozifanya wakati akiwatembelea wananchi mbalimbali Unguja na Pemba.

Ameeleza kuwa, tatizo hilo linamnyima usingizi na ndio maana mara akichaguliwa. atahakikisha anafanya kila mbinu kuona udhalilishaji na dawa za kulevya, zinakuwa historia Zanzibar.

Aidha, mgombea huyo wa urais amesema, kutokana na mengi ambayo aliyafanya rais anayemaliza muda wake, kazi yake itakuwa ndogo mara akiingia madarakani ambapo alieleza kuwa tayari Dkt.Shein ameliimarisha zao la karafuu na kusababisha kuvunwa kwa tani 3,321 mwaka 2015 na kufikia tani 8,277 ambazo ni nyingi mno.

Aidha, amesema, eneo jingine ambalo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa ni sekta ya elimu kwa kujengwa skuli za ghorofa za Kizimbani, Limbani na ile Chasasa pamoja na chuo cha amali kilichopo Daya wilaya ya Wete.

Kuhusu kuliimarisha zao la mwani, Dkt.Mwinyi amesema, tayari Serikali ya Awamu ya Saba, imeshaanza ujenzi wa kiwanda cha kusarifia mwani, eneo la Chamanangwe sambamba na kuwakabidhi vihori 80 wakulima wa mwani wa Wilaya ya Wete.

‘’Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020, lazima nikiri kuwa ilipata msimamizi Dkt Shein, maana hata sekta ya utalii imeimarika kwa kuongeza watalii kufikia laki tano kutoka watalii 37,900 mwaka 2015,’’amesisitiza.

Katika hatua nyingine, mgombea huyo wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, amewataka wananchi wa Zanzibar kuhakikisha kura zao hawazipotezi, kwa kuvipa vyama ambayo havina muelekeo.

Amesema, CCM ndio chama kinachojali maisha ya watu wote wakiwemo wanyonge, wakulima na wakwezi hivyo, dhamira hiyo haiwezi kuendelezwa na kiongozi yeyote, isipokuwa anaetoka CCM.

‘’Tupeni ridhaa sisi wagombea wote wa CCM, ili tuendelee dhamira na ari ya kweli ya kuwatumikia, pasi na kujali maeneo mnayotoka wala rangi, na hii ndio shabaha ya waasisi wa taifa hili,’’ameeleza Dkt. Mwinyi.

Mapema Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Abdalla Juma Mabodi alisema, ushindi wa CCM hauna shaka, kutokana na kuitekeleza vyema Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020.

‘’Leo kutoka mjini Wete hadi kijiji cha Gando, unatumia dakika zisizozidi 20, maana barabara imejengwa tena kwa kiwango cha lami, hayo ndio mambo ya CCM,’’amesema Dkt.Mabodi.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mberwa Hamad Mberwa ametoa pongezi kwa Rais Dkt. Shein kwa maendeleo makubwa yaliyopelekwa na katika mkoa huo na Serikali anayoiongoza Dkt. Shein.

Wagombea nafasi Udiwani CCM walipokuwa wakitambulishwa katika mkutano wa kampeni za CCM uliofanyika leo Septemba 27,2020 Uwanja wa Mpira wa Gando Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba. (IKULU).

Nao wagombea Ubunge, Uwakilishi na Udiwani wa Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba walitambulishwa na Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar ambapo walitumia fursa ahiyo kuomba kura na kuwataka wananchi na wanaCCM wote kuwachagua ili wazidi kupeleka maendeleo katika maeneo yao.

Viongozi mbalimbali wa CCM walihudhuria akiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, Waziri Kiongozi Mstaafu Shamsi Vuai Nahodha pamoja na viongozi wengine wa CCM.

Mkutano huo wa kampeni ulikwenda sambamba na burudani kadhaa zilizotolewa na wasanii mbalimbali wakiwemo wale wa kizazi kipya pamoja na wakongwe kama vile Bi Fatma Issa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news