Majaliwa: Urais si sehemu ya majaribio, Magufuli anatosha, mambo haya hapa tumetekeleza na tutatekeleza zaidi

Mjumbe wa Kamati kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Kassim Majaliwa amesema kiti cha urais siyo cha mchezo, kinahitaji mtu makini."Uongozi wa nchi siyo jambo la mchezo, linataka kiongozi makini, kiongozi anayetetea rasilmali na anayetetea wanyonge dhidi ya rushwa na ufisadi," amesema. 

Ametoa kauli hiyo leo mchana (Alhamisi, Septemba 24, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa kata za Hungumalwa na Ngudu wilayani Kwimba, mkoani Mwanza kwenye mkutano uliofanyika kwenye viwanja vya sokoni.

 

"Wengine watakuja kuomba kura lakini kazi yao kubwa ni kukashifu kila jambo linalofanywa na Serikali. Naomba kura za wananchi wote, wana CUF, CHADEMA, ACT mkipigie kura Chama cha Mapinduzi sababu maendeleo hayana chama."

 

"Wakija hapa muwasikilize; mkiwauliza Ilani yao watakwambia wanayo ila iko kwenye website. Sisi ya kwetu tunayo hii hapa," alisema huku akionesha Ilani ya CCM ya 2020 - 2025."

 

Amewataka wakazi hao wafanye maamuzi thabiti ya kutafuta viongozi tena wanaozungumza lugha moja. "Viongozi hao ninawaombea kura ni Rais, Mbunge na Diwani. Msichague viongozi ambao kazi yao ni kusema hapana kwenye mambo ya maendeleo au kwenye bajeti ya Taifa. Naomba kura kwa viongozi hao watatu," amesema.

 

Mheshimiwa Majaliwa ambaye yuko mkoani Mwanza kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, alitumia fursa hiyo kumwombea kura mgombea ubunge wa jimbo la Kwimba, Bw. Shanif Mansoor, mgombea udiwani wa Hungumalwa, Bw. Bukaba  Majoge na madiwani wa kata zote za wilaya ya Kwimba.

 

Wakati huohuo, mgombea ubunge wa jimbo la Geita Vijijini, Bw. Joseph Kasheku Msukuma ambaye aliwepo kwenye mikutano huo, alitumia fursa hiyo kuiomba Serikali iwajengee soko la kisasa wakazi wa Hungumalwa kwa sababu eneo hilo pana biashara kuwa ya dengu, choroko na kunde.


USAFIRI


Wakati huo huo Mjumbe wa Kamati kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema Serikali ya CCM imeimarisha miundombinu ya usafiri nchini ili wananchi waweze kuchagua aina ya usafiri wanaotaka pindi wanapotaka kusafiri.

 

"Tunataka tuhakikishe Watanzania wanatumia njia zote za usafiri kulingana na matakwa yake ndio maana tunatengeneza barabara, tumenunua ndege, tunajenga reli pamoja na kuendelea kuboresha usafiri wa majini," amesema.

 

Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Septemba 24, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa Misungwi kwenye mkutano uliofanyika kwenye uwanja wa Amani wilayani humo, mkoani Mwanza. 

 

"Tunajenga reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro na Dodoma, baadaye itatengenezwa ifike hadi Tabora na Mwanza. Ukitaka kupanda ndege una uhuru, ukitaka treni nenda, ukitaka basi, barabara nzuri zipo na ukienda majini nako pia tumeboresha usafiri,” amesema.

 

Mheshimiwa Majaliwa yuko mkoani Mwanza kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli. Aliwasisitiza wakazi hao wasiache kupiga kura siku hiyo. Mbunge wa jimbo la Misungwi, Bw. Alexander Mnyeti na madiwani wote 27 wa jimbo hilo wamepita bila kupingwa.

