Utekelezaji miradi kwa kutumia 'force account' waneemesha Manyara



Mkurugenzi Msaidizi Menejimenti ya Rasilimali Watu Wizara ya Maji , Ingrid Sanda akimtwisha mama ndoo ya maji wakati wa ziara ya ukaguzi wa utekelezaji wa miradi ya maji mkoani Manyara. (WM).

Matumizi ya Utekelezaji Miradi ya maji kwa kuwatumia wataalamu wa wizara (Force account) mkoani Manyara umewezesha ongezeko la miradi tisa ambayo itasababisha wananchi 20,000 kufikiwa na huduma ya maji, anaripoti Evarity Masuha, WM.

Akizungumza na wataalamu wa Wizara ya Maji waliopo katika ziara ya kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maji mkoani humo, Kaimu Meneja wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Manyara,Mhandisi Walter Kirita amesema, mpango wa awali ulikuwa ni kuwafikia wananchi 26,000.

Hata hivyo, baada ya kuanza kutekeleza miradi hiyo kwa kutumia mfumo huo wameweza kubakiza fedha ambazo zitapelekwa katika miradi mingine mipya.

“RUWASA makao makuu wamenunua vitu vingi kwa bei nzuri, tukaamua kutumia 'force account' ambayo imewezesha kuongeza miradi mipya tisa ambayo itaongeza upatikanaji wa maji kwa wananchi 20,000. Hii imekuwa zaidi ya matarajio kwani awali tulitarajia kwamba tungewafikia wananchi 26,000 pekee,”amesema Mhandisi Walter Kirita.

Anasema, kwa mwaka 2020/2021 RUWASA imetenga shillingi bilioni 13.4 kwa ajili ya kutekeleza miradi 45 ambayo itasaidia upatikanaji wa maji kwa watu 157,903.

Mafundi wakiendelea na ujenzi wa miundombinu ya maji mkoani Manyara. (WM).

Ofisa na mtaalamu huyo wa maji amepongeza Serikali kwa kuweka msisitizo katika utekelezaji wa miradi kwa kutumia 'force account' kwani miradi mingi imeweza kukamilika kwa haraka na kwa gharama nafuu.

Amesema, wana uhakika wa kutekeleza miradi mingi zaidi kutokana na matokeo yaliyopatikana kutokana na matumizi ya mfumo huo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Menejimenti ya Rasilimali watu kutoka Wizara ya Maji, Ingrid Sanda amewapongeza watumishi wa wizara hiyo kwa kufanya kazi kwa bidiii.

Amesema, wizara inao wataalamu wa kutosha hivyo matumizi ya force account ni nafasi nzuri ya kuonesha uwezo, ujuzi na maarifa waliyosomea.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news