Machinga Kilimanjaro:Asante Rais Magufuli, vitambulisho vyako vimetutua mzigo,utamu wake tunaujua wenyewe,tutakupatia zawadi yetu Oktoba

WAFANYABIASHARA wadogo maarufu kama Machinga katika Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro wamesema Vitambulisho wa Wajasiriamali wadogo vimewatua mzigo, hivyo
wanawashangaa baadhi ya wanasiasa wanaopotosha kuhusu vitambulisho hivyo, anaripoti Pius Ntiga, Kilimanjaro.

Wakizungumza na Amsha Amsha 2020 ya Uhuru FM inayoangazia mafanikio yaliyofikiwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli, wafanyabiashara hao wamesema utamu wa vitambulisho hivyo wanaujua wao.

Wamesema awali walikuwa wanalipa shilingi 500 kwa siku, sawa na shilingi 182,000 kwa mwaka, kiasi ambacho wamesema ni kikubwa ukilinganisha na shilingi 20,000 wanayolipa sasa kwa mwaka.

"Tulikuwa tukilipa shilingi 200 ya usafi kwa siku, sawa na shilingi 73,000 kwa mwaka, ambapo sasa mateso kama hayo hatuyapati tena tunashukuru sana Rais Magufuli kwa kutuona na tutampa zawadi mwaka huu," wamesema Machinga.

Kwa mujibu wa wafanyabiashara hao wadogo, mkombozi wao ni Rais Magufuli amekuja na mpango wa shilingi 20,000 tu kwa mwaka na sasa kero za migambo kuwafukuza hazipo tena.
" Nikwambie tu kuwa mabenki nayo yamesema kwa kuwa tuna vitambulisho, shughuli zetu zimerasimishwa sasa, hivyo tumeanza kupewa mikopo, huku vitambulisho vikiwa ni dhamana yetu,"Wamesema.

Wamesema hivi sasa hawasumbuliwi tena na askari wa jiji wala mgambo kama ilivyokuwa hapo awali.

"Vitambulisho vya wamachinga vimetusaidia sana, tunanunua kwa ridhaa yetu, hatulazimishwi,"Wamesema Machinga.

Aidha, wamefafanua kuwa uwepo wa vitambulisho hivyo vimewaondolea kero na kwa sasa biashara yao imeimarika zaidi na kipato chao kimeongezeka na wamefanikiwa kununua ardhi na kujenga nyumba.
Kutokana na mafanikio hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Moshi, Michael Mwandezi, amesema tangu kuanza kwa utaratibu huo zaidi ya asilimia 70 ya Wamachinga wamepatiwa vitambulisho katika Manispaa ya Moshi.

Mwandezi amesema, fedha inayotokana na vitambulisho hivyo huenda Hazina na kisha kurudishwa katika Manispaa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ambayo inawagusa moja kwa moja wananchi.

"Pia tumewasaidia hawa wajasiriami kuwajengea uwezo wa kimtaji ambapo sasa wanakopesheka kupitia vitambulisho, hivyo vimewanufaisha kwa kukopa fedha benki,"amesema Mkurugenzi.

Hivi karibuni baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakipotosha kuhusu vitambulisho hivyo vya Wamachinga kuwa haviwanufaishi na badala yake wanaibiwa, kauli ambayo Rais John Magufuli ambaye ni Mgombea wa Urais kupitia CCM, amewataka wafanyabiashara hao kuwapuuza wanasiasa na badala yake waunge juhudi za serikali za kuwakomboa Wamachinga.


Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news