Mtego wa polisi wanasa makachero wa kujipachika, matapeli wa Kimataifa

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limefanikiwa kuwakamata majambazi tisa ambao wamekuwa wakiwatapeli watu kwa njia ya mitandao, anaripoti MWANDISHI WETU wa DIRAMAKINI kutoka DAR ES SALAAM.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, SACP Lazaro Mambosasa.

Kati ya wahalifu hao, saba ni raia wa kigeni kutoka mataifa tofauti ikiwemo Nigeria, Liberia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Afrika Kusini na India. 

Hayo yamethibitishwa na Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, SACP Lazaro Mambosasa.

Amesema,kutokana uchunguzi uliofanywa na jeshi hilo umewakamata na kuwa watachukuliwa hatua za kupelekwa mahakamani na kushtakiwa kwa mujibu wa sheria na na ametoa onyo kwa wale wote wanaondelea kufanya vitendo hivyo kuacha mara moja ikiwa ni pamoja na kuwaomba wananchi kutoa taarifa wanapobaini kuwepo kwa matukio kama hayo.

Kamanda Mambosasa amewataja watuhumiwa hao kutoka mataifa mbalimbali ya kigeni kwa tuhuma za kufanya uhalifu kwa njia mtandao kuwa ni Adewale Nuren Oyedes (34) raia wa Nigeria, Ibrahim Darbey (44) raia wa Liberia,Cream Milton Elias (38) raia wa Liberia, Basube Dominic (44) raia wa DRC,Prince Tito (46) raia wa Liberia, Sibongile Arhur (44) raia wa Afrika Kusini na Baljit Singh (28) raia wa India.

Mambosasa amesema kuwa, jeshi hilo linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kujifanya maofisa usalama wa Taifa, polisi na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambao ni Patrick Tarimo (32) mkazi wa Mwenge ambaye anajitambulisha kama Afisa Usalama wa Taifa. 

Mwingine ni Castory Wambura (57) mkazi wa Kibamba ambaye anajitambulisha kama Afisa wa Polisi na kwamba watuhumiwa wote wawili wamekuwa wakitapeli raia wema kwa kujifanya waajiriwa wa Idara ya Usalama wa Taifa na Jeshi la Polisi.Matukio mapya soma hapa.

“Mtuhumiwa Patrick Tarimo mnamo tarehe 10 mwezi wa 8 mwaka 2020 alijipatia kiasi cha sh.milioni 20,000,000 kutoka kwa raia wa kigeni ambapo alimkamata na kujitambulisha kuwa yeye ni Afisa Usalama wa Taifa na kufanikiwa kujipatia kiasi hicho,”amesema Kamanda Mambosasa.

“Kwa upande wa mtuhumiwa Castory Wambura mnamo tarehe 21 mwezi wa 8 mwaka huu 2020 alitapeli kiasi cha sh.15,000,000 kutoka kwa wafanyabiashara watano wa Kariakoo, ambapo alijitambulisha kuwa yeye Afisa wa Polisi na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),”amesema.

No comments

Powered by Blogger.