Serikali yazindua kamusi ya kwanza ya kidigitali kwa wanafunzi viziwi nchini

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imezindua Kamusi ya kwanza ya lugha ya alama ya kidijitali yenye lengo la kupunguza changamoto ya mawasiliano katika ufundishaji na ujifunzaji kwa wanafunzi viziwi nchini.

Naibu Katibu Mkuu wizara hiyo, Dkt. Ave Maria Semakafu amezindua kamusi hiyo mkoani Tabora katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya viziwi yenye kauli mbiu “Kuhakikisha upatikanaji wa haki za binadamu kwa viziwi”,

Dkt.Semakafu amesema, Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa makundi yote yenye ulemavu kupata elimu na huduma nyingine za kijamii nchini.

Amesema, pamoja na maboresho makubwa yaliyofanyika katika sekta ya elimu, kundi la viziwi lilikuwa limeachwa nyuma huku changamoto kubwa ikiwa ni mawasiliano na kutokuwepo kwa walimu wa kutosha hasa katika ngazi ya sekondari.

Dkt.Semakafu amesema, ndio maana Serikali imeandaa kamusi hiyo kuwe na lugha moja ya alama na kutoa mafunzo kwa walimu wanaofundisha katika shule zinazopokea watoto viziwi nchini.

“Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na lugha moja ya alama kwa ajili ya kuwezesha mawasiliano ya watumiaji wa lugha hiyo, hivyo itaendelea kusimamia uendelezaji na usanifishaji wa lugha ya alama ili kuwezesha utoaji elimu, kurahisisha ujifunzaji na kuboresha mawasiliano katika jamii,"amesema.

Kwa upande wake Kamisha wa Elimu, Dkt. Lyabwene Mtahabwa amesema, kilele cha maadhimisho ya wiki ya viziwi duniani ndio mwanzo wa mafanikio katika mchakato wa ujifunzaji na ufundishaji nchini kwani ni siku ambayo kamusi ya lugha ya alama ya kwanza nchini tena ya kidijitali inazinduliwa pamoja na mwongozo wa utekelezaji wa mtaala wa elimu ya sekondari kwa wanafunzi viziwi.

Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt. Aneth Komba amesema, taasisi anayoisimamia ndio walipewa jukumu la kuandaa Kamusi hiyo na kwamba imeandaliwa kwa kufuata taratibu zote ikishirikisha wadau wote na kwamba itatumiwa na wanafunzi viziwi kutoka Tanzania Bara na Visiwani.
Mkurugenzi wa Kitengo cha Elimu Maalum kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Magret Matonya amesema, uzinduzi wa Kamusi hiyo ni muendelezo wa jitihada za Serikali kuhakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalum nchini wakiwemo viziwi wanapata elimu bora.

Pia ameongeza kuwa, wizara imeanza ujenzi wa shule ya mfano ya viziwi katika Halmashauri ya Masasi mkoani Mtwara ikiwa ni jitihada za kuboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji wanafunzi viziwi ambapo ujenzi wake utagharimu shilingi bilioni 1.5.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Viziwi Taifa (CHAVITA),Selina Mlemba amesema, wanaishukuru Serikali kwa hatua hiyo na kwamba wanaamini miaka michache ijayo watapata wataalamu wengi katika maeneo mbalimbali wakiwemo madaktari kwa kuwa sasa wamepata kamusi itakayowawezesha kusoma bila changamoto.

Mtaalamu Elekezi wa Uandaaji wa Kamusi ya lugha ya alama kutoka Archbishop Mihayo University College (AMUCTA), Profesa Henry Muzale amesema, uaandaji wa kamusi hiyo umezingatia changamto zote za viziwi na hii ni kutokana na utafiti uliofanyika katika shule zenye watoto viziwi ikiwemo Njombe viziwi ambao ufaulu wao uliendelea kushuka.

Kilele cha maadhimisho ya wiki ya viziwi duniani kitaifa yamefanyika mkoani Tabora ikiwa ni hatua ya kuenzi historia ya chimbuko la elimu kwa viziwi kwani shule ya kwanza ya viziwi nchini Tanzania ilianzishwa huko.

No comments

Powered by Blogger.