Jumla
ya shilingi bilioni 1.79 zimetumika kwa ajili ya kufanya matengenezo Skuli ya Sekondari ya
Lumumba ili kuirejesha katika hadhi yake,anaripoti Talib Ussi (Diramakini) Zanzibar.
Akizungumza
wakati wa hafla ya makabidhiano ya Skuli ya Sekondari Lumumba baada ya
kumaliza kufanyiwa matengenezo, Mkurugenzi wa Idara ya Mipango Sera na Utafiti Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Bw.Khalid Masoud
Waziri amesema wizara hiyo imekuwa ikifanya matengenezo majengo yake
kila mwaka kupitia ruzuku ya bajeti yake kutoka serikalini ili
kuimarisha skuli zake na kutoa kiwango bora cha elimu.
Bw.Khalid amesema, matengenezo hayo yamefanyika kwa skuli yote kwa kuondoa
bati zote na kuezeka bati mpya ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba
mpya ya walimu ili kuweka walimu karibu na skuli waweze kutoa elimu kwa wanafunzi kwa ufanisi zaidi.
Amesema
kuwa, matengenezo hayo makubwa yamejumuisha maabara zote za Kemia,Biolojia na Fizikia, maktaba, madarasa ya kusomea, ofisi, nyumba ya walimu pamoja na ukumbi wa kufanyia mitihani.
Akizungumza
baada ya kusaini makabidhiano ya skuli hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar,Mhandisi Idrissa Muslim Hija
amesema, wizara yake imeanza kurekebisha baadhi ya majengo yaliochakaa
ili kuendelea kuimarisha sekta ya elimu na miundombinu yake.
Dkt
Idrisa amesema ukarabati wa skuli hiyo utasaidia kuimarika utoaji wa elimu katika mazingira bora kwa wanafunzi na kuwafanya kupata
haki yao ya elimu katika mazingira mazuri na salama.
Amesema,ushirikiano mzuri uliopo kati ya wakandarasi wa skuli hiyo pamoja na wakandarasi wa Wizara ya Elimu Zanzibar umepelekea
kuifanya kazi hiyo katika ubora.
Kwa
upande wake Mhandisi Mkuu wa Kampuni ya Modern Building Contractor
Ltd, Ali Pandu Sharif amesema wamehakikisha wanafanya kazi kwa
bidii ili kuhakikisha wanamaliza matengenezo hayo ingawa kulijitokeza
tatizo, lakini kwa ushirikiano wao mzuri na wizara tatizo hilo waliweza
kulimaliza.
Ukarabati wa skuli ya Sekondari Lumumba ulianza rasmi Januari 3, mwaka huu na kumalizika Septemba 19,2020.