Maadhimisho ya Miaka 56 ya Sherehe za Elimu Bila Malipo Zanzibar yafana, Rais Shein asema mafanikio ni makubwa, wanatarajia kufanya zaidi

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba katika kipindi cha miaka 10 ya uongozi wake imeendeleza dhamira ya kutangazwa kwa elimu bure na kuziendeleza jitihada zilizofanywa na uongozi wa Serikali zilizotangulia katika kuimarisha sekta ya elimu nchini, inaripotiwa na Mwandishi Diramakini.

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt. Ali Mohamed Shein akihutubia katika hafla ya Maadhimisho ya Tamasha la 56 la Elimu Bila Malipo Zanzibar lililofanyika katika Uwanja wa mpira wa Mao Tse Tung Jijini Zanzibar, baada ya kupokea maandamano ya wanafunzi wa Skuli za Unguja na Pemba.(IKULU).

Hayo yamesemwa leo Septemba 23, 2020 na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Ali Mohamed Shein katika Tamasha la 56 la Elimu Bila Malipo katika Uwanja wa Mao Zedong jijini Zanzibar.

Wanafunzi wakipita kwa maandamano wakati kilele cha miaka 56 ya Sherehe za Maadhimisho ya Elimu Bila Malipo Zanzibar katika uwanja wa MaoDze Dong leo Septemba 23,2020. (IKULU).

Wanafunzi wakiongozwa na walimu wao wakipita kwa maandamano wakati wa kilele cha miaka 56 ya Sherehe za Maadhimisho ya Elimu Bila Malipo Zanzibar katika uwanja wa MaoDze Dong leo Septemba 23,2020. (IKULU).

Tamasha lililohudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd pamoja na wanafunzi wa skuli za maandalizi,msingi,sekondari na vyuo wakiongozwa na walimu wao.

Amesema, katika kuuenzi na kuthamini uamuzi wa kutangaza elimu bure wa Septemba, 23, 1964 kuanzia mwaka wa fedha wa 2015/2016 Serikali iliamua kufuta michango yote waliyokuwa wakitozwa wazazi wa wanafunzi katika skuli za msingi na kuondoa gharama za mitihani ya skuli za sekondari kuanzia mwaka wa fedha 2016/2017.

Dkt.Shein amesisitiza kuwa, Serikali yenyewe ilibeba tena dhima ya kugharamia elimu kwa kutoa fedha za kufidia michango hiyo ambapo kwa mwaka wa tano sasa wanafunzi wote katika skuli za Serikali kuanzia ngazi ya elimu ya maandalizi hadi Sekondari  ya awali hupatiwa madaftari ya mahudhurio bila ya matatizo.
Ameongeza kuwa, mbali ya vifaa hivyo, skuli zote za sekondari za Serikali huingiziwa fedha taslimu kulingana na idadi ya wanafunzi kwa ajili ya kusaidia uendeshaji wa skuli hizo katika kipindi hiki ambacho Serikali imefuta michango ya wazazi.

Kadhalika Rais Dkt.Shein ameeleza kuwa, katika mwaka wa fedha wa 2019/2020, skuli zote za sekondari za Serikali zimeingiziwa jumla ya sh.bilioni 2.2 kwa ajili ya kufuta michango iliyokuwa ikitolewa na wazazi au walezi wa wanafunzi ambapo kwa mwaka wa fedha wa 2020/2021 Serikali imetenga jumla ya sh.bilioni 4.577 kwa ajili ya kufuta michango kwa skuli zote za Sekondari za Serikali.

Amesema, kwa lengo la kuleta ufanisi zaidi katika sekta ya elimu, Serikali inakusudia kutoa zawadi kwa walimu bora na kufanya marekebisho ya maslahi ya walimu wakuu na walimu wa kawaida kwa kuwapandisha madaraja baada ya kufanya tathmini ya utendaji wao.

Wanafunzi wa Skuli mbalimbali za Zanzibar wakiwa katika Sherehe za maadhimisho ya Miaka 56 ya Elimu Bila Malipo zilizofanyika leo katika Uwanja wa Mao-Dze Dong Mkoa wa Mjini Magharibi ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Ali Mohamed Shein (hayupo pichani).(IKULU).
 
Wanafunzi wa Chuo cha Afya kwa Mchina wakipita kwa maandamano mbele ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.Ali Mohamed Shein (hayupo pichani) katika Uwanja wa Mao-Dze Dong wakati wa kilele cha maadhimisho ya Miaka 56 ya Sherehe za Elimu Bila Malipo zilizofanyika leo. (IKULU).

"Napenda nikuhakikishieni kuwa dhamira hii njema ya Serikali yenu itaendelezwa na Awamu ya Nane itakapoingia madarakani baada ya mimi kuondoka madarakani ambapo skuli zote zitaendelea kupatiwa fedha kwa ajili ya uendeshaji wa skuli na kununua vifaa na mafunzo yatakayochangia katika ubora wa elimu,”amesema Dkt.Shein.

Ameeleza kuwa, katika kufanikisha dhamira hiyo katika mwaka wa fedha wa 2019/2020, skuli zote za sekondari za Serikali zimeingizwa jumla ya sh.bilioni 2.291 kwa ajili ya kufuta michango iliyokuwa ikitolewa na wazazi au walezi wa wanafunzi.Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Ali Mohamed Shein akisalimiana na mwanafunzi Maimuna Iddi Riziki (asiyeona) wa Skuli ya Umoja Uzini Mkoa wa Kusini Unguja baada ya kuhani utenzi akiwa na mwenzake Ramla Iddi Riziki (asiyeona) katika Uwanja wa Mao-Dze Dong wakati wa kilele cha maadhimisho ya Miaka 56 ya sherehe za Elimu bila malipo zilizofanyika leo Septemba 23, 2020. (IKULU).

Aidha, amesema katika kipindi cha miaka 10 ya uongozi wake mafanikio makubwa yamepatikana katika sekta ya elimu katika Utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2010-2015, Dira ya Maendeleo ya na Mipango mengine ya Kitaifa na Kimataifa.

Picha ya kushoto viongozi wa Serikali na chama wakifuatilia hotuba ya Maadhimisho ya Tamasha la 56 la Elimu Bila Malipo Zanzibar, wakati Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein (hayupo pichani) akihutubia katika viwanja vya Mao Tse Tung jijini Zanzibar. Kulia ni wanafunzi wakiwa na picha za viongozi. (IKULU).

Ameeleza kuwa, moja kati ya mafanikio muhimu yaliyopatikana ni kuweza kuwaandikisha watoto wote waliofika umri wa kusoma kwa asilimia mia moja.

Amesema kuwa, Zanzibar kabla ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964 kulikuwa na skuli moja tu ya maandalizi  iliyokuwa na wanafunzi 60 na skuli 62 za msingi zilizokuwa na wanafunzi 24,334 na skuli tano za sekondari zilizokuwa na wanafunzi 1,038.

Ameongeza kuwa, wakati huo haikuwa rahisi kwa mtoto wa kinyonge kupata haki na fursa ya elimu kwani elimu ilikuwa ni ya kulipia na ilitolewa kwa misingi ya ubaguzi na vile vile skuli zenyewe zilikuwa chache sana. 

Kwa maelezo ya Rais Dkt. Shein hivi sasa Skuli za Elimu ya Maandalizi zimefikia 728, Skuli za Msingi ni 503, Skuli za Sekondari ni 295 sambamba na ongezeko la vyuo vikuu ambapo hivi sasa vipo vitatu vyenye wanafunzi 7,273.

“Leo hii miaka 56 imepita tangu kutangazwa kwa elimu bure kwa hivyo, ni haki yetu kujipongeza kwa mafanikio makubwa tuliyoyapata katika sekta ya elimu baada ya Mapinduzi,"amesema Dkt.Shein.

Aidha, Rais Dkt.Shein amesema kuwa, Bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali imeongezwa kutoka TZS Bilioni 47.093 mwaka 2010/2011 hadi kufikia TSZ Bilioni 178.917 mwaka 2019/2020 huku akieleza kuwa katika skuli za Sekondari walimu wapya 1,175 wameajiriwa kwa kipindi cha mwezi Julai 2019 hadi mwezi Septemba mwaka 2020 kwa skuli za Unguja na Pemba.
Picha ya kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar,Mhandisi Dkt.Idriss Muslim Hijja, akizungumza wakati wa hafla hiyo ya Maadhimisho ya Tamasha la 56 la Elimu Bila Malipo Zanzibar lililofanyika katika Uwanja wa Mao Tse Tung jijini Zanzibar.Kulia ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Riziki Pembe akizungumza katika hafla hiyo. (IKULU).

Pia, Rais Dkt.Shein amesema kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeshaamua kwa makusudi kwamba wale walimu ambao wanajitolea na hawajaajiriwa kuanzia wale wanaosomesha elimu ya TUTU hadi Sekondari Serikali itawaajiri.

Sambamba na hayo, Rais Dkt.Shein ametoa zawadi kwa kutoa nafasi 100 za ufadhili wa masomo kwa wanafunzi waliofanya vizuri zaidi katika mitihani yao ya kidato cha sita ambapo mwaka jana zilikuwa 60 na mwaka juzi zilikuwa 30.

Rais Dkt.Shein pia, amewataka wazazi na walezi kuendelea kushirikiana katika kuwapatia fursa na kuwaruhusu vijana kushiriki vyema katika michezo na kuondokana na dhana kwamba mwanafunzi anayeshiriki michezo akiwa skuli anapoteza muda wake na hataweza kufanya vizuri katika masomo yake.

“Mtazamo huu sio sahihi na hauna ukweli hata kidogo na badala yake tufahamu kwamba hata sayansi inatueleza kwamba michezo ni sehemu muhimu ya mazoezi yanayojenga afya ya mwili na akili .......mimi na wenzangu ni mifano ya wale tulioshiriki michezo na sanaa tulipokuwa wanafunzi na tulifanya vizuri katika masomo na kufaulu mitihani katika ngazi mbalimbali,”amesema Dkt.Shein.

Pamoja na hayo, Rais Dkt.Shein ametumia fursa hiyo kuwakumbusha wananchi kuzingatia umuhimu wa amani na utulivu katika kufanikisha uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao wa Oktoba, mwaka huu wa 2020.

Amesisitiza kwamba, uchaguzi sio mwisho wa maisha na kuwataka wananchi kutambua kwamba hakuna mbadala wa amani na kila mtu ana dhima ya kutunza amani.

Rais Dkt.Shein pia, ametoa wito kwa wanafunzi kutambua kwamba na wao wana dhima ya kusoma ili wawe wataalamu wa hapo baadae na wazazi na walezi nao wana dhima ya kuwasimamia watoto wao.

Rais Dkt.Shein ametumia fursa hiyo kuwapongeza viongozi wa awamu zote za uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zilizopita kwa jitihada na michango ya katika kuimarisha sekta ya elimu huku akiuopongeza uongozi wa Wizara ya Elimu pamoja na wafanyakazi wake kwa mashirikiano mazuri ya kuiendeleza sekta hiyo.

Mapema Rais Dkt.Shein alipokea maandamano ya wanafunzi wa Skuli za Maandalizi, Msingi, Sekondari, Vyuo pamoja na walimu yaliyoongozwa na Brassband ya Chuo Cha Mafunzo Zanzibar ambapo katika maandamano hayo pia, wanafunzi walipita na picha mbalimbali za viongozi walioongoza Zanzibar.

Naye Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma amesema kuwa, kwa niaba ya walimu wenzake wanatoa shukurani kubwa kwa Rais Dkt.Shein kwa mafanikio makubwa yaliopatikana katika sekta ya elimu.

Amesema kuwa, katika sekta ya elimu Rais Dkt.Shein amefanya mambo mengi katika uongozi wake ikiwa ni pamoja na kuweka miundombinu mizuri ikiwa ni pamoja na kujenga skuli za ghorofa.

Mapema, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Dkt.Idris Muslim Hijja alieleza mchakato wa sherehe hizo ambazo zilizinduliwa Septemba 17, mwaka huu 2020 huko katika Mkoa wa Kaskani Unguja na leo kufikia kilele chake.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Ali Mohamed Shein akizungumza na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Riziki Pembe, wakati wa hafla ya Maadhimisho ya
Tamasha la 56 la Elimu Bila Malipo lililofanyika katika Uwanja wa Mao Tse Tung jijini Zanzibar. (IKULU).
Picha ya kulia Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Ali Mohamed Shein akizungumza jambo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, wakiwa katika hafla ya Maadhimisho ya Tamasha la 56 la Elimu Bila ya Malipo Zanzibar, lililofanyika katika uwanja wa Mao Tse Tung Jijini Zanzibar. Kushoto ni wanafunzi. (IKULU).

Aidha, Katibu Mkuu huyo alisisitiza kuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali inaendelea kuimarisha elimu ya Mafunzo ya Amali ili vijana waweze kuajiriwa na kujiajiri wenyewe.

Ameongeza kuwa, mnamo tarehe 21 Septemba mashindano katika mpango wa Sports 55 yalifanyika lakini kutokana na maradhi ya Covid 19 mwaka huu mashindano mengi yaliondoshwa huku akieleza juhudi kubwa zinazochukuliwa katika kuimarisha sekta ya michezo katika skuli.

Ameeleza kuwa, utaratibu wa kubadilishana sherehe kwa kufanyika Unguja na Pemba zimekuwa zikiwasaidia sana wanafunzi kwa lengo la kuimarisha uhusiano.

Wakati huo huo, wanafunzi waliimba wimbo wa Tamasha la Elimu Bila Malipo ambapo baada ya hapo utenzi ulisomwa na wanafunzi wasioona ambao wote ni baba mmoja na mama mmoja. Sambamba na hayo watoto walionesha vipaji vyao katika  michezo.

Rais Dkt.Shein pia ametoa zawadi kwa washindi walioshinda katika michezo mbali mbali ikiwemo riadha, kuandika insha Maalim Othman Ali Msabaha ambaye ameibuka kuwa ni mwalimu bora wa michezo mwaka huu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news