Usanifu wa miradi ya Agri-Connect kupitiwa upya

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff ameagiza usanifu wa miradi yote ya barabara inayojengwa kwa kiwango cha lami chini ya mradi wa Agri-Connect kupitiwa upya ili kurekebisha kasoro katika maeneo ambayo yana shida ili ziweze kuwa zenye viwango na ubora kwa mahitaji ya sasa, anaripoti Erick Mwanakulya, (TARURA) Mbeya.

Ujenzi wa Barabara ya Masebe DSP-Mpuguso TCC-Bugoba Kibaoni kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 4.9 ukiwa unaendelea katika Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya. Barabara hii inajengwa chini ya mradi wa Agri-Connect unaofadhiliwa na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU), na kusimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).

Mtendaji Mkuu ameyasema hayo jijini Mbeya alipofanya ziara ya ukaguzi wa miradi hiyo inayofadhiliwa na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU) na kusimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).

“Tulikuwa na tatizo la usanifu katika miradi yote ya Agri-Connect lakini sasa usanifu unapitiwa ili kurekebisha maeneo yote yenye shida,”amesema Mhandisi Seff.

Mtendaji Mkuu amesema kuwa, katika Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe jumla ya kilomita 11 zinajengwa kwa kiwango cha lami na tayari ameshamuelekeza Mkandarasi GS Contractors anayetekeleza ujenzi wa Barabara ya Masebe DSP-Mpuguso TCC-Bugoba Kibaoni yenye urefu wa kilomita 4.9, na Mkandarasi Summer Construction Ltd anayetekeleza ujenzi wa Barabara ya Masebe- Lugoba-Lutete yenye urefu wa kilomita 7.2 kuhakikisha wanamaliza miradi hiyo ifikapo mwezi Desemba, 2020 kulingana na mkataba.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff (mwenye fulana ya bluu), akikagua ujenzi wa Barabara ya Lupeta-Wimba-Zumbwe kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 10.1 katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya mkoani Mbeya. Barabara hii inajengwa chini ya mradi wa Agri-Connect unaofadhiliwa na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU), na kusimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).

“Nimepita katika miradi inayotekelezwa na nimewaelekeza wafanye kazi kwa viwango, pia wamenihaidi kufikia mwezi Desemba 2020 watakuwa wamemaliza miradi hii kama muda ulivyopangwa japokuwa wapo nyuma ya muda, pia kutoka barabara kuu barabara yetu inaanzia katikati kipande kingine kinatekelezwa na TANROADS nimewaelekeza wafanye usanifu sehemu ya kipande cha mita 800 ili kuwe na muendelezo wa lami kutoka barabara kuu”.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff (mwenye fulana ya bluu), akitoa maelekezo kwa Wahandisi wa TARURA pamoja na Mkandarasi Milembe Construction wakati akikagua ujenzi wa Barabara ya Inyala-Simambwe kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 16.7 iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya mkoani Mbeya.

Aidha, Mhandisi Seff ameonesha kutoridhishwa na kasi ya Mkandarasi M/S Canopies International Ltd anayetekeleza Barabara ya Lupeta-Wimba-Zumbwe yenye urefu wakilomita 10.1km na Mkandarasi Milembe Construction anayetekeleza Barabara ya Inyala- Simambwe yenye urefu w kilomita 16.7 katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Vijijini kutokana na kasi ya utekelezaji kuwa chini na hivyo watashindwa kumaliza miradi hiyo kwa wakati.

“Maendeleo ya miradi hayaridhishi, hivyo nimemwacha mwandisi kutoka Makao Makuu ili ashirikiane na wahandisi wa hapa Mbeya vijijini kupitia upya miradi yote na kuja mapendekezo na jinsi ya kutatua changamoto ambazo zimejitokeza katika miradi hii”, alisema Mtendaji Mkuu wa TARURA.

Ameongeza kuwa Wakandarasi ni kama hawafahamu ukubwa wa kazi waliyonayo kwa maana muda umepita kwa asilimia 50 na utekelezaji wa kazi upo chini ya asilimia 20 kitu ambacho kinaonyesha kwa miezi minne iliyobaki hawawezi kumaliza miradi hiyo kwa wakati.

Ujenzi wa Barabara ya Inyala–Simambwe kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 16.7 ukiwa unaendelea katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, mkoani Mbeya. Barabara hii inajengwa chini ya mradi wa Agri-Connect inayofadhiliwa na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU), na kusimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).

Katika hatua nyingine, Mtendaji Mkuu amemuelekeza Mratibu wa TARURA Mkoa wa Mbeya pamoja na Mameneja wa TARURA katika Halmashauri zote za Mkoa wa Mbeya kuhakikisha wanasimamia miradi iliyopo katika maeneo yao ya kazi. Vile vile, amemtaka Meneja wa TARURA katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya kuhakikisha anafanya ukarabati wa barabara kwenye eneo lake kwakuwa hali yake hairidhishi.

Miradi ya Agri-Connect ina lengo la kuwawezesha wakulima kusafirisha mazao yao kwa urahisi kutoka mashambani kwenda sokoni ikiwa inagusa mazao mbali mbali yakiwemo chai, kahawa, mbogamboga na matunda ambayo inatekelezwa katika Mkoa wa Iringa (Kilolo DC na Mufindi DC) pamoja na Mbeya (Mbeya DC na Rungwe DC).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news