Mario Millinga kutoka CHADEMA anadi vipaumbele vinavyogusa maisha ya wakulima wa kahawa,wafanyabiashara,,wafugaji na watumishi

MGOMBEA Ubunge kupitia tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Jimbo la Mbinga Mjini mkoani Ruvuma, Mario Millinga amesema endapo wananchi watampa ridhaa ya kuwa mwakilishi wao atahakikisha anafufua zao la kahawa ambalo limekuwa muhimu kiuchumi  na tegemeo kubwa.

Ameyasema hayo wakati alipokuwa akinadi sera za chama hicho kwa wananchi wa jimbo la Mbinga Mjini waliofika kumsikiliza kwenye mkutano wake wa kampeni uliofanyika kwenye viwanja vya Soko la Mazao.

Amesema kuwa, tangu Serikali ianzishe mfumo wa vyama vya ushirika uzalishaji wa zao hilo umeshuka na kuporomoka kutokana na baadhi ya wakulima kukata tamaa baada ya mfumo huo kuwawekea mazingira magumu ya kukopeshwa pembejeo za kilimo kwa urahisi toka kwa wafanyabiashara.

“Kabla ya kuanza kwa mfumo huo wakulima walikuwa wanaweza kuhudumia mashamba yao kutokana na kupata mkopo wa pembejeo za kilimo kama vile madawa kwa urahisi kutoka kwa wafanyabiashara kwa madai kwamba mfumo ule uliwasaidia kujiamulia mahali pa kuuzia kahawa yao kwa ajili ya kutatua matatizo na changamoto mbalimbali zinazowakabili kwa urahisi tofauti na ilivyo sasa,

Amesema kuwa, endapo wananchi watakipigia kura chama hicho na kushinda katika uchaguzi mkuu ujao Oktoba 2,8 mwaka huu atahakikisha anaanzisha maabara ya kilimo na kituo cha utafiti ili wakulima waweze kulima kilimo chenye tija na bora kwa ajili ya kujiinua kiuchumi pamoja na kufuta tozo zote kandamizi zinazowakabili wakulima hao.
Aidha amevitaja vipaumbele vyake atakavyoanza navyo pindi atakapochaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo kuwa ni kuanzisha soko huria la kuuzia mazao ya kahawa na mahindi, kuhakikisha kwenye zahanati na vituo vya afya vinakuwa na madawa ya kutosha,kuboresha mazingira ya wodi ya mama na mtoto pamoja na kujifungulia akina mama.

Mgombea huyo pia ameongeza kuwa pindi akiwa madarakani atahakikisha anatatua changamoto nyingine mbalimbali zikiwemo kuboresha miundombinu ya barabara,kuboresha huduma ya maji safi na salama,kutoa elimu ya ujasiriamali kwa wananchi, kufuta sheria kandamizi na manyanyaso kwa wananchi.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wa Wilaya ya Mbinga,  Steven Mateso amewataka wananchi wilayani humo kujitokeza kwa wingi katika mikutano ya kampeni na siku ya kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu ujao kusudi waweze kukichagua chama hicho ili kiweze kupima mji wa Mbinga kwa lengo la kuwarahisishia wananchi kupata mikopo ya fedha katika taasisi za fedha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news