Kasi ya TAKUKURU yatoa tabasamu Arumeru, mamilioni ya fedha yarejeshwa, DC Muro awaonya wazee wa mikopo umiza

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) wilayani Arumeru imekabidhi jumla ya shs 21,700,000 kwa wananchi saba wilayani Arumeru, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mkuu wa TAKUKURU wilayani Arumeru, Deo Mtui amesema, kiasi cha shilingi 21,700,000 zimekabidhiwa kwa wananchi saba ambapo kiasi cha sh.7,500,000 kimekabidhiwa kwa walimu sita wa Shule ya Sekondari Mariado.
Walimu hao ni Abdallah Marambo,Ezekiel Mwaipopo,Andrew Mike,Samson Hamza,Christina Lekashu na Ellen A. Lomau ikiwa ni mishahara yao ambayo hawakulipwa na mwajiri.

Kiasi cha shilingi milioni 14,000,000 kimekabidhiwa kwa Emmnuele Vumilia Kilembe ambaye alidhulimiwa katika mauzo ya gari lake kinyume na mkataba wa mauziano.

Aidha, Mtui ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuiamini TAKUKURU na endapo wana malalamiko ambayo wanasadiki ni malalamiko ya kweli, wasisite kufika TAKUKURU na kama ilivyo ada, TAKUKURU itayafanyia kazi na kuhakikisha wanapata haki yao. 

Mkuu wa wilaya hiyo, Jerry Muro amesema Serikali haitamfumbia macho yeyote anayewadhulumu wananchi ambapo amemwagiza Mkuu wa TAKUKURU wilaya hiyo kumkamata mtu mmoja ndani ya saa 48 anayedaiwa kuwa chanzo cha migogoro ya ardhi kwa kuuza ardhi kwa mtu zaidi ya mmoja.

Muro amewaonya wanaofanya biashara ya mikopo kinyume na taratibu, kwani wamekuwa wakiwanyanyasa wananchi kwa mikopo yenye riba kandamizi sambamba na kuchukua vitambulisho vya taifa vya wananchi hao.

"Ni muhimu kusajili biashara ili iwe halali na kufanyika kwa kuzingatia taratibu,”amesisitiza Muro.

Wananchi waliopata haki kwa kukabidhiwa fedha zao wameishukuru Serikali kutetea haki za wanyonge ambapo Mwalimu Abdalah Malambo ameushukuru uongozi wa wilaya na kukiri kunufaika na sera ya Rais Dkt.John Pombe Magufulu ya kujali wanyonge.

Naye Emanuel G. Kilembe ambaye amekabidhiwa sh.14,000,000 kama mauzo ya gari lake amesema amefarijika sana na utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano kwani neno Hapa Kazi Tu linatekelezwa kwa vitendo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news