Dkt.Hussein Ali Hassan Mwinyi kujikita katika uchumi wa bluu, Rais Shein asema ni mtu asiyejikweza, Zanzibar itastawi

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein amewataka wana CCM pamoja na wananchi wote wa Zanzibar kumchagua Dkt.Hussein Ali Hassan Mwinyi kuwa Rais wa Zanzibar kwani ana sifa zote za Urais, anaripoti MWANDISHI WETU kutoka DIRAMAKINI.

Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Hassan Mwinyi akiwapungia mkono wanachama wa CCM alipowasili katika viwanja vya Kibanda Maiti (Uwanja wa Demokrasia Kibanda Maiti ) wakati wa hafla ya uzinduzi wa kampeni za CCM leo mchana Septemba 12, 2020.(Picha na Ikulu/Diramakini).

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein akisalimiana na Rais Mstaafu wa Tanzania, Mzee Ali Hassan Mwinyi, alipowasili katika Uwanja wa Demokrasia Kibanda Maiti jijini Zanzibar kuhudhuria Mkutano wa Ufunguzi wa Kampeni za CCM Zanzibar .(Picha na Ikulu/Diramakini).Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Hassan Mwinyi akimsalimia Mama Fatma Karume alipowasili katika Uwanja wa Demokrasia Kibanda Maiti jijini Zanzibar, wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Kampeni za CCM.(Picha na Ikulu/Diramakini).

Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Abdalla Juma Mabodi akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar,Dkt. Ali Mohamed Shein, kufungua Mkutano wa Uzinduzi wa Kampeni za CCM Zanzibar zilizofanyika katika Uwanja wa Demokrasia Kibanda Maiti jijini Zanzibar. (Picha na Ikulu/Diramakini).

Dkt.Shein ameyasema hayo leo katika mkutano wa uzinduzi wa Kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM), uliofanyika katika viwanja vya Kibandamaiti maarufu viwanja vya Demokrasia ambavyo vipo jijini Zanzibar ndani ya Mkoa wa Mjini Magharibi na kuhudhuriwa na maelfu ya wanaCCM na wananchi waliofurika katika viwanja hivyo.

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,DkT. Ali Mohamed Shein akihutubia maelfu ya wanachama na wananchi wakati wa wzinduzi wa kampeni za Chama Cha Mapinduzi Zanzibar zilizofanyika katika Uwanja wa Kibanda Maiti jijini Zanzibar, kabla ya kumtambulisha Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM.(Picha na Ikulu/Diramakini).



Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt. Ali Mohamed Shein akimtambulisha Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi mbele ya maelfu ya wananchi (hawapo pichani), katika ufunguzi wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Demokrasia Kibanda Maiti jijini Zanzibar huku akimkabidhi ilani ya Uchaguzi 2020-2025.(Picha na Ikulu/Diramakini).

Katika maelezo yake, Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar amesema kuwa CCM imemchagua Dkt.Hussein Mwinyi kuwa mgombea nafasi ya Urais kutokana na sifa zote za kuwa Rais hasa ikizingatiwa kuwa yeye si mwanagenzi wa siasa kwani amewahi kuwa kiongozi katika nyadhifa mbalimbali ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema kuwa, kutokana na uwezo alionao Dkt.Hussein Mwinyi ana uwezo mkubwa wa kuipaisha Zanzibar na kuleta maendeleo hasa pale akiendelea kushirikiana na mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Mgombea wake Mwenza Mama Samia Suluhu Hassan na wagombea wengine wote wa chama hicho katika nafasi mbalimbali.

Rais Dkt.Shein ameeleza sifa mbalimbali za Dkt.Hussein Mwinyi ikiwa ni pamoja na kuwa muungwana, mwenye heshima kwa wakubwa na wadogo, asiye na mbwembwe za uongozi na pia ni daktari aliyebobea katika fani yake.

Aidha, ameeleza kuwa, Dkt. Hussein ni mgombea nafasi ya Urais pekee ambaye atayalinda Mapinduzi ya Januari 12, 1964 pamoja na kuulinda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao umeleta mafanikio makubwa nchini.

Makamu Mwenyekiti huyo alitumia fursa hiyo kumuombea kura Dkt. Hussein Mwinyi pamoja na wagombea wengine wote wa CCM huku akitumia fursa hiyo kuwanadi wagombea Ubunge, Uwakilishi na Udiwani wa CCM wa Mkoa wa Mjini kichama pamoja na kuwakabidhi Ilani ya chama hicho ili waende wakainadi.

Rais Dkt. Shein amesema kuwa, mikutano ya kampeni ya chama hicho itaendelea katika maeneo mengine mbalimbali katika mikoa na wilaya za Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuelekea kisiwani Pemba.

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Ali Mohamed Shein akimtambulisha Mgombea Ubunge wa Jimbo la Chumbuni Zanzibar, Ussi Salum Pondeza, wakati wa uzinduzi wa kampeni za CCM Zanzibar,
uliofanyika katika Uwanja wa Demokrasia Kibanda Maiti jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu/Diramakini).


Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt. Ali Mohamed Shein,akimtambulisha Mgombea Ubunge wa Jimbo la Jangombe Zanzibar,Ali Hassan Omar ( King) wakati wa Uzinduzi wa Kampeni za CCM Zanzibar,
uliofanyika katika Uwanja wa Demokrasia Kibanda Maiti jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu/Diramakini)


Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dkt. Amani Karume, Mama Fatma Karume, Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi wakiwa katika jukwaa la viongozi wakifuatilia hafla ya Uzinduzi wa Kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM). (Picha na Ikulu/Diramakini).

Nae mgombea nafasi ya Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dkt.Hussein Ali Hassan Mwinyi ameeleza mafanikio yaliopatikana katika utekeleza wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015-2020 chini ya uongozi wa Rais Dkt.Shein na kuaahidi atayaendeleza katika Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020-2025 aliyokabidhiwa.

Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi,Dkt.Hussein Ali Hassan Mwinyi akihutubia katika hafla ya ufunguzi wa Kampeni za Chama Cha Mapinduzi zilizofanyika katika Uwanja wa Demokrasia Kibanda Maiti jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu/Diramakini).

Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi wakimshangilia Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM,Dkt. Hussein Mwinyi (hayupo pichani) wakati akihutubia katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Demokrasia Kibanda Maiti jijini Zanzibar.(Picha na
Ikulu/Diramakini).


Mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) akimshangilia Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Kampeni za kuwatambulisha wagombea wa Ubunge na Uwakilishi uliofanyika katika Uwanja wa Demokrasia Kibanda Maiti jijini
Zanzibar.(Picha na Ikulu/Diramakini).


Hivyo, Dkt. Hussein almeeleza haja kwa wanaCCM na wananchi kukichagua chama hicho ili kuendeleza mafanikio hayo huku akieleza azma yake ya kuyaendeleza Mapinduzi pamoja na kuutunza na kuulinda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Aidha, ameeleza azma yake pamoja na vipaumbele vyake iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuiimarisha sekta ya uchumi wa bahari (blue economy), hasa uvuvi wa bahari kuu kwa lengo la kuinua ajira kwa vijana sambamba na kuimarisha pato la Taifa.

Pamoja na hayo, Dkt.Hussein ameyaeleza mambo mengine atakayoyapa kipaumbele ikiwa ni pamoja na kuiimarisha sekta ya utalii, sekta ya uvuvi, viwanda ufugaji wa samaki, kuwasaidia wavuvi, kuimarisha sekta ya kilimo na sekta nyinginezo.

Dkt.Hussein pia, ameeleza kuwa atahakikisha katika kuendelea zoezi la upatikanaji wa mafuta na gesi atahakikisha mikataba itakayofungwa inawanufaisha wananchi wa Zanzibar sambamba na kuhakikisha Wazanzibari wanapata fursa kubwa ya ajira katika sekta hiyo.

Ameeleza kuwa, katika kuhakikisha uchumi unaimarika ni lazima miundombinu ya barabara, bandari na uwanja wa ndege yote hiyo inaimarisha pamoja na kuhakikisha vinapatikana vyanzo vipya vya umeme kazi ambayo ataiendeleza kwa lengo la kukuza uchumi na maendeleo ya Zanzibar.

Sambamba na hayo ameeleza azma yake ya kuimarisha huduma za jamii zikiwemo elimu bora bila ya malipo hadi sekondari, kuongeza ufaulu kwa wanafunzi na kupitia upya mitaala ya elimu ikiwemo elimu ya ufundi ili vijana waweze kujiajiri wenyewe, kuongeza udahili, fedha kwa wanafunzi vyuoni huduma za afya kuanzia msingi hadi rufaa, kukuza bajeti ya afya, maji safi na salama.

Sekta ya kilimo, kikiwemo kilimo cha biashara na chakula vyote ataviimarisha sambamba na kuviendeleza na kuanzisha viwanda vikiwemo vya kusindika.


Msanii wa Bongo Fleva Ali Kiba akitoa burudani wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Kampeni za Chama Cha Mapinduzi zilizofanyika katika Uwanja wa Demokrasia Kibanda Maiti jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu/Diramakini).

Pia, ametoa pongezi kwa Rais Dkt.Shein kwa kusimamia amani na utulivu huku akiahidi na yeye kwa upande wake iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar ataiendeleza kwani anatambua umuhimu wake kwa maendeleo ya jamii na taifa kwa jumla.

Dkt. Hussein amegusia suala zima la utawala bora katika kukuza uchumi na kusisitiza suala zima la uwajibikaji na kueleza kuwa hatowavumilia wale wote waliokuwa hawawajibiki na kuhakikisha kwamba watu hawatofanya kazi kwa mazoea.

Mapema Naibu Katibu wa CCM Zanzibar, Abdalla Juma Mabodi ameeleza kuwa, Dkt.Hussein Mwinyi ana uwezo mkubwa wa kuuinua na kuuendeleza uchumi wa Zanzibar.

Msanii wa muziki wa Taarab, Aisha Mashauzi akitoa burudani wakati wa hafla ya ufunguzi wa Kampeni za Chama Cha Mapinduzi.(CCM) ukiofanyika katika Uwanja wa Demokrasia Kibanda Maiti
jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu/Diramakini).

Aidha, ameeleza kuwa, uwezo alionao Dkt. Hussein Mwinyi katika kusimamia amani na utulivu pamoja na Muungano ni mkubwa sana hasa ikizingatia historia yake ya uongozi wake ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mkutano huo ulikwenda sambamba na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali wa ndani ya nje ya Zanzibar wakiongozwa na msanii nguli Bongo Fleva Ali Kiba pamoja na mwana dada anaeinukia katika miondoko hiyo Zuhura Othman Soud (Zuchu) wakiungana na wasanii wa Bongo Movie na makundi mengine kadhaa ya wasanii.

Viongozi mbalimbali wa CCM walihudhuria akiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd pamoja na viongozi wengine wastaafu akiwemo Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Zanzibar Dkt. Amani Abeid Karume, Makamu wa Rais Mstaafu Dkt. Mohamed Kharib Bilali na viongozi wengine wa CCM kutoka Tanzania Bara.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news