'Mpewa hapokonyeki’, ‘Zanzibar ya Dkt.Hussein Mwinyi’ yasimamisha Jiji la Zanzibar

WANACHAMA na wapenzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) usiku wa jana walikongwa nyoyo zao baada ya kikundi cha Culture Musical Club kutumbuiza katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul Wakil, mjini hapa.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt. Ali Mohamed Shein akiwa na Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia CCM, Dkt.Hussein Mwinyi wakifurahia jambo wakati wa Taarab maalum ya kumpongeza Mgombea Urais wa Zanzibar CCM kwa kuteuliwa na chama chake kugombea nafasi ya Urais, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi  Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni jijini Zanzibar usiku wa kuamkia leo. (Picha na Ikulu).

Burudani hiyo ambapo mgeni rasmi alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein, ilikuwa na lengo la kumpongeza Dkt.Hussein Mwinyi kwa kuteuliwa kuwa mgombea wa Urais wa Zanzibar kutoka CCM.

Katika taarabu hiyo nyimbo mbalimbali mpya na za zamani ziliimbwa na kuwafanya wapenzi wa muziki huo wa taarabu asilia kushindwa kujizuia kwenye viti vyao muda wote.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Ali Mohamed Shein na (kulia kwa Rais) Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia CCM, Dkt.Hussein Mwinyi, Mke wa Rais wa Zanzibar Mama
Mwanamwema Shein na Mke wa Mgombea Urais wa Zanzibar, Mama Maryam Mwinyi, wakipiga makofi kumpongeza msanii wa Kikundi cha Taarab cha Culture Musical Bwa. Iddi Suwed, baada ya kumaliza wimbo wake wa “Kama Kupenda ni Dhara”  wakati wa hafla ya Taarab rasmin iliofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni jijini Zanzibar usiku wa kuamkia leo.(Picha na Ikulu).

Miongoni mwa nyimbo hizo ni pamoja na ile ya ‘pongezi kwa mgombea’ iliyoghaniwa kwa umahiri mkubwa na al-anisa Fatuma Dawa.

Nyingine ni ‘Mpewa hapokonyeki’ (al-anisa Mtumwa Mbarouk), ‘hongera Dkt. Shein (ustadh Idd Suweid),’wahoi (al-anisa Sabina Hassan) pamoja na ‘Tunapendana iliyoghaniwa na mwimbaji maarufu al-anisa Fatma Abdisalami.

Aidha, nyimbo nyingine ambazo ziliwafanya wasikilizaji kutabasamu na kuibua shangwe na nderemo ilikuwa ni pamoja na ‘Zanzibar ya Dkt.Hussein Mwinyi’ iliyoimbwa na al-anisa Mgeni Khamis, ‘Haya maumbile yangu (al-anisa Amina Abdalla), ‘kama kupenda ni dhara (ustadh Idd Suweid) pamoja na ‘Mazoweya yana taabu iliyoghaniwa na al-anisa Fatma Dawa.

Katika hatua nyingine, mgombea wa Urais wa Zanzibar kutoka CCM, Dkt.Hussein Mwinyi alitumia fursa hiyo kuzungumza na washiriki wa burudani hiyo na kutoa shukurani za dhati kwa Dkt.Shein kwa kuandaa burudani hiyo iliyofana.

Alisema, kwa kipindi chote tangu alipoteuliwa na chama hicho kuwa mgombea wa kiti cha Urais wa Zanzibar mjini Dodoma, ameendelea kupata ushirikiano mkubwa na wanachama wa chama hicho, chini ya uongozi wa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar.

Aidha, ameelezea kuridhishwa kwake na maandalizi ya kampeni yanayoendelea kufanyika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu.
Dkt. Mwinyi aliahidi kuyaendeleza mambo yote mazuri yaliosisiwa na mtangulizi wake pamoja na kuweka ahadi ya kufanyika burudani ya aina yake baada ya chama hicho kufanikisha azma yake na kuingia Ikulu.

Hafla hiyo iliyoandaliwa na Ofisi Kuu ya CCM Zanzibar pia iliwashirikisha viongozi mbalimbali wa Serikali, akiwemo mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mama Mwanamwema Shein, Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd, mke wa Makamu wa Pili wa Rais, Mama Asha Ali Idd pamoja na mke wa mgombea Urais wa Zanzibar Mwinyi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news