Same mpya, tabasamu jipya, wakulima wa Tangawizi ni mwendo wa maendeleo tu, kiwanda cha tangawizi mambo waziwazi

Kilio cha muda mrefu cha wananchi wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro cha kupata Kiwanda cha Kuchakata Tangawizi, sasa kimepata ufumbuzi na kitaanza kufanya kazi mwezi Novemba, mwaka huu baada ya kupata mwekezaji,anaripoti Pius Ntiga, Same.

Kiwanda hicho kilichoanzishwa mwaka 2012, kilifanya kazi kwa muda mfupi kikaharibika chini ya Chama Cha Ushirika cha Tangawizi Mamba, Miamba, ambapo sasa kimeingia ubia na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii-PSSSF na kitaanza kufanya kazi Novemba, mwaka huu.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Uwekezaji-PSSSF, Fortunatus Magambo katika Kata ya Mamba, miamba wakati akikabidhi rasmi mashine za kuchakata Tangawizi zilizotolewa na mfuko huo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Same, Rosemary Senyamule.

Katika mkutano na wananchi wa Mamba, Miamba ambao ulihudhuriwa pia na Amsha Amsha 2020 ya Uhuru FM kijijini hapo, Magambo amesema mashine hizo za kisasa zimenunuliwa nchini China kwa gharama ya shilingi Bilioni-1.83 na zinafanya kazi bila kutoa sauti.

Kwa mujibu wa ubia huo PSSSF ina hisa ya asilimia 60 huku 40 zikiwa ni za wananchi wa Wilaya ya Same ambao zao lao kuu la biashara ukiachia Mkonge ni Tangawizi.

Aidha, amesema kiasi cha shilingi milioni-800 zitatumika kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa majengo ya kiwanda, Ofisi, Hospitali, Karakana na miundombinu pamoja na matumizi ya awali ya kiwanda hicho.

"Tunataka kuona mradi huu unakamilika na kusaidia kuboresha hali ya maisha ya wananchi wa Same na utakamilika kwa wakati,"amesema Magambo.

"Wataalamu kutoka China wanatarajiwa kuwasili nchini mwezi Oktoba, mwaka huu kwa ajili ya kufunga Mashine hizi tayari kwa kuanza uzalishaji." Aliongeza Magambo.Naye Mkuu wa Wilaya ya Same, Rosemary Senyamule amewaambia wananchi waliohudhuria mkutano huo kuwa Serikali ya Awamu Tano imejipambanua kuwa ni Tanzania ya viwanda, hivyo uwepo wa kjwanda hicho utachochea kukuza vipato vyao na Taifa kwa ujumla.

Amesema, tani 5,000 kwa mwaka zinahitajika kiwandani hapo, hivyo akawataka wakulima kuongeza uzalishaji wa Tangawizi ambayo itakuwa inasindikwa hapa hapa nchini kwa matumizi ya hapa nchini na nje ya nchi.

Aidha, DC Rosemary amesema Soko la Tangawizi litakuwa kubwa mara kitakapoanza uzalishaji kiwanda hicho cha kusindika Tangawizi .

Pia amewataka wananchi kuwapuuza wanasiasa wakiwemo wa upinzani wanaojipitisha kwao wakidai kuwa mashine za kiwanda hicho wamezileta wao wakati zimeletwa na Serikali ya Awamu ya Tano.

"Wananchi wangu wa Same hasa hapa Mamba,  Miamba, Corona ilichelewesha ufungaji wa mashine hizo, lakini sasa zipo hapa na nyie leo mmeshuhudia, hivyo muda wowote zitaanza kufanya kazi, endeleeni kuiunga mkono serikali yenu," amesema DC Rosemary.

Wakizungumza na Amsha Amsha 2020 ya Uhuru FM, baadhi ya wananchi akiwemo Mzee Ndimangwa Manento, aliyetoa shamba lake kwa ajili ya kujengewa kiwanda hicho cha Tangawizi, wameishukuru Serikali kwa kusikiliza kilio chao cha kuleta mashine za kisasa zisizo na sauti na wakawaomba wananchi wenzao mwaka huu wasifanye makosa katika Uchaguzi Mkuu wakampigie kura nyingi Rais Magufuli,wabungena madiwani wa CCM.

Wakati huo huo, zaidi ya shilingi Milioni-400 zimetumika kujeng majengo mapya ya Kituo cha Afya cha Ndungu ikiwemo Maabara, Chumba cha Kuhifadhi Maiti,  Jengo la Upasuaji, pamoja na Wodi ya Akina mama wajawazito. 

Hayo yamesema na Afisa Mipango Halmshauri ya Same,  Simion Mzee wakati akizungumza na Amsha Amsha 2020 ya Uhuru FM.

Nao baadhi ya wananchi wa Ndungu akiwemo Hatibu Mlindoko, wamepongeza serikali kwa kuwajengea Kituo hicho cha afya na wakaiomba serikali kupandisha Hadhi kituo hicho ili kiwe  Hospitali.

Naye, Kaimu Mganga Mkuu Kituo hicho cha Afya cha Ndungu, Hamis Waziri Juma, amesema kabla ya majengo hayo walikuwa wanatoka rufaa nyingi kwenda Hospitali ya Wilaya ya Same kwa ajili ya matibabu, lakini sasa wajawazito wanajifungua katika kituo hichi na hivyo kupunguza gharama ya wanachi kuwapeleka Same.

Katika Hatua Nyingine, zaidi ya Shilingi Milioni-60 zimetumika kwa ajili ya ukarabati wa Shule Kongwe ya Same Sekondari katika miaka mitano ya serikali ya Tano chini ya Rais Magufuli.

Mkuu wa Shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1954 Mwalimu Hoza Mgonja, amesema  Majengo 24 yamekarabatiwa yakiwemo Mabweni, Jiko,  Madarasa, Maabara, Zahanati, Ofisi na kujenga Tenki la Maji kwa ajili ya matumizi ya Shule hiyo ambayo sasa ni ya Kidato cha Tano na Sita.

Wakizungumzia mafanikio hayo baadhi ya Wanafunzi wamesema Shule hiyo sasa imekuwa ya kisasa baada ya Majengo ya zamani kubadilishwa na kujengwa mapya imesaidia pia kuongeza ufaulu na walimu kufundisha katika mazingira mazuri na wameipongeza Serikali.

Aidha, shilingi Milioni-25 zimepelekwa na serikali kukarabati na kujenga  Ofisi na Madarasa Mawili katika Shule ya Sekondari Mamba, iliyopo Kata ya Mamba, Miamba Wilayani Same Mkoani Kilimanjaro.

Kiasi hicho cha fedha kimetajwa na Mkuu wa Shule hiyo Elizabet Irira, ambaye pia ameipongeza serikali kwa kupeleka kiasi hicho cha fedha Shuleni hapo, hatua ambayo pia imepongezwa na Wanafunzi wa Shule hiyo iliyopo Milimani Kilometa 90 kutoka Mjini Same hadi Mamba, Miamba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news