Kaskazini, Magharibi, Mashariki hadi Kusini maji safi ni tele kwa tele kasi yaongezeka, Mtwara kuchele, tabasamu kila konaRais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akishika maji ya bomba mara baada ya kuzindua mradi mkubwa wa Maji wa Kibamba-Kisarawe mkoani Pwani, uzinduzi huo ulifanyika Juni 28, 2020, kabla na baada ya hapo miradi ya kihistoria ya maji kuanzia Kanda ya Kaskazini, Mashariki, Magharibi na Kusini imekuwa ikitekelezwa kwa kasi na imeleta matokeo chanya kwa mamilioni ya Watanzania waishio vijijini na mijini.
HUDUMA YA MAJI KATIKA MANISPAA YA MTWARA YAZIDI KUIMARIKA

Wizara ya Maji imeridhika na utekelezaji wa miradi ya maji inayoendelea katika Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara baada ya timu ya ufuatiliaji na tathmini kutoka Wizara ya Maji ikiongozwa na Mkurugenzi wa Huduma ya Ubora wa Maji, Philipo Chandy kuanza kazi ya ukaguzi wa miradi mkoani humo, Mwandishi Diramakini anakujuza.

Akitoa tathimini baada ya ukaguzi wa miradi hiyo, Mkurugenzi Chandy amesema, kazi kubwa imefanyika katika Manispaa ya Mtwara, huku akipongeza hatua mahsusi zilizochukuliwa kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa majisafi na salama pamoja na kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wizara ya Maji, Prisca Henjewele akitoa elimu kwa msimamizi wa miongoni mwa vituo vya kuchotea maji vya Mradi wa Maji wa Lukuledi unaotoa huduma kwa wakazi 17,060 katika vijiji vitano vya Halmashauri ya Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara.

Mkurugenzi Chandy ameridhishwa na kazi nzuri usimamizi miradi katika manispaa hiyo inayofanywa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mtwara (MTUWASA) na kuitaka iongeze mtandao waweze kutumia vizuri maji katika chanzo cha Mtawanya chenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 15 kwa siku wakati kwa sasa zinatumika lita milioni 7 pekee kwa siku.

Amesema kuwa, pamoja na mpango wa kuongeza uzalishaji wa maji kupitia vyanzo vya maji vya Mchuchu na Mjimwema kutaongeza kiwango cha uzalishaji na kukidhi kwa asilimia kubwa mahitaji ya lita milioni 18 kwa siku katika mji wa Mtwara unaokuwa kwa kasi kimaendeleo.
Miongoni mwa vituo vya Mradi wa Maji wa Lukuledi vikitoa huduma katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara.

Katika hatua nyingine Kaimu Mkurugenzi MTUWASA, Mhandisi Festo Fulgence amesema, lengo ni kufikisha asilimia 95 ya upatikanaji wa maji mjini na kwa kuongeza uzalishaji wa maji kutawawezesha kuongeza mtandao zaidi na kufikisha maji kwa wateja wengi zaidi kwa saa 24, ambapo kwa sasa ni asilimia 85.

Akitoa shukrani zake kwa Wizara ya Maji kwa kutoa zaidi ya sh.Bilioni 5 kwa MTUWASA kwa ajili ya utekelezaji wa miradi katika wilaya mbalimbali katika Mkoa wa Mtwara.
Kiongozi wa Timu ya Wataalam wa Wizara ya Maji, Mkurugenzi Philipo Chandy (aliyekaa) akiwa pamoja na Timu ya Wataalam ya Wizara ya Maji katika Chanzo cha Maji cha Mbwinji katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara.

Mhandisi Fulgence amesema utekelezaji wa miradi inayoendelea katika Manispaa ya Mtwara inajumuisha ujenzi wa chujio, kuongeza uzalishaji wa maji katika chanzo cha maji Mchuchu, kuboresha maji katika maeneo ya Mangamba, Mtawanya na Lwelu iko katika hatua nzuri jambo linalotoa matumaini kwa wakazi wa Manispaa ya Mtwara na vitongoji vyake kupata huduma ya uhakika ya majisafi na salama.

BILIONI 24 KUINUA KIWANGO CHA HUDUMA YA MAJI MTWARA VIJIJINI

Wakati huo huo, Serikali imetenga kiasi cha shilingi Bilioni 24 kwa ajili ya kazi ya ujenzi wa miradi ya maji katika vijiji 205 ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa ahadi ya kumaliza tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji kwa wakazi wa maeneo ya vijijini mkoani Mtwara, ambao kati yao asilimia 60.1 wanapata huduma.
Mhandisi Joshua Lawrence wa Wizara ya Maji akikagua baadhi ya mashine zinazotumika katika chanzo cha Maji cha Mitema katika Halmashauri ya Wilaya ya Newala, mkoani Mtwara.

Meneja wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoa wa Mtwara, Mhandisi Mbaraka Ally amesema fedha hizo zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 31 itakayonufaisha wakazi zaidi ya 300,000 katika vijiji 205 kwa mwaka huu wa fedha wakati akitoa taarifa kwa Wataalam wa Wizara ya Maji wakiwa katika ufuatiliaji na kutathmini ujenzi wa miradi ya maji ya Kilidu Mnui na Mnolela katika Wilaya ya Newala.

“Kati ya Sh. bilioni 24 zilizotengwa, tumeshapokea Sh. bilioni 8 na zimeanza kutumika kwenye ujenzi wa Mradi wa Maji wa Kilidu Mnui ambao umeshakamilika kwa gharama ya zaidi ya Sh. bilioni 1.4, ukiongeza lita 720,000 kwa siku na kuhudumia wanachi 60,000 wa Newala mjini na vijiji jirani, changamoto iliyopo ni umeme ambapo tayari tumeshachukua hatua ya kubadilisha mita ya LUKU na baada ya muda mfupi mradi utaanza kutoa huduma,’’amesema Mhandisi Ally.
Wataalam wa Wizara ya Maji wakikagua maendeleo ya kazi ya ya uboreshaji wa Chanzo cha Maji cha Mbwinji katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara.

“Vilevile Mradi wa Maji wa Mnonela umefikia asilimia 45 na utakamilika mwezi Desemba, 2020 kwa gharama ya zaidi ya sh.milioni 400 na kuhudumia wakazi 2,805 wa vijiji vya Dodoma, Mkunjo, Mtanda na Mnonela katika Halmshauri ya Wilaya ya Newala inayopata huduma ya maji kwa asilimia 55,” amefafanua Mhandisi Ally.

Aidha, wakazi 17,060 wa vijiji vya Lukuledi, Nasindi, Polapola, Kalinga na Napata wameanza kupata huduma ya majisafi na salama mara baada ya Mradi wa Maji wa Lukuledi kukamilika kwa asilimia 95 kwa kiasi cha zaidi ya Sh. milioni 600 na kumaliza kilio cha muda mrefu.
Ujenzi wa tenki la Mradi wa Maji wa Mnolela ukiendelea katika Halmashauri ya Wilaya ya Newala mkoani Mtwara.

Mkurugenzi wa Huduma ya Ubora wa Maji, Philipo Chandy ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Masasi-Nachingwea (MANAWASA) kwa kazi ya uboreshaji wa Chanzo cha Maji cha Mbwiji katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi.

Amesema kuwa, maendeleo ya ujenzi ni mazuri na utakapokamilika utaimarisha zaidi huduma ya maji kwa wananchi waishio katika wilaya za Masasi mkoani Mtwara, Nachingwea na Ruangwa mkoani Lindi.

No comments

Powered by Blogger.