Mgombea Urais Dkt.Hussein Ali Mwinyi:Vijana msiyumbishwe wala kurubuniwa

Mgombea Urais Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt.Hussein Ali Mwinyi (CCM) amewataka vijana kutokubali kuyumbishwa, kurubuniwa na watu wasiopenda maendeleo kwa kushawishiwa kuvunja amani na utulivu kwa kisingizio cha siasa na dini, kwani bila amani hakuna maendeleo, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Dkt.Mwinyi ameyasema hayo leo Septemba 26,2020 kwenye Kongamano la Siku ya Amani Duniani ambalo limefanyika katika Ukumbi wa Shekh Idris Abdul wakil Kikwajuni jijini Zanzibar.

Amesema kuwa, ni muhimu kujifunza yaliyotokea nchi za wenzetu baada ya kuvunja amani ambapo waathirika wakubwa ni wanawake na watoto.

Pia amesema, Tanzania ina bahati kwa kuwa na amani na wananchi wanapenda utulivu, hivyo sio vyema kuharibu amani ya nchi kwa kisingizio cha siasa.

Hata hivyo Dk.Hussein ameongeza kusema kuwa vijana waendelee kuwa na imani na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wagombea wake kwani wanania ya kukuza uchumi na kutengeneza ajira kwa vijana.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Vijana Utamaduni Sanaa na Michezo Zanzibar, Amour Hamil Bakari amesema, dhamira ya kuandaa kongamano hilo ni kwenda sawa na Siku ya Amani Duniani ambayo inaongozwa na kaulimbi ya 'Tumarishe Amani kwa Pamoja'

Ametumia nafasi hiyo kuwataka vijana kuendelea kudumisha amani, upendo na mshikamano ukiwemo utulivu hususani katika kipindi hiki ambacho nchi inaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu.

No comments

Powered by Blogger.