Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania labaini uwepo wa viashiria vya mafuta Mto Manonga

SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeanza hatua ya awali ya utekelezaji wa mradi wa utafutaji wa mafuta katika Bonde la Mto Manonga baada ya utafiti wa awali kubaini uwepo wa miamba yenye viashiria vya mafuta katika bonde hilo.

Mradi huo ujulikanao kama Eyasi-Wembele unatatekelezwa katika mikoa ambayo mto huo unapitia ikiwemo Bonde la Ziwa Eyasi na Bonde la mto Manonga unaopatikana katika mikoa ya Tabora, Shinyanga, Singida na Manyara.

Picha ya Satelite ikionyesha taswira ya Ziwa Eyasi ambapo pia Mto Manonga hupitia. Picha na www.diramakini.co.tz

Akitambulisha mradi huo kwa uongozi wa Mkoa wa Shinyanga, Mtaalam Mshauri wa mradi huo, Dkt. Allan Mzengi kutoka TPDC amesema, mradi huo unaanza na hatua ya awali ya kuangalia athari za kimazingira katika Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga hatua itakayoshirikisha wadau kuanzia ngazi ya kata hadi mkoa.

Dkt.Mzengi ameueleza uongozi wa Mkoa wa Shinyanga kuwa, pamoja na kuangazia suala la kimazingira hatua ya pili ya mradi itakuwa ni ujenzi wa Mkuza katika eneo ambao mradi huo utatekelezwa na baadae kuweka vilipuzi vitakavyosaidia kubaini maeneo ya ujenzi wa visima vya majaribio ya utafutaji mafuta katika eneo la mradi.

Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga,Albert Msovela akiongoza ujumbe wa Mkoa wa Shinyanga kutoa maoni kwa wataalam wa TPDC waliofika ofisini kwake kutambulisha mradi wa utafiti wa mafuta katika Bonde la Mto Manonga eneo la Kishapu mkoani Shinyanga.

Naye Mjilojia kutoka TPDC, Gaston Canuty ameueleza uongozi wa Mkoa wa Shinyanga kuwa, tayari TPDC imeishachimba visima vifupi katika eneo la mradi kubaini miamba yenye uwezekano wa kuhifadhi mafuta na sasa mradi huo unakusudia kwenda mbali zaidi kuangalia mafuta yako wapi chini ya ardhi baada ya kubaini miamba hiyo katika eneo la Kishapu.

Ili kufanikisha zoezi hilo, Mjiolojia Gaston ameongeza kuwa, utafiti utatumia njia ya jiofizikia ambapo watajenga Mikuza ambayo itawekwa vilipuzi laini ambavyo vitakapolipuliwa vitawawezesha kupata data chini ya ardhi itakayowawezesha kutambua mahali penye uwezekano wa mafuta.

Baadhi ya viongozi wa Mkoa wa Shinyanga wakifuatilia kwa makini ujumbe wa wataalam wa TPDC waliofika mkoani Shinyanga kwa lengo la kutambulisha mradi wa utafiti wa awali kuhusu utafutaji wa mafuta katika Bonde la Mto Manonga Wilaya Kishapu mkoani Shinyanga.

Kwa upande wake Loveness Njogela ambaye pia ni Mjiolojia amesema, utafiti wa mafuta katika eneo la mradi ulianza kwa kutumia ndege ya utafiti ambayo iliwawezesha kuona maeneo yenye miamba yenye tabaka gumu na ile ya tabaka laini na kwa kanuni za kijiolojioa maeneo yale ambayo yana mkandamizo mkubwa wa miamba tabaka ndiyo yatakayofanyiwa jaribio la utafutaji mafuta.

Njogela ameongeza kuwa, pamoja na baadhi ya maeneo kuwa na miamba yenye mgandamizo mkubwa inayotumika kama sampuli za mafuta yana tabia ya kuhama katika eneo la miamba hiyo na kutafuta mtego mahali pengine ndio maana wataweka vilipuzi laini vitakavyowezesha kutambua ni wapi kuna uwezekano wa kuwa na mtego wenye mafuta.

Baadhi ya viongozi wa Mkoa wa Shinyanga wakifuatilia kwa makini ujumbe wa wataalam wa TPDC waliofika mkoani Shinyanga kwa lengo la kutambulisha mradi wa utafiti wa awali kuhusu utafutaji wa mafuta katika Bonde la Mto Manonga Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga.

Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga, Albert Msovela amehaidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wataalam hao kwa lengo la kufanikisha utafiti huo ambao utafanyika katika kata za Mwamalasa, Gana na Mwamashele wilayani Kishapu Mkoa wa Shinyanga.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

1 Comments

  1. Kazi nzuri, hongereni sana TPDC, endeleeni kutafiti, Tanzania ina utajiri mkubwa wa mafuta na gesi. Karibuni sana Shinyanga penye rasilimali za kutosha

    ReplyDelete
Previous Post Next Post

International news