Mwenyekiti CCM Mkoa wa Mara awataka wenzake kupangua madai ya uongo yanayolenga kumchafua Rais, awapongeza Makamu wa Rais, Majaliwa

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Samuel Kiboye (Namba Tatu) amewataka viongozi kuanzia ngazi ya mashina hadi juu kuhakikisha wanamsaidia mgombea Urais kupitia CCM ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Magufuli kujibu hoja zinazotolewa na wapinzani ambazo zinalenga kupotosha Watanzania na kuwaondoa katika mwelekeo sahihi, anaripoti Mwandishi Diramakini.

"Ukweli ni kwamba Mheshimiwa Rais Dkt.Magufuli anachoka sana huku kunadi sera na ilani ya chama, huku kujibu hoja za wapinzani, hilo linapaswa tulifanyie kazi sisi viongozi wa chama, haiwezekani kumchosha, inabidi sasa tuanze kufanya kazi ya kuwapa majibu hao wenye hoja nyepesi nyepesi ambazo hazina nyuma wala mbele.

"Watambue kuwa, ishara ya hoja nyepesi ni hatua ya kuona kuwa, mbeleni ushindi hamna,na kweli ushindi kwao hamna maana Watanzania na Dunia inajua kuwa, yupo mtu mmoja ambaye ameibadilisha Tanzania kwa miaka mitano tu, tena kwa kutumia rasilimali za ndani na huyo si mwingine bali ni Dkt.John Pombe Magufuli, hivyo wanapoibuka na hoja za ovyo ovyo, basi tuwajibu sisi viongozi wa chini, Rais aendelee kunadi sera na ilani ili ushindi wa Oktoba 28, mwaka huu ukawe wa kishindo tena kishindo cha kutisha;

Kiboye ameyasema hayo mjini hapa wakati akielezea juu ya namna ambavyo chama mkoani hapa kimeridhishwa na namna ambavyo Dkt.Magufuli anaendesha kampeni za kistaarabu na zenye kujikita katika masuala ya Watanzania kuliko wanaojikita katika mambo binafsi.

Pia ametumia nafasi hiyo kuwapongeza Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa kwa namna ambavyo wanafanya kazi nzuri ya kumsaidia Rais Dkt.John Magufuli kuelekea Oktoba 28, mwaka huu.

Amesema, viongozi hao wamekuwa mstari wa mbele kujikita katika sera na ilani ya chama, hivyo kuendelea kuwapa mwanga wananchi kuhusu mambo mbalimbali ambayo yamefanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, jambo ambalo litawasaidia wananchi ifikapo Oktoba 28, mwaka huu kufanya uamuzi sahihi wa kuwapa wagombea wote wa CCM kura za kishindo.

"Na hatua hiyo ndiyo msingi wa kwenda kukamilisha hesabu ya ushindi kupitia mafiga matatu, kwa maana ya madiwani, wabunge na Rais kupitia CCM, hivyo nichukue nafasi hii kuwapongeza sana kwa kazi nzuri,"amesema Kiboye.


No comments

Powered by Blogger.