 

“Tunataka tuwe na kiongozi ambaye anaweza kuratibu maendeleo ya Watanzania, kiongozi ambaye anaweza kurudi chini na kujua kuna changamoto gani, tunataka kiongozi ambaye ana uwezo wa kusimamia rasilimali zetu, na huyo si mwingine bali ni Dkt. John Pombe Magufuli,” amesema.

 

Akielezea sekta ya mifugo, Mheshimiwa Majaliwa amesema: “Rais wetu amefanya maboresho makubwa sana katika sekta ya mifugo, Rais anataka kuona wafugaji na wavuvi wananufaika na shughuli zao, yale mapori makubwa tunachukua ili wafugaji wapate sehemu za malisho pia tunajenga mabwawa hukohuko, tunajenga maabara kwa ajili ya kutibu mifugo yetu. Kwenye uvuvi tunaimarisha sekta hiyo, ili kuhakikisha tunaendelea kuinua sekta hiyo, tumepunguza kodi pamoja na kuondoa tozo mbalimbali.”

 

MAJI


Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) imekamilisha ukarabati na upanuzi wa miradi ya maji katika miji mikuu ya wilaya, miji midogo na miradi ya kitaifa kwa sh. bilioni 58.8 ukiwemo mji wa Nansio, Ukerewe.

 

“Shilingi bilioni 58.8 zimetumika kwenye ukarabati na upanuzi wa miradi ya maji ambapo miradi ya maji katika Mji ya Longido, Sengerema na Nansio-Ukerewe imekamilika,” alisema.

 

Hayo yamebainishwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Kassim Majaliwa wakati akizungumza na wakazi wa mji wa Nansio jana jioni (Jumatano, Septemba  23, 2020) kwenye uwanja wa Getrude Mongella, mjini Nansio, mkoani Mwanza.

 

Alisema kati ya fedha hizo, sh. bilioni 13 zimetolewa kwa ajili ya miradi ya maji ikiwemo sh. bilioni 10.9 za uboreshaji wa huduma ya majisafi mjini Nansio ambapo wakazi wapatao 108,653 wananufaika na mradi huo katika eneo lote la mji wa Nansio. Alisema sh. bilioni 2.1 zilitumika kwa uboreshaji huduma ya usafi wa mazingira mjini Nansio.

 

Aliitaja miradi mingine ya maji kuwa ni miradi ya maji Pamoja na uchimbaji visima ambapo zilitolewa sh. bilioni 1.3 kwa miradi hiyo ikiwemo ukarabati wa mradi wa maji Irugwa, mradi wa maji ya bomba ya Nansore, mradi wa maji wa Muriti/Ihebo, upanuzi wa mradi wa maji wa Chabilungo na upanuzi na ukarabati wa mradi wa maji Kazilankanda.

 

Mheshimiwa Majaliwa ambaye yuko mkoani Mwanza kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, alitumia fursa hiyo kumwombea kura mgombea ubunge wa jimbo la Ukerewe, Bw. Joseph Mkundi na madiwani wa kata zote za wilaya ya Ukerewe.

 

Akielezea sekta ya uvuvi, Mheshimiwa Majaliwa alisema katika kutekeleza Ilani ya CCM, Serikali iliondoa kuondoa kodi katika zana na malighafi za uvuvi zikiwemo injini za kupachika, nyuzi za kushonea nyavu (twines) na vifungashio.

 

“Pia tumepunguza ada ya leseni ya kuuza samaki na mazao ya uvuvi yanayovuliwa kwenye maji baridi. Serikali itaendelea kufanya upya mapitio ya tozo mbalimbali katika sekta ya uvuvi ili kuwapunguzia kero wavuvi. Tumeweka mazingira wezeshi ya upatikanaji wa vifaa bora vya uvuvi, kuzuia uingizaji na uzalishaji wa zana haramu za uvuvi na kuhamasisha uwekezaji katika uzalishaji wa zana na vyakula vya samaki,” alisema.

 

Kuhusu sekta ya afya, Mheshimiwa Majaliwa alisema hospitali ya wilaya hiyo ilipatiwa sh.  milioni 570 ujenzi jengo la kisasa la upasuaji (theatre), ujenzi wa duka la dawa, ukarabati wa jengo la kuhifadhia maiti na ukarabati mkubwa wa wodi saba ambazo zote zinatumika.

 

Kuhusu umeme, alisema kati ya vijiji 76, vijiji 70 vimepelekewa huduma ya umeme na vijiji sita bado havina umeme. Alivitaja vijiji hivyo kuwa ni Kaseni, Busangumugu, Murutilima, Kitanga, Namakwekwe na Muhande.

 

Kuhusu elimu, Mheshimiwa Majaliwa alisema mpango wa elimu bila malipo kuanzia 2015/2016 – 2019/2020 uliwezesha shule za msingi 123 zipatiwe sh. bilioni 3.29 kwa ajili ya ukarabati, utawala, michezo, mitihani na posho kwa maofisa elimu kata na walimu wakuu.

 

Chini ya mpango huo, shule za sekondari 23 zilipatiwa sh. bilioni 2 kwa ajili ya fidia ya ada, chakula kwa shule za bweni na posho ya madaraka kwa wakuu wa shule.

 

Akielezea utekelezaji wa mfumo wa uboreshaji wa miundombinu ya shule wa Lipa Kutokana na Matokeo (EP4R) uliotekelezwa tangu 2015 hadi 2020, Mheshimiwa Majaliwa alisema sh.  milioni 309 zilitolewa kwa ajili ya ukamilishaji wa miundombinu ya madarasa, vyoo na ofisi kwa shule mbalimbali zikiwemo Kalendelo, Murutunguru na Kakerege.

 

Kwa upande wa shule za sekondari, alisema shilingi milioni 873 zilitolewa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya madarasa, vyoo na maabara kwa shule mbalimbali ikiwemo; Bukongo, Pius Msekwa, Bwisya, Muriti na Lugongo.

 

Mapema, akiwa Bwisya kwenye kisiwa cha Ukara, Mheshimiwa Majaliwa alitembelea kituo cha afya cha Bwisya na kukagua wodi ya wanaume na ya wazazi. Akiwa wodini, alielezwa kwamba uwepo wa kituo hicho umewaokoa akinamama wajawazito ambao zamani walilazimika kuvuka kwenda hospitali ya wilaya iliyoko Nansio ili kupata huduma za upasuaji.

 

Mkazi wa Bwisya, Bibi Chausiku Kalemo Kategu alisema amepita mjukuu baada ya mwanaye kuwafanyiwa upasiaji kwenye kituo hicho na akajifungua salama saa 8 za usiku. “Taarifa kuwa ukipata mtoto wa kike unadaiwa sh. 40,000 na na kiume sh. 50,000 siyo za kweli kabisa. Tena watu walikuwa wanasema kituo hiki kimejengwa kwa damu za watu, ni uongo mtupu,” alisema mama huyo.

 

Kabla ya kukagua kituo hicho, Mheshimiwa Majaliwa alikwenda kuweka shada la maua kwenye mnara wa kumbukumbu ya watu waliokufa kwenye ajali ya kivuko cha MV Nyerere, Septemba 20, 2018. Ibada fupi ya kuwaombea marehemu hao iliongozwa na Padre Peter Paul wa Parokia ya Nyamwaga, Ukara na Sheikh Mudhakiru Maguza wa msikiti wa Bwisya.

 

Kuhusu usafiri wa majini, Mheshimiwa Majaliwa alisema kivuko cha Ukara hadi Bugolora  ujenzi wake umefikia asilimia 95 na kwamba imebakizwa kazi ya ukaguzi ili kiwe tayari kwa matumizi..

 

Aliuagiza uongozi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) uhakikishe unakamilisha kazi ya ukaguzi wa kivuko hicho ili ifikapo Oktoba mosi, kivuko hicho kianze kufanya safari zake kati ya Ukara na Bogolora (Nansio).



Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news