Makachero wa TAKUKURU walivyomsomea ramani Mwalimu Mkuu akitaka kuvunja amri ya sita na mwanafunzi wake 'gesti'

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani Mbarali mkoani Mbeya inamshikilia Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyeregete, Bw.Adelhard Mjingo (44) kwa kosa la kutaka rushwa ya ngono kutoka kwa mwanafunzi wake mwenye umri wa miaka 14, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Picha ya Satelite ikionyesha ineo ambalo makachero wa TAKUKURU walitumia mbinu zao kuzima nia ovu ya Mwalimu Mkuu huyo. (Diramakini).

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mbeya, Julieth Matechi ameyabainisha hayo leo Septemba 25, 2020 amesema, Mkuu huyo wa shule ametenda kosa hilo kinyume cha kifungu cha 25 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007.

Amesema, TAKUKURU ilipokea taarifa kutoka kwa raia mwema kuwa, mwanafunzi wa Shule ya Msingi Nyeregete amekuwa akiombwa rushwa ya ngono na mwalimu wake mkuu kwa ahadi ya kumsaidia katika mtihani wake wa darasa la saba.

Pia amesema, mwalimu huyo alikuwa amemtishia mwanafunzi huyo kuwa endapo angemkatalia kufanya nae mapenzi angefanya kila liwezekanalo kuhakikisha kuwa, mwanafunzi huyo hafaulu mtihani wake wa kumaliza darasa la saba.

Matechi amesema, TAKUKURU baada ya kupata taarifa hiyo ilifuatilia na kujiridhisha na taarifa iliyotolewa na kuamua kuweka mtego na kufanikiwa kumkamata, mwalimu huyo Septemba 23, 2020 ndani ya chumba cha nyumba ya kulala wageni iitwayo Executive iliyopo Rujewa mjini Mbarali akiwa na mwanafunzi wake wa darasa la saba kabla mtuhumiwa hajatekeleza dhamira yake ovu dhidi ya mwanafunzi huyo.

"Siku hiyo ya tukio mwalimu huyo alikuwa ameaga shuleni kuwa anaenda kwenye semina ya chanjo Rujewa Mbarali na aliondoka na waalimu wenzake, lakini alipofika kwenye semina alisaini na kuomba udhuru na kuelekea Guest House na wakati ho alikuwa amekwisha mwambia mwanafunzi huyo arudi nyumbani na abadili nguo aende kumchukua na kumpeleka eneo watakalokutana.

"Hivyo mwalimu baada ya kufika alicvhukua chumba na kumpokea mwanafunzi na kuingia nae chumbani, alimuuliza mwanafunzi kama amekula na alipojibiwa hajala alitoka na kumnunulia chipsi na soda na kurudi chumbani kwa lengo la kutimiza adhima yake mbaya. Ndipo makachero wa TAKUKURU waliokuwa wakifuatilia tukio hilo waliingia na kumuweka chini ya ulinzi mwalimu huyo.

"Uchunguzi wa tuhuma hii unaendelea kwa mujibu wa sheria na baada ya kukamilika hatua zitachukuliwa dhidi ya mtuhumiwa ikiwa ni pamoja na kumfikisha mahakamani.

"Kukamatwa kwa mwalimu huyo ni matunda ya uanzishwaji wa klabu za wapinga rushwa mashuleni na vyuoni na mafunzo ya kampeni ya vunja ukimya, kataa rushwa ya ngono ambayo tumeendelea kuitoa kwa vijana wetu ili kuwajengea ujasiri wa kukataa rushwa ya ngono kwa kutoa taarifa na kuwa sehemu ya mapambano dhidi ya rushwa.

"Natumia fursa hii kuwapongeza wale wote ambao wameendelea kushirikiana na TAKUKURU kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa. Nazidi kuwasisitiza kuvunja ukimya na kukataa rushwa ya ngono kwa kutoa taarifa ya vitendo hivyo katika ofisi zetu zilizopo katika wilaya na mikoa yote. Kutumia huduma ya simu kwa kupiga namnba 113, kuandika ujumbe mfupi wa maneno kwenda namba 113 au kubonyeza  *113# na kufuata maelekezo. Huduma hii ni bure na ni rahisi kwa mtu yeyote mwenye simu ya mkononi. Taarifa zitapokelewa na kufanyiwa kazi kwa usiri.

"Nipende kuwakumbusha watu wote wenye dhamana na mamlaka mbalimbali ambao wanahudumia jamii kutotumia nafasi walizonazo kushawishi au kuomba rushwa ya ngono kama kigezo cha kutoa huduma, kwani kwa kufanya hivyo ni kosa na inasababisha athari za kiuchumi na kijamii,"amesema Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mbeya, Julieth Matechi.

No comments

Powered by Blogger.