Mwenyekiti CCM Mkoa wa Mara avuruga mipango ya Ester Bulaya, Bunda Mjini wasema 'MitanoMadiwani, MitanoUbunge, Mitano JPM'

*Kangi Lugola, Kabaka wanogesha uzinduzi, wasisitiza kura zote CCM, Maboto asema baada ya Oktoba 28 kuna mambo mazuri Bunda Mjini

PENGINE huenda ni matani!Lakini ukweli ni kwamba sauti za maelfu ya wananchi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamesema kuwa, mgombea Ubunge Jimbo la Bunda Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA,Ester Bulaya anapaswa kujiandaa kustaafu siasa au kama itampendeza ajiunge chama tawala ili huko mbeleni aonewe huruma, anaripoti AMOS LUFUNGILO (Diramakini) MARA.

Hayo yamejiri leo Septemba 15, 2020 wakati chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bunda kikizindua kampeni za wagombea wa Udiwani na Ubunge katika Jimbo la Bunda Mjini.

Uzinduzi huo unalenga kuomba kura na kunadi sera zake kwa wananchi katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu, ambapo kimewaomba wananchi wakichague kiweze kuwaletea maendeleo huku wakiridhia kufanya hivyo ifikapo Oktoba 28, mwaka huu ambapo wamesema watawachagua madiwani, Mbunge wa Bunda Mjini, Robert Chacha Maboto na Dkt.John Magufuli kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mara, Samwel Kiboye (Namba Tatu) mwenye kofia akimnadi mbele ya maelfu ya wananchi Mgombea Ubunge wa Jimbo la Bunda Mjini, Robert Chacha Maboto katika uzinduzi wa kampeni leo Septemba 15, mwaka huu Mjini Bunda.(Picha na Amos Lufungulo/Diramakini).

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hizo zilizofanyika Mjini Bunda, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Samwel Kiboye (Namba Tatu) amesema Rais Magufuli ameweza kushinda janga la Corona kwa kumtegemea Mungu tofauti na mataifa mengine.

Pia ametekeleza miradi mingi mikubwa ya maendeleo nchini kupitia fedha za ndani, jambo ambalo limeifanya nchi iweze kupaa kiuchumi, na hivyo amewaomba Wanabunda wamchague tena yeye Rais Magufuli, wabunge na madiwani aweze kuendelea na utumishi wa kuwatumikia Watanzania.

Huku akishangiliwa na maelfu hao, Kiboye amesema Mara kwa sasa inahitaji viongozi wenye maono mema kwa ajili ya kuuwezesha mkoa na Bunda kwa ujumla kupiga hatua, kwani dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kutekeleza kila mradi kufikia matokeo chanya.

Kwa upande wake Mgombea Ubunge kupitia chama hicho, Jimbo la Bunda Mjini, Robert Chacha Maboto amesema, endapo atachaguliwa atahakikisha anashirikiana na Serikali kutatua changamoto za maji, kuimarisha utoaji wa mikopo kwa kinamama na vijana, barabara, huku akisisitiza kuwa hata madiwani wa chama hicho wakichaguliwa watashirikiana kwenye miradi ya maendeleo ya jimbo hilo kwa manufaa ya wananchi wa jimbo hilo.

Sehemu ya umati wa maelfu ya wananchi waliofurika mjini Bunda leo wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa kampeni zilizohutubiwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Samwel Kiboye (hayupo pichani). (Picha na Amos Lufungulo/Diramakini).

"Fedha za miradi ya maendeleo zitakazotolewa na Serikali nitazilinda kama mboni ya jicho, hususan kinamama vijana na walemavu na watu wa chini wapate manufaa ya watu kuiweka madarakani CCM na hii ndiyo shabaha kubwa niliyonayo kwa maslahi ya Wanabunda,"amesema Maboto.

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mara, Shaibu Ngatiche amesema kuwa , Wanabunda wanapaswa kukichagua Chama Cha Mapinduzi kuanzia madiwani hadi Rais kwa ajili ya kupata mnyororo bora wa kuwaletea maendeleo katika Jimbo la Bunda Mjini na kutatua changamoto zilizopo ndani ya jimbo hilo.

"Wapo waliofikiri kura za maoni zingeigawa CCM, hii ni CCM mpya chini ya Rais Magufuli chama kipo imara na thabiti sana kushinda kwa kishindo kuanzia madiwani na hadi Rais, na umoja huu utatuwezesha kushinda kwa kishindo na kuweza kuendelea kuwaletea maendeleo Watanzania," amesema.

Naye Mbunge wa Jimbo la Mwibara aliyemaliza muda wake Kangi Lugola amesema, wananchi wa Jimbo la Bunda Mjini wamchague Robert Chacha Maboto ambaye ndiye chaguo la Chama Cha Mapinduzi ili aweze kutekeleza ilani ya chama akishirikiana na Serikali ya Rais Magufuli na siyo kuchagua mgombea wa chama cha upinzani ambaye hawezi kuwa na msaada kwa maendeleo yao.

"Wananchi wa Bunda tusitoe Ubunge ovyo ovyo, tukichague Chama Cha Mapinduzi ambacho ndicho chama pekee chenye dira ya kuleta nuru ya maendeleo. tusipochagua Chama Cha Mapinduzi Bunda Mjini maendeleo hayatapatikana kwa haraka, tuzingatie hata ushauri wa Rais alipopita hapa alisema tumchague Maboto ili changamoto za Bunda ziweze kutatuliwa,"amesema Kangi.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Taifa ( UWT), Gaudencia Kabaka, amewataka kinamama wote kujitokeza kupiga kura siku ya uchaguzi mkuu ili chama hicho kishinde na kuanza utekelezaji wa mikakati yake ya kutekeleza ilani ya uchaguzi ambayo imesheheni mambo mengi ya kutekeleza kwa Maendeleo ya Watanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news