Majaliwa alivyotumia jukwaa kuwapa habari njema wafugaji,wakulima na kuelezea miradi kuelekea Oktoba 28

*ASEMA SERIKALI INAWATHAMINI WAFUGAJI,WAKULIMA NA WATUMISHI NCHINI

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali inawathamini wafugaji na itaendelea kuboresha sekta yao, inaripoti DIRAMAKINI.

Ameyasema hayo leo Jumatano, Septemba 16, 2020 wakati akiwasalimia wananchi waliojitokeza kumlaki kwenye kata ya Bukundi, tarafa ya Nyaranje, wilayani Meatu akiwa njiani kutokea Mkalama, Singida.

"Tunatambua na kuwathamini sana wafugaji kwa sababu tunajua mifugo ni fedha," amesema wakati akimuombea kura mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, mgombea ubunge wa jimbo la Meatu, Bi. Leah Komanya na Mgombea udiwani wa kata ya Bukundi, James Sombi.

"Serikali yenu imedhamiria kuboresha sekta ya mifugo nchi nzima na ndiyo maana Waziri mwenye dhamana ya mifugo amekuwa anakutana na wafugaji nchi nzima ili waeleze ni maeneo gani yanawapa kero."

Amesema Serikali iliruhusu vijiji 920 kati ya 970 vilivyokuwa kwenye maeneo ya hifadhi virasimishwe ili wananchi waendelee na ufugaji na kilimo.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi wa Kata ya Bukundi, katika Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu, Septemba 16, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Amesema eneo la Bukundi lina wakazi wengi ambao asilimia 60 kati ya hao ni wafugaji. Kwa hiyo amewaomba wagombea hao wakipita, warudi kwa wananchi na kutatua kero zao kwenye sekta ya mifugo.

Mapema, mgombea ubunge wa jimbo la Kisesa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Bw. Luhaga Mpina alisema wakati Serikali ya awamu ya tano inaingia madarakani, majosho 1,000 kati ya 2,400 yaliyokuwepo yalikuwa ni mabovu.

"Chini ya uongozi wa Rais wetu jemedari, Dkt. Magufuli, majosho 600 yamekarabatiwa na tumejenga majosho mengine mapya 104. Yote yamepewa dawa ya ruzuku na wafugaji wanayatumia kuosha mifugo yao," alisema.

WAKULIMA

Katika hatua  nyingine Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa Singida waingie kwenye kilimo cha kisasa ili waweze kuinua uchumi wao.

“Wananchi ingieni kwenye kilimo cha Kisasa na chenye tija ili muinue kipato chenu. Hili eneo la Gumanga ni zuri sasa kwa kilimo na wengi wenu wanalima mbogamboga. Vijana msikae kusubiri ajira za ofisini, ajira siyo lazima ukae ofisini, unaweza kujiajiri kwenye kilimo,” alisema.

Ametoa kauli hiyo jana Jumanne, Septemba 15, 2020 wakati akizungumza na wananchi waliohudhuria mkutano wa kuwanadi mgombea ubunge wa Iramba Mashariki, Bw. Francis Isack Mtinga na mgombea udiwani, Bw. James Mkwega uliofanyika kwenye viwanja vya stendi ya mabasi Gumanga, wilayani Mkalama, mkoani Singida.

Mheshimiwa Majaliwa ambaye alikuwa mkoani Singida kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, alisema Serikali inatekeleza kwa vitendo ilani ya CCM ya mwaka 2020 hadi 2025 na moja ya mkakati wake ni kutoa fursa tofauti ili wananchi waweze kunufaika.

“Huku Singida ni wakulima wazuri wa alizeti na mna viwanda vingi vya kusindika mafuta. Tumieni fursa hii ya kilimo kuinua kipato chenu, Serikali yenu itaendelea kuboresha fursa za uwekezaji.”

Mapema, mgombea ubunge wa jimbo la Iramba Magharibi na Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Mwigulu Nchemba aliwataka wakazi wa Singida wasifanye mzaha kwenye masuala ya uchumi.

“Tuache mzahamzaha katika masuala ya uchumi na maendeleo na siku ya tarehe 28 Oktoba, tufuatane wote tukapige kura kwa Dkt. John Pombe Magufuli. Raha ya ushindi ni kuwa na kura nyingi za Rais, Wabunge na madiwani,” alisema.

Naye mbunge aliyemaliza muda wake, Bw. Allan Kiula aliahidi kusaidiana na Bw. Mtinga kufanya kampeni ili kuhakikisha Chama cha Mapinduzi kinapata ushindi mkubwa.

“Tutasaidiana na Bw. Francis Isack kutafuta kura za CCM. Tutafanya hivyo pia kwa ajili ya kura za madiwani wetu. Tunahitaji madiwani wa kutosha ili Bw. Isack aweze kupata timu ya kufanya nayo kazi kwa urahisi,” alisema.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ameagiza ekari 2,500 kati ya ekari 5,432 zilizoko kwenye kijiji cha Sagala zirejeshwe kwa wananchi ili zitumike kwa kilimo.

“Tunaboresha uchumi ili ushuke kwa wananchi iwe kwenye kilimo, uvuvi au ufugaji. Nina taarifa kuwa Halmshauri ya Singida kwenye Kijiji cha Sagala wamechukua ekari 5,432 na kuamua kuzikodisha kwa wannchi wakidai kuwa ni kitega uchumi cha Halmashauri.”

“Wao hawalimi, na kama hawana cha kufanya kwenye eneo lile, walirudishe kwa wananchi. Mkuu wa Mkoa wa Singida, uende kule na uanze mchakato wa kupunguza eneo hilo ili yapatikane mashamba ya kuwagawia wananchi. Nasikia wanawakodisha kwa sh. 50,000.”

“Najua hawawezi kulima ekari zote 5,000. Nenda kawapunguzie ekari 2,500 ili wagawiwe wananchi. Ingekuwa mjini hapa Ilongero, tungesema wanataka kupima viwanja na ningewasamehe, lakini kule ni mbali lazima warudishe hilo eneo kwa wananchi,” alisema na kuamsha shangwe kwa wananchi hao.

Aliwataka wananchi hao watakapopatiwa eneo hilo, walime kwa bidii ili mazao yao yaweze kuuzwa mjini na kwenye kata ya Ilongero.

MIRADI

Mbali na hayo Serikali imetumia zaidi ya sh. bilioni 6.318 kwa ajili ya ujenzi wa miradi kwenye vijiji mbalimbali vya wilaya ya Mkalama, mkoani Singida ili kuwaondolea adha ya maji safi wananchi wake.

Hayo yamesemwa jana Jumanne, Septemba 15, 2020 na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akizungumza na wananchi waliohudhuria mkutano wa kuwanadi wagombea ubunge na udiwani wa CCM uliofanyika kwenye viwanja vya stendi ya mabasi Gumanga, wilayani Mkalama.

Mheshimiwa Majaliwa ambaye alikuwa mkoani Singida kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, alisema Serikali ya awamu ya tano imejenga miradi ya kimkakati zaidi ya 1,490 kwenye sekta ya maji nchi nzima.

Akifafanua baadhi ya miradi iliyofanyika katika kipindi cha mwaka 2015/2016 na 2019/2020, Mheshimiwa Majaliwa alisema kati ya fedha hizo, sh. bilioni 1.37 zimetumika kwa ajii ya mradi wa maji vijiji vya Mughano, Ngimu, Mgori, Malolo, Kijota, Ghaluyangu na Mangida.

“Miradi mingine ni mradi wa maji kijiji cha Mwankoko ‘B’ ambao umetumia shilingi milioni 656, na mradi wa maji kijiji cha Kisaki ambao umetumia shilingi milioni 551. Pia, shilingi milioni 428 zimetumika kwa ajili ya mradi wa usambazaji wa maji kijiji cha Gumanga na shilingi milioni 910 zimetumika kwa ajili ya mradi wa usambazaji wa maji kijiji cha Nyahaa,” alisema.

Akifafanua zaidi, Mheshimiwa Majaliwa alisema sh. milioni 341 zimetumika kwa ajili ya mradi wa uchimbaji wa visima virefu saba katika maeneo ya Nduguti, Kisuluiga, Matongo, Ipuli, Mkiko, Mwanga, Wangeza, Kinampundu, Kinyangiri, Msingi, Senene, Milade, Mbigigi, Nduguti (visima viwili), Tumuli (kisima kimoja) na Ibaga (kisima kimoja).

Alisema sh. milioni 158 zimetumika kwa ajili ya mradi wa uboreshaji maji katika kijiji cha Nduguti na sh. milioni 70 zimetumika kwa ajili ya uboreshaji maji katika kijiji cha Kinyangiri.

Mbali ya juhudi zote hizo, Mheshimiwa Majaliwa alisema sh. bilioni 1.37 zimetumika kwenye mradi wa maji kwa vijiji 10 vya Ibaga, Lyelembo, Mpambala, Ikolo, Kinyambuli, Ipuli, Makuro, Donimic, Ishinsi Nkalalala na Lukomo.

Wakati huohuo, Mheshimiwa Majaliwa alisema sh. milioni 235.98 zimetumika kwa ajili ya uchimbaji wa visima visima virefu na vifupi 20 ikiwa ni pamoja na ufungaji wa pampu za mkono.

Alisema kiasi kingine cha sh. milioni 144 kimetumika kwa ajili ya upanuzi wa mradi wa maji kijiji cha Mntamba na sh. milioni 85 nyingine zimetumika kwa ajili ya ukarabati wa mradi wa maji kijiji cha Ipuri.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news