John Shibuda: Wapiga kura jitokezeni kwenye mikutano ya kampeni kwa vyama vyote

Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya siasa nchini, John Shibuda ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanajitokeza kwenye mikutano ya kampeni za wagombea wa vyama vyote vya siasa ili kusikiliza hoja na kisha kufanya maamuzi sahihi itakapofika Oktoba 28, mwaka huu ambayo ndio siku ya kupiga kura kuwachagua madiwani, wabunge na Rais, anaripoti Fatma Ally (Diramakini) Dar es Salaam.
Ameyasema hayo leo Septemba 25,2020 jijini Dar es Salaam alipokuwa akielezea hali ya kampeni za uchaguzi mkuu ambao unatarajiwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu.

Pia ametumia nafasi hiyo kuzungumzia mambo mbalimbali yanayoendelea nchini.

Shibuda amesema, ni vema wananchi wakaenda kusikiliza sera na hoja za wagombea wa vyama vyote na kisha watakuwa na maamuzi sahihi ya kutambua nani ana sifa za kuongoza nchi ifikapo Oktoba 28, mwaka huu.

"Siku ya kupiga kura mkapate nguvu ya kufanya uamuzi sahihi, wagombea wapo 15, nani ana sifa bora, nani ana weledi,nani ana elimu ya uraia kutekeleza yale ambayo Baba wa Taifa aliyaanzisha.

"Taifa letu lina majibu ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, Watanzania tukumbuke historia inafundisha, uchaguzi mwaka 2015 tulidai mabadiliko, tulidai mageuzi hatukujua yana ladha chungu, lakini kuna mafanikio ambayo yametendeka.

"Serikali ya Awamu ya Tano tunajua kuna mafanikio ambayo yamefanyika, lakini CCM imejikosesha yenyewe kwa kutokuwa na mikutano ya hadhara.Hivyo nashauri baada ya uchaguzi mkuu mwaka huu, kuwepo na utaratibu wa vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara,"amesema Shibuda.

Amefafanua kuwa,wananchi kutopiga kura ni makosa, hivyo amewaomba wajitokeze kwani wasipojitokeza ni janga la Taifa.

"Uchaguzi ni ufunuo wa kuwatambua wanaopenda maslahi ya Taifa. Nendeni mkapige kura muamue nani anafaa kuwa kiongozi katika nchi yetu,"amesema Shibuda.

Pia amefafanua kuwa,kama wapiga kura watapenda porojo na wakaogopa ladha chungu, watakwenda kupata wachumia tumbo na wasije kulalamika mirija ikirejea ya kunyonywa kwa Taifa letu na kwamba wakumbuke ukweli huchelewa kukomaa masikioni.

Amewataka wanasiasa wa vyama vyote na hasa wanaogombea kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge na urais kuhakikisha wanakuwa na lugha ambazo zinaunganisha Taifa badala ya kusababisha uvunjifu wa amani iliyopo nchini pamoja na kujenga chuki miongoni wa jamii ya Watanzania.

"Wanasiasa na wagombea tengenezeni mashindano ya hoja kujenga ambazo zina maslahi kwa Taifa letu badala ya kuwa na siasa za uongo na uzushi ambazo madhara yake ni makubwa.

"Hizo ndio nasaha zangu kwa wagombea kuanzia ngazi ya Udiwani, Ubunge na Urais ,ikumbwe uongo wa siasa huanda dhuluma dhidi ya vizazi na vizazi.Kwa hiyo wagombea wote wakumbuke ukweli una thawabu kwa Mwenyezi Mungu, ukweli huzaa haki dhidi ya dhuluma,"amesema Shibuda.

Amesisitiza kila chama cha siasa, kila mwanachama ajifanyie ukaguzi na kujitathimini ili kujitambua na kujiongeza na kujisahihisha kwa lengo la kufanya siasa safi hapa nchini.

"Wagombea upukeni kugeuza michakato ya kunadi sera kuwa mipango mikakati ya makusudi ya kutoleana lugha za kugombanisha na kuvuruga umoja wa jamii yetu ya watanzania,"amesema huku akivitaka vyombo vya ulinzi nchini katika kipindi hiki cha kampeni na kuelekea uchaguzi mkuu kufanya kazi yao kwa weledi ili kuhakikisha nchi ibaki salama kabla na baada ya uchaguzi huo wa Oktoba 28, mwaka huu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news