TAMWA, Action Aid wazipa jamii mbinu za kukomesha udhalilishaji

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) Zanzibar kwa kushirikiana na Shirika la Action Aid kwa lengo la kupambana na udhalilishaji wa kijinsi wamewapatia mafunzo wanajamii 660 kutoka shehia 22 Wilaya ya Kaskazini B Unguja jijini Zanzibar, anaripoti Talib Ussi (Diramakini) Zanzibar.

Afisa wa Masuala ya Udhalilishaji kutoka TAMWA-Zanzibar,Zaina Salum Abdaala amesema, lengo kuu la mafunzo hayo kwa wanajamii hususani wanawake ni kujengewa ufahamu zaidi juu ya dhana nzima ya udhalilishaji na madhara yake kwa kuwa bila kuwa na elimu sahihi dhidi ya matendo hayo hayataweza kumalizika.

Wasanii kutoa Taasisi ya Thesode wakionesha igizo ambalo linaashirikia kukamatwa na mhusika wa matukio ya udhalilishaji kwa wanawake huku lengo kuu likiwa ni kutoa elimu kwa jamii kutoyafumbia macho matendo hayo. (Diramakini).

Ameeleza kuwa, anaamini elimu hiyo ilitoyotolewa kwa muda wa wiki mbili kwa wanajamii italeta mabadiliko makubwa ikiwemo wanajamii kufahamu viashiria vya udhalilishaji sambamba na umuhimu wa kutoa taarifa mara moja pale matukio hayo yanapojitokeza kwenye jamii.

Baadhi ya wananchi wa Shehia ya Bumbwini Wilaya ya Kaskazini B Unguja waliohudhuria katika mkutano maalumu wa utoaji wa elimu dhidi ya matendo ya udhalilishaji yaliotolewa na TAMWA-Zanzibar kwa kuhirikiana na Action Aid.(Diramakini).

Amesema kuwa, katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar hadi sasa baadhi ya wanajamii wamekua wakiyafumbia macho matendo hayo kwa wanawake na watoto kutokana kuhofia sababu mbalimbali ikiwemo kuvunjika kwa ndoa zao.

‘’Kuna matukio mbalimbali ya udhalilishaji yanafanyika, lakini watu wapo tayari kuona yanaendela, lakini hushindwa kusema kwa kuhofia kupewa talaka na waume zao,"ameongeza.

Hata hivyo, Afisa huyo ameiasa jamii kubadilika na kutokuwa na muhali badala yake watoke na kutoa taarifa dhidi ya matendo hayo kwa lengo la kuchukuliwa hatua kali zaidi kwa watendaji wote watakaobainika kutenda unyama huo.

Akizungumza kwa niaba ya Masheha wenzake Sheha wa Shehia ya Kitope, Khamis Ndende Juma amesema, ni kweli kuwa wamekua wakikabiliwa na matukio mbalimbali ya udhalilishaji kwenye jamii kiasi kwamba walio wengi wameanza kushtuka na kuhofia madhara zaidi.

Amesema, suala la muhali bado ni tatizo ambalo wanaendelea kukabiliana nalo ndani ya jamii zao kwa kuwa wapo baadhi ya watu wanatendewa matendo hayo na kisha kuamua kunyamaza kimya.

Hata hivyo Sheha huyo amesema kupitia elimu hiyo iliyotolewa na TAMWA-Zanzibar anaamini kwa kiasi kikubwa itakwenda kubadili jamii na hatimae watu kuwa tayari kutoa ushirikiano wa kina dhidi ya matendo hayo kwa lengo la kuyamaliza kabisa.

Wasanii kutoka Taasisi ya Thesode wakionesha igizo ambalo tayari mtuhumiwa wa ubakaji ameshafikishwa katika Dawati la Jinsia kwa hatua ya awali ya uanzaji wa kesi. (Diramakini).

Mzee Ali Makame kutoka Shehia ya Kitope amesema ili jamii iweze kumaliza tatizo hilo ipo haja kuhakikisha wazazi na walezi wanakua karibu zaidi na watoto wao kila wakati.

Amesema, baadhi ya matukio mengi yanayotokea yanaonesha wazi kuwa baadhi ya wazazi ama walenzi wamekosa umakini katika suala zima la uangalifu kwa watoto na wakati mwingine huwa sababu ya kufanyiwa unyama huo.

Kwa upade wake Afisa Dawati la Jinsia Mkoa wa Kaskazini Unguja, Salum Khamis Machano amesema, Jeshi la Polisi kupitia Dawati la Jinsia wanajitahidi kwa kiasi kikubwa kupambana na matukio hayo ikiwemo kuwachukulia hatua wale wote wanaofikishwa katika dawati hilo.

Hata hivyo, Afisa huyo amesema, bado kuna tatizo ndani ya jamii ikiwemo la kukosa utayari wa kuendelea na baadhi ya kesi ambazo huwa tayari zimeshafikishwa katika vituo mbalimbali vya polisi.

Aliomba jamii kubadilika na kuyachukuliwa matendo hayo kuwa ni ya kinyama na yasiopaswa kuvumiliwa kwa mtu yoyote yule awe mzee,mtoto ndugu au jirani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news