Tume ya Haki za Binadamu yalaani tukio la kushambuliwa watu watatu msikitini

Tume ya Haki za Binadamu Zanzibar imelaani vikali tukio lililotokea Septemba 22,2020 la kushambuliwa kwa mapanga watu watatu wakiwa msikitini wakifanya ibada katika Kijiji cha Kangagani kisiwani Pemba, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Mashambulizi hayo ya kikatili kwa watu wasiokuwa na hatia ni kitendo cha kinyama na chenye kutia aibu na kuhatarisha amani nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa na Tume hiyo imesema kuwa,kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 19 na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 Ibara ya 19 zinaeleza uhuru wa mtu kuabudu na kufuata imani aitakayo.

Tume hiyo imeleza kuwa, kuvamia watu msikitini, kanisani, au mahali  popote pa ibada na kusababisha kutoendelea na ibada zao ni sawa na kuwanyima haki ya kuabudu.

“Mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda ambayo Tanzania ikiwemo Zanzibar imeridhia, inatoa ulinzi juu ya haki na uhuru wa mtu kuabudu na kufuata imani aitakayo,” imeeleza Tume hiyo

Taarifa hiyo imeeleza kuwa Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu la mwaka 1948 (Ibara ya 18) na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa wa mwaka 1966 Ibara ya 18), pamoja na mambo mengine vinaeleza haki na uhuru wa kuabudu.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa, kuvamiwa na kushambuliwa waumini hao wakiwa katika kutekeleza imani zao ni kitendo kinachopaswa kulaaniwa vikali na kila mwananchi anayethamini na kuheshimu haki za binadamu.

Hata hivyo, taarifa hiyo imeeleza kuwa vitendo kama hivyo visipochukuliwa hatua za haraka na mapema hupelekea kutokea madhara zaidi ikiwemo uvunjifu wa amani na kukosekana utulivu katika jamii na taifa kwa ujumla.

Tume hiyo imewakumbusha wananchi kuwa vitendo vya aina yoyote vya kikatili vinavyofanywa na raia wasio wema ni ukiukwaji wa sheria, haki za binadamu na misingi ya utawala bora. 

Hivyo inawasisitiza wananchi kutii sheria za nchi na kutojiingiza katika vitendo vya uvunjifu wa amani na usalama.

Aidha,Tume inatoa wito kwa Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina ili kuwakamata na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria wale wote watakaobainika kuhusika na tukio la kuvamiwa na kushambuliwa katika msikiti husika.

Hata hivyo, Tume hiyo imewaomba wananchi wa Kangagani na maeneo mengine kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kuhakikisha kuwa waliohusika kufanya kitendo hicho wanakamatwa na kufikishwa katika mamlaka husika na kuchukuliwa hatua za sheria.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news