Yanga SC yaicharaza Mtibwa Sugar, sasa bega kwa bega na Simba SC

Lamine Moro 61' aliyeunganisha kwa mguu wa kulia kona ya chini chini ya kiungo Carlos Carlinhos imewezesha Yanga SC kung'ara Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro,anaripoti Mwandishi Diramakini.

Ni kupitia michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo imewakutanisha na Mtibwa Sugar mjini humo leo Septemba 27,2020.

Matokeo ya leo yanaifanya Yanga SC kufikisha alama 10, sawa na mabingwa watetezi, Simba SC ambao wanaendelea kukaa nafasi ya pili kwa faida ya mabao mengi waliovuna katika michezo iliyopita. 

Aidha, wanalambalamba Azam FC inaendelea kuongoza baada ya kufanikiwa kushinda mechi zake zote nne za awali wakiwa na alama kumi na mbili.

Wakati huo huo leo Ruvu Shooting imelazimishwa sare ya bila kufungana na Biashara United Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wa Mwadui FC imeibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Ihefu, mabao ya Fred Felx 6' na Wallace Kiango 37' Uwanja wa Mwadui Complex, Kishapu mkoani Shinyanga.

Hata hivyo,raundi ya nne ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakamilishwa kesho kwa mchezo mmoja tu kati ya Coastal Union wakiwa wenyeji wa JKT Tanzania katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

No comments

Powered by Blogger.