Septemba 15, 2020 yawekwa katika kumbukumbu ya Dunia kwa kubadilisha historia ya Mashariki ya Kati

JANA Septemba 15, 2020 ilikuwa siku ya kihistoria baada ya Israel kusaini nyaraka za makubaliano na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Ufalme wa Bahrain, inaripoti DIRAMAKINI.

Mtukufu Mfalme Hamad bin Isa bin Salman al-Khalifa na Waziri Mkuu wa Israel,Benjamin Netanyahu wamekubaliana kufungua ukurasa mpya wa urafiki na mahusiano kwa ajili ya kuufanya Ukanda wa Mashariki ya Kati kuwa salama na mshikamano kwa ajili ya kuwafanya wananchi wa ukanda huo kunufaika.

Makubaliano ya kuhalalisha uhusiano yaliyofikiwa kati ya Israel, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Bahrain yametiwa saini katika hafla iliyoandaliwa na Rais wa Marekani, Donald Trump katika Ikulu ya White House mjini Washington.

Mbali na Rais Trump, Waziri Mkuu wa Israel, Binyamin Netanyahu, Waziri wa Mambo ya Nje wa UAE, Abdullah bin Zayid Al Nahyan, Waziri wa Mambo ya Nje wa Bahrain, Abdullatif bin Rashid ez-Zeyani na Waziri wa Mambo ya Nje wa Taifa hilo, Abdullatif Al Zayani walikutana mjini Washington.

Wakati Israel na UAE zikisaini makubaliano ya kuhalalisha uhusiano kati ya Israel na Bahrain, nchi tatu pia zilitia saini makubaliano yanayoitwa Abraham Accords.


Waziri wa Mambo ya Nje w a Bahrain,Abdullatif bin Rashid Al-Zayani,Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Rais wa Marekani,Donald Trump wakishiriki katika zoezi la utiaji saini nyaraka ya Abraham Accords katika Ukumbi South Lawn Ikulu ya White House Septemba 15, 2020 mjini Washington, DC. (Alex Wong/Getty Images/AFP).

Rais Trump katika hotuba yake wakati wa zoezi hilo aliwashukuru viongozi waliohudhuria sherehe hiyo.

"Leo tuko hapa kubadilisha historia. Baada ya miaka ya mgawanyiko na mizozo, tupo katika mwanzo wa Mashariki ya Kati mpya,"amesema Rais Donald Trump.

Pia Rais Trump ameeleza kwamba,wamechukua hatua muhimu kuelekea siku za usoni ambazo watu wa dini zote na asili zote wataishi kwa amani na ustawi na makubaliano yaliyofanywa.

Amesema, mafanikio hayo kati ya Israel, Bahrain na UAE yamefikiwa ndani ya mwezi mmoja tu, jambo ambalo linafaa kupomgezwa kwa mustakabali wa amani katika Ukanda wa Mashariki ya Kati..

Amesisitiza kwamba, nchi nyingine pia zitasaini makubaliano ya amani na Israel,"Israel, UAE na Bahrain watateua mabalozi wa pande zote mbili, na sekta mbalimbali kama utalii, biashara, afya hadi usalama zitaanza kutengeneza ushirikiano.

"Mkataba wa Abraham pia umefungua milango kwa Waislamu kote Ulimwenguni kutembelea maeneo Matakatifu huko Israel na kuabudu kwa amani katika Masjid al-Aqsa,"amesema.

Rais Trump amesema kuwa, makubaliano yaliyofikiwa yatakuwa msingi wa amani katika eneo hilo na kuongeza kuwa,

"Uongo uliorithishwa kutoka kizazi hadi kizazi kwamba Wayahudi na Waarabu ni maadui na kwamba Masjid al-Aqsa inashambuliwa imesababisha kuenea kwa ugaidi na vurugu katika eneo hilo na Ulimwenguni kote. Makubaliano haya yamesaidia watu wa eneo hilo kuachana na mambo ya kale, hivyo tunaanza ukurasa mpya,"amesema Rais Trump.

Amebainsha kuwa, katika Ulimwengu wa leo, nchi za Mashariki ya Kati hupendelea ushirikiano kuliko mizozo.

"Nchi hizi zimechagua siku za usoni ambapo Waarabu, Waisrael, Waislamu, Wayahudi na Wakristo wataweza kuishi pamoja kwa utulivu na amani, kuabudu na kutengeneza mustakabali wao bega kwa bega,"amesema Rais Trump.

Aidha, Rais Donald Trump amekumbushia pia kuwa nchi tano au sita zaidi zinaweza kusaini makubaliano ya kuhalalisha mahusiano na Israel bila ya kuyaja majina ya nchi hizo mbele ya viongozi hao.

Agosti 13, mwaka huu, Rais Donald Trump alitangaza kuwa, Israel na UAE zilifikia makubaliano ya kurekebisha kabisa uhusiano wao na Septemba 11, mahusiano yalirekebishwa kati ya Israel na Bahrain, hatua ambayo ni kubwa na yenye mafanikio.

Hata hivyo, mafanikio hayo yanakuja ikiwa Misri mwaka 1979 na Jordan mwaka 1994 zilifikia makubaliano ya kuhalalisha Israel.

Hivyo, makubaliano ya sasa kati ya Israel na UAE inakuwa nchi ya tatu ya Kiarabu huku Ufalme wa Bahrain ukiwa wa nne kuhalalisha mahusiano mema na Israel.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news