UVCCM: Iwe jua, iwe mvua Ubungo hatutaliachia tena, miaka 10 inawatosha

MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi  (UVCCM) Kata ya Kimara Wilaya ya Ub ungo mkoani Dar es Salaam, Cliff Maulid Mtapai amewataka wananchi wa kata hiyo kutorudia makosa walioyafanya 2015 kwa kuuchagua upinzani, anaripoti FATMA ALLY kutoka DAR ES SALAAM.

Kauli hiyo ameitoa jijini Dar es Salaam leo wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye uzinduzi wa kampeni za ndani kwa ajili ya kutafuta