Humphrey Polepole:Mzunguko wa kampeni unaanzia Iringa kesho

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole amesema,Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Magufuli kesho ataendelea na mzunguko wake wa mikutano ya kampeni kwa ajili ya kunadi sera na ilani ya Uchaguzi kwa Watanzania mkoani Iringa, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Lengo likiwa ni kuwaomba Watanzania ifikapo Oktoba 28,mwaka huu wampe kura za kishindo ili akatekeleze miradi aliyoianza, inayoendelea na mingine mipya kwa ajili ya maendeleo yao na Taifa.

Polepole ambaye alikuwa anazungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Septemba 27,2020 amesema, Dkt.Magufuli ataondoka jijini Dodoma kuelekea Iringa kuendelea na kampeni.

Amesema, Dkt.Magufuli anatarajiwa kuwa na mikutano ya njiani, kwani uzoefu unaonesha mara nyingi wananchi hujitokeza kwa ajili ya kumuona.

Amesema, katika mikutano hiyo ambayo maelfu ya wananchi huwa wanajitokeza, mgombea wao huwa anaitumia kuwaombea wagombea ubunge na madiwani kura.

Polepole amesema, Dkt.Magufuli atakuwa anatumia gari hadi Uwanja wa Samora mjini Iringa ambapo atafanya mkutano mkubwa.

Amesema, Dkt.Magufuli atakuwepo yeye na viongozi wengine wa Chama Cha Mapinduzi, viongozi wa chama Mkoa wa Iringa, wagombea udiwani,ubunge, Wana CCM na wananchi mbalimbali.
Mbali na hayo amesema,Dkt.Magufuli Septemba 29,mwaka huu ataelekea mkoani Mbeya na kabla ya kufika huko atakuwa na mkutano mkubwa mjini Makambako, Njombe.

Amesema Septemba 30,mwaka huu Dkt.Magufuli atakuwa na mkutano mkubwa jijini Mbeya.

No comments

Powered by Blogger.