TAMWA yadhamiria kutokomeza vitendo vya ukatili kwa watoto,wanawake

CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA)-Zanzibar kwa lengo la kuhakikisha udhalilishaji wanawake na watoto unamalizika Zanzibar kimewapa mafunzo ya kupambana na matendo hayo wanajamii wapatao 1,972 katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, anaripoti TALIB USSI (Diramakini) ZANZIBAR.

Mjumbe wa mtandao wa kupingana na udhalilishaji Mkoa wa Kaskazini Unguja, Kamu Vuai Khamis akiwasilisha ripoti fupi dhidi ya matukio ya udhalilishaji baada ya kufanyika kwa mafunzo ya kupambana na matukio ya udhalilishaji katika Mkoa wa Kaskazini Unguja. (Picha na Talib Ussi/Diramakini).
Mafunzo hayo yamewanufaisha wanajamii wa makundi mbalimbali kutoka shehia tofauti ndani ya mkoa huo kwa kutumia wana mtandao maalumu ambao wamewezeshwa na chama hicho katika utoaji wa elimu dhidi ya udhalilishaji kwa wanawake na watoto.

Akizungumza katika uwasilishwaji wa taarifa baada ya kufanyika wa mafunzo hayo Afisa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka TAMWA-Zanzibar, Mohamed Khatib amesema,utolewaji wa mafunzo hayo kwa jamii unalenga kuionesha jamii madhara ya udhalilishaji kwa watoto ambapo anaamini kuwa jamii isipokua na uelewa huenda matendo hayo yakaendelea kusalia siku hadi siku.

Amesema,wameamua kutoa elimu hiyo kwa idadi kubwa ya watu kutoka katika makundi mbalimbali ambayo yamekuwa katika mazingira hatarishi na kuna ulazima wa kupatiwa elimu hiyo.

Hata hivyo Afisa huyo amesema kuwa,miongoni mwa wanufaika wa mafunzo hayo ni pamoja na wanafunzi waliopo vyuoni ikiwemo Chuo cha Amali Mkokotoni pamoja na kambi za JKU ambapo kwa kiasi kikubwa wanaonekana kuwa katika mazingira hatarishi kufuatia mchanganyiko wao na jamii tofauti.

Pamoja na hayo Afisa huyo amewataka wanamtandao wa kupambana na udhalilishaji wa kijinsia Mkoa wa Kaskazini Unguja kuhakikisha wanafanya kazi zao bila kuchoka kwa maslahi ya jamii dhidi ya matendo hayo maovu.

‘’Ni lazima muwe na utaratibu wa kuitazama jamii kwa jicho la mbali na ikiwezekana elimu iliyotolewa iwafikie wengi zaidi hata wale wasiokuwepo kwenye mikutano yetu,"amesema.

Akiwasilisha ripoti ya utafiti mdogo uliofanywa na wanamtandao huo wa Kaskazini Unguja, Bi.Kamu Vuai Khamis amesema, zipo changamoto mbalimbali ambazo zinaendelea kuwakabili katika kupambana na vita ya udhalilishaji.

Akitaja changamoto hizo amesema ni pamoja na baadhi ya wanajamii kutokuwa tayari kutoa ushirikiano kwa wanamtandao kwa lengo la kuibua kesi za udhalilishaji ambazo miongoni mwao ni watoto wao wanaofanyiwa.

‘’Kwa mfano hivi sasa katika moja ya shehia Mkoa wa Kaskazini Unguja mama mtoto amediriki kuficha taarifa za mtoto wake aliyebakwa na kuamua kumpa dawa za Kiswahili akiamini anaweza kupoa na hadi sasa bado mtoto huyo anaedelea na maumivu,"amesema.

Akizungumzia kuhusu hali halisi ilivyo dhidi ya matukio hayo ya udhalilishaji amesema, kwa kipindi cha miezi miwili iliyopita jumla ya kesi nane zimeripotiwa huku saba kati ya hizo zinaendelea na ufuatiliaji na moja imeibuliwa kwa hatua ya awali.

Kwa upande wake,Hadia Ali Makame kutoka Mkoa wa Kaskazini Unguja ambaye pia ni miongoni mwa wanamtandao wa kupinga matendo ya udhalilishaji amesema licha ya elimu kubwa inayoendelea kutolewa, lakini bado kuna changamoto ikiwemo muitikio mdogo kwa baadhi ya wanajamii.


Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news