RC Joachim Wangabo atoa maagizo ukamilishaji Stendi Kuu ya Mabasi Sumbawanga

MKUU wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo ametembelea Stendi Kuu ya Mabasi Sumbawanga baada ya kuona ujenzi unasuasua na kutoa maagizo.

Stendi hiyo ambayo ilitarajiwa kumalizika mwezi Juni, mwaka huu ujenzi wake umeonekana kusuasua, hivyo baada ya mkuu huyo wa mkoa kufanya ziara ametaka kupewa maelezo juu ya mkwamo wa ujenzi huo.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa,Joachim Wangabo akikagua ujenzi wa vyoo vya kulipia vilivyopo ndani ya jengo la abiria katika Stendi Kuu ya Mabasi Sumbawanga.

Ikiwa huo ni miongoni mwa miradi ya kimkakati ya mkoa katika kuongeza mapato ya Manispaa ya Sumbawanga. Miradi mingine ya kimkakati.

RC Wangabo amesema kuwa, ukamilifu wa stendi hiyo utaongeza shughuli nyingi za kiuchumi kwa wananchi hasa wajasiriamali pamoja na wafanyabiashara mbalimbali wa ndani na nje ya mkoa kutokana na miundombinu iliyomo kwenye stendi hiyo inayotarajiwa kuongeza ubora wa utoaji wa huduma kwa abiria zaidi ya 400 kwa wakati mmoja.

“Kilichobakia ili hii Stendi Kuu ya Mabasi ifanye kazi ni kitu kidogo, ni asilimia nane tu na hiyo asilimia ni vitu vidogo vidogo ambavyo tunaweza kuvifanyia kazi, Mkurugenzi ningependa kuona stendi hii kuu ya mabasi inafanya kazi mwanzoni mwa mwezi Oktoba, jitahidini sana kutatua changamoto ya fedha ambayo amesema hapa mkandarasi mumlipe, ‘ame-raise certificate’ ya shilingi milioni 350 mlipeni.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo (katikati) alipotembelea Stendi Kuu ya Mabasi Sumbawanga ili kujionea maendeleo ya ujenzi wa stendi,Kulia ni Mkurugenzi wa Sumry Enterprises Ltd, Humud Sumry pamoja na Meneja wa TARURA Manispaa ya Sumbawanga, Mhandisi Suleiman Mziray.

“Stendi ikianza kufanya kazi mtaendelea kuingiza mapato, mtalipana tena polepole wakati mnafuatilia hela hazina na mahali pengine kama mlivyosema kuliko kukaa kimya kunakuwa na mdororo, halafu kunakuwa na maswali mengi yasiyokuwa na majibu, lakini pia tunapokaa muda mrefu kuna vitu vinaweza kuanza kupotea, halafu maumivu ya stendi kutofanya kazi yakawa makubwa zaidi,”amesema RC huyo.

Pia amemuagiza mkurugenzi kuhakikisha anakamilisha miundombinu ya maji kabla ya stendi hiyo kuanza kutumika pamoja na kumtaka kuwa makini na watumiaji wa huduma zinazopatikana katika stendi hiyo ikiwemo utunzaji wa vyoo na kumtaka Katibu Tawala wa Mkoa kuhakikisha Mkandarasi analipwa fedha anazodai ili stendi hiyo ikamilike kwa wakati.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, James Mtalitinya almekitri kuwa fedha zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa stendi hiyo tayari zimeisha na chanzo pekee cha fedha kilichobaki kwa ajili ya kumlipa mkandarasi ni makusanyo ya ndani ya halmashauri pamoja na kutegemea kuomba fedha kutoka Serikali Kuu.

“Tumekuwa tukishauriana na mkandarasi hasa aweze kukamilisha jengo hili la abiria angalau aweze kufunika hizo ‘fisher board’ angalau muonekano wa jengo na huduma zinazoweza kuanza ziweze kuanza kwa sababu mahitaji makubwa hapa ni maji pamoja na ukamilishaji wa muonekano wa jengo, kwa hiyo hayo tumeendela kushauriana nae ili kuyakamilisha na stendi ianze, ndio maana kazi nyingine zote tumezisimamisha kwa sasa,"amesema.

Wakati akisoma taarifa ya ujenzi wa stendi hiyo, Meneja wa Wakala wa Barabara za Mjini na Vijiji (TARURA) Manispaa ya Sumbawanga, Mhandisi Suleiman Mziray amesema kuwa, katika mkataba wa awali stendi hiyo ilitakiwa kujengwa pamoja na jengo la chini pekee kwa gharama ya shilingi bilioni 5.4, lakini Kamati ya Uchumi na Fedha ya Manispaa ilishauri lijengwe ghorofa na hivyo gharama kuongezeka na kufikia shilingi Bilioni 5.9.

“Vilevile wakati wa utekelezaji wa mradi huu kulikuwa na kazi zinaonekana zinaongezeka, ikapelekea mpaka mkataba tulionao sasa hivi kufikia bilioni 7.2 na kazi Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa ilianza tarehe 24 mwezi Aprili 2019 na inategemewa kumalizika tarehe 20, Septemba 2020 na kwa ujumla ujenzi umekamilika kwa asilimia 92,”amesema.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Sumry Enterprises, Humud Sumry amesema kuwa, jambo kubwa linalokwamisha ujenzi wa stendi hiyo ni upatikanaji wa fedha ambapo wanadai karibu shilingi bilioni mbili huku akionyesha wasiwasi wa kulipwa fedha hizo kwa wakati na kutoa maombi yake.
Muonekano wa sehemu ya kuegesha mabasi katika Stendi Kuu ya Sumbawanga.

"Maombi yangu, serikali iangalie kuisaidia manispaa ili kuonekana wapi pesa inapatikana ili kumalizia kilichobaki na stendi itumike na kuleta tija kama mradi ulivyokususdiwa,"amesema.

Stendi hiyo ya mabasi ikianza kutumika itakuwa na jengo la abiria 400, kituo cha polisi,baa,vyumbwa 16 vya kulala wageni, sehemu ya mazoezi (GYM), ofisi 24 za kukatia tiketi, vyoo vya kulipia, vyumba vya benki na ATM, vibanda vya mlinzi na maduka 100.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news