Majaliwa apokea wanachama 20 wa CHADEMA, awataka wananchi wasidanganyike bei ya kahawa

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amewapokea wanachama 20 kutoka Chama cha Demokrasia (CHADEMA) ambao wameamua kurudi CCM.

 Mjumbe wa Kamati Kuu, Kassim Majaliwa, akipokea kadi za wanachama wa vyama pinzani, waliyohamia CCM, katika mkutano wa kampeni, uliyofanyika katika viwanja vya Mayunga, Jimbo la Bukoba Mjini, Septemba 28, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Wanachama hao wameongozwa na Mwenyekiti wa Vijana wa CHADEMA wa Mkoa wa Kagera, Bw. Francis Mutachunzibwa ambaye pia alimtambulisha Naibu Katibu Mkuu wa BAVICHA, Bi. Getrude Ndibalema ambaye alijiuzulu uongozi tangu mwaka jana.

 Aliyekua Mwenyekiti wa BAVICHA Mkoa wa Kagera, Francis Rutha, akizungumza mbele Mjumbe wa Kamati Kuu, Kassim Majaliwa na wananchi wa Bukoba mjini, baada ya kuhamia rasmi CCM, katika mkutano wa kampeni, uliyofanyika katika viwanja vya Mayunga, Jimbo la Bukoba Mjini, Septemba 28, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Bw. Mutachunzibwa alisema: “Ninaijua vizuri CHADEMA, nilipotea, nilitenda dhambi lakini sasa nimeamua kurudi nyumbani, nipokeeni.”

“Ninawaomba wana-Bukoba tumchague Dkt. Magufuli, mashine ya kusaga na kukoboa, jembe la nguvu. Kuanzia kesho, nitamnadi yeye na Advocate Byabato hadi kieleweke.”

Akizungumza na maelfu ya wakazi wa mji wa Bukoba leo jioni Septemba 28, 2020 waliojitokeza kwenye mkutano uliofanyika kwenye uwanja wa Mashujaa, Manispaa ya Bukoba, mkoani Kagera, Mheshimiwa Majaliwa aliwataka wakazi hao wajitafakari sana wanapofikiria kumchangua mtu wa kuongoza nchi.

 Mjumbe wa Kamati Kuu, Kassim Majaliwa, akiwahutubia wananchi wa Jimbo la Bukoba Mjini, katika mkutano wa kampeni, uliyofanyika katika viwanja vya Mayunga, Jimbo la Bukoba Mjini, Septemba 28, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

“Tunataka kiongozi mwenye hofu ya Mungu na ili umpate ni lazima umjue historia yake. Kuongoza nchi si lelemama, kiongozi wa nchi ni Mkuu wa Nchi, tena ni Mkuu wa Majeshi.”

Mheshimiwa Majaliwa ambaye ameanza ziara katika mkoa wa Kagera kumuombea kura mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, alitumia fursa hiyo kuwaombea kura mgombea ubunge wa jimbo la Bukoba Mjini kwa tiketi ya CCM, Wakili Steven Byabato, mgombea udiwani wa kata ya Bilele, Bw. Tawfiq Sharif Salum na madiwani wengine wa jimbo hilo.

Aliwasimamisha wazee wa Kagera wakiwemo aliyekuwa Meya wa Bukoba, Dkt. Anatoly Amani, aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Balozi Khamis Kagasheki ambao wote waliomba kura za Dkt. Magufuli, Wakili Byabato na madiwani wa jimbo hilo.

Kwa upande wake, aliyekuwa Waziri wa Viwanda, Bw. Charles Mwijage, alisema Muleba wana ajenda ya kuhakikisha kura zote zinaenda kwa Dkt. Magufuli na wabunge wa CCM na akawataka wana-Bukoba nao wafanye hivyo ili kuhakikisha majimbo yote tisa yanabakia CCM na pia wanapata wabunge wanne wa viti maalum.

MSIDANGANYIKE KUHUSU BEI YA KAHAWA

Wakati huo huo,Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema Serikali ya CCM imedhamiria kuhakikisha kilimo kinamnufaisha mkulima wa Tanzania.

"Watu wasije kuwadanganya kwamba Serikali haiwajali, siyo kweli. Kuna sababu zilizochangia kuyumba kwa bei ya kahawa kwenye soko la dunia."

Ametoa kauli hiyo leo mchana Septemba 28, 2020 wakati akizungumza na wakazi wa Rubale kwenye mkutano uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Rubale, wilayani Bukoba, mkoani Kagera.

"Serikali ya awamu ya tano ilipoingia madarakani, iliazimia kufufua mazao matano ya kimkakati ambayo ni kahawa, pamba, korosho, chai na tumbaku. Mazao haya bei ilishuka na si katika zao la kahawa tu."

"Kuyumba kwa bei haikuwa katika zao la kahawa tu bali katika mazao mengine kama pamba na korosho. Kahawa bei yake iliathirika kwa sababu ya ugonjwa wa Corona. Korosho bei ilishuka kutoka sh.3,300 hadi sh. 1,900. Pamba pia ilishuka bei," amesema.

Amesema Kenya ndiko mnada wa kahawa huwa unafanyika lakini hadi sasa bado wanasumbuliwa na ugonjwa wa Corona kwa hiyo haikuwa rahisi kufanya biashara katika kipindi chote hicho.

Mheshimiwa Majaliwa ambaye ameanza ziara katika mkoa wa Kagera kumuombea kura mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli. Ametumia fursa hiyo kuwaombea kura mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM, Bw. Jason Rweikiza, mgombea udiwani wa kata ya Rubale, Bw. Rwegasira Renatus Rwechungura na madiwani wengine wa jimbo hilo.

Kuhusu maji, Mheshimiwa Majaliwa amesema sh. bilioni 4.09 zilitolewa ili kuboresha miradi ya maji katika vijiji kadhaa ambayo yote imekamilika. Almevitaja vijiji hivyo kuwa ni Ibwera, Kasharu, Kitahya, Katale, Itongo, Bituntu, Kibona, Katoro, Mikoni, Kibirizi Ngarama, Ruhoko na Ruhunga.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news