Suga kutoka Liberal Democratic Party aidhinishwa kuwa Waziri Mkuu Japan

YOSHIHIDE Suga (Uncle Reiwa) ndiye Waziri Mkuu wa 99 wa Japan akiwa amechukua nafasi ya Shinzo Abe ambaye alitangaza kujiuzulu hivi karibuni kutokana na matatizo ya kiafya.

Abe aliwaeleza waandishi wa habari kuwa,afya yake ilianza kuwa ya mgogoro tangu mwishoni mwa mwezi Aprili,mwaka huu na hakutaka maamuzi yake ya kisiasa yaathiriwe kwa namna yoyote na ugonjwa. Shinzo Abe aliingia madarakani mwaka 2012.
Yoshihide Suga (wa tatu kutoka kushoto) akisheherekea ushindi. (Picha na Gettyimages).

Baada ya hatua hiyo, leo Septemba 16,2020 Bunge la Japan limemthibitisha Suga ambaye ni kiongozi wa chama tawala cha Liberal Democratic Party (LDP) kuwa Waziri Mkuu.

Suga,Waziri Mkuu huyo mpya anakabiliwa na changamoto ya moja kwa moja ya kupambana na janga la virusi vya Corona (COVID-19) nchini Japan na uchumi uliodorora kwa asilimia kubwa.

Kiongozi huyo ambaye juzi alipata ushindi mkubwa wa uongozi wa LDP ameidhinishwa na mabunge yote yanayoongozwa na chama cha LDP na chama kidogo katika Serikali ya Muungano cha Komeito.

Suga mwenye umri wa miaka 71 ambaye ameahidi kuendeleza sera za mtangulizi wake Shinzo Abe, anatarajiwa kuunda baraza lake la mawaziri leo.

Hata hivyo, anatarajiwa kuwateua mawaziri waliokuwa katika baraza lililopita kama Waziri wa Fedha, Taro Aso na Waziri wa Mambo ya Nje, Toshimitsu Motegi kwa ajili ya kusaidia kusongesha gurudumu la maendeleo nchini humo.

No comments

Powered by Blogger.