Maalim Seif ahaidi kuwafuta machozi wakulima wa mwani, wavuvi Zanzibar

MGOMBEA Urais wa Zanzibar kupitia Tiketi ya Chama cha ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad amesema endapo wananchi wa Zanzibar watamchagua na kumuweka madarakani kuwa Rais atahakikisha wakulima wa mwani wanapata faida kwa kuweka bei nzuri ambayo itawezesha zao hilo kuwanufaisha zaidi, anaripoti TALIB USSI (Diramakini) ZANZIBAR.

Maalim Seif ameyaeleza hayo huko Tumbe wakati akizungumza na wakulima wa mwani pamoja na wavuvi wa eneo hilo.

Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia ACT-Wazalendo akiangalia mwani aina ya Spinosioum,mwani mwembamba ambao hulimwa katika maji madogo katika Kijiji cha Tumbe Wilaya ya Michdweni Mkoa wa Kaskazini Pemba. (Picha na Twalib Ussi/Diramakini).

Amesema kuwa, wanunuzi wa mwani wamekuwa wakiwadhulumu wakulima kwa kununua zao hilo kwa bei ya chini ya sh.600 kwa kilo moja, jambo ambalo limekuwa likisababisha lawama kwa kuwa badala ya mkulima kufaidika,wanunuzi wao ndio wanufaika wakubwa.

“Tukingia madarakani nitahakikisha Serikali yangu inawahudumia wakulima wa mwani kwa kuwapatia vyombo ambavyo vitafika maji marefu ili waweze kulima mwani bora wa Cotonee ambao una bei kubwa katika Soko la Dunia,”amesema Maalim Seif.

Mapema wakulima wa zao hilo walimweleza mgombea huyo kuwa, wakulima na wavuvi wengi wanafariki baharini kutokana na vyombo vidogo vidogo wanavyotumia na kukosekana vyombo vya uokozi.

Bi.Halima Ali ambaye ni mkulima wa mwani ameieleza Diramakini kuwa, wamekuwa wakipoteza nguvu kazi kutokana kulima mwani kwenye maji ya kina kirefu kwa kutumia vyombo vidogo.

“Licha ya kwenda mbali na kina kikubwa cha maji Maalim bei hii haituridhishi hata kidogo, nyonga zote zimekufa kwa kuinama kucha, halafu tunapewa shilingi 600 kwa kilo moja,”amesema Mkulima huyo.

Bikuu Hamad Omar ambaye ni mkulima wa mwani katika Kijiji cha Tumbe Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pembe akieleza kero za uzalishaji wa zao hilo. (Picha na Talib Ussi/Diramakini).

Masoud Abdallah Mwinyi ambaye ni mvuvi kwa kutumia mtumbwi amesema, kutokana na mkondo mkali walionao katika ukanda wa bahari yao wamekuwa wakihatarisha maisha yao na kueleza kuwa, wenzao zaidi ya sita wamepotea mwaka huu.

“Tunakuomba Maalim Seif ukiwa rais au kama una mpango wowote tufanyie ili tupate boti za kileo za uvuvi pamoja na za uokozi ambazo zitatufaa sisi na wakulima wa mwani,”amesema Mwinyi.

Kufuatia kilio hicho, Maalim Seif amesema, mara tu akiingia madarakani atahakikisha wavuvi wanakopeshwa boti za bei nafuu ili waweze kuvua katika maji ya kina kirefu na kuwa salama.

“Tutahakikisha KMKM wanajeshi wa maji wanakuwa na boti nzuri na zenye 'speed' (kasi) zikipata tetesi za ajali kwa wavuvi wafike haraka kwa ajili ya uokozi,”amesema Maalim Seif.

Amesema, atahakikisha wavuvi wote wanakuwa na mawasiliano na wanamaji ili likitokea tatizo waweze kufanya mawasiliano ya haraka.

Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia ACT-Wazalendo akiangalia mwani aina ya Spinosioum,mwani mwembamba ambao hulimwa katika maji madogo katika Kijiji cha Tumbe Wilaya ya Michdweni Mkoa wa Kaskazini Pemba. (Picha na Talib Ussi/Diramakini).

“Tunakusudia kuyabadilisha maisha ya Wazanzibar kwa muda mfupi bila kuwabagua watu kwa sababu ya vyama vya siasa au dini,”ameeleza Maalim Seif ambaye aliwahi kuwa Makamu wa Rais katika Serikali ya Zanzibar yenye mfumo wa umoja wa kitaifa.

Ameeleza kuwa, katika Serikali yake atahakikisha bei ya mwani inafikia sh.1000 kwa kilo na kuwapatia vifaa vyoote ambavyo vitarahisisha katika kazi zao.

Mgombea huyo wa ACT-Wazalendo yuko kisiwani Pemba leo kwa siku ya pili akinadi sera zake huku akiwa na kauli mbiu ya chama hicho ya 'Kazi na Bata'.

1 comment:

  1. NDUGU MNAFANYA KAZI NZURI SANA KUHABARISHA UMMA, TANGU NIANZE KUFUATILIA BLOGU HII NIMEONA HAIPENDELEI, INATOA HABARI ZA VYAMA TOFAUTI TOFAUTI, HILO NDILO TUNALOHITAJI SISI WANANCHI ILI TUWEZE KUELEWA SERA NA VIPAUMBELE VYA WAGOMBEA, HATUA AMBAYO ITATUWEZESHA KUCHAGUA WATU SAHIHI IFIKAPO SIKU YA UCHAGUZI, ENDELEENI KWA MOYO HUU HUU ILI KUTUPASHA HABARI KATIKA KIPINDI HIKI MUHIMU AMBACHO KIMEBEBA HATIMA YA MAISHA YETU IWE MWANASIASA, MCHUMI, MKULIMA, MFUGAJI, MVUVI, MWALIMU, MFANYABIADHARA NA WENGINE WENGI KIPINDI HIKI NI CHA MUHIMU SANA KWETU KWA AJILI YA KUWAPIMA WAGOMBEA TUWEZE KUFANYA MAAMUZI MEMA. KWA MARA NYINGINE HONGERENI SANA DIRAMAKINI BLOG

    ReplyDelete

Powered by Blogger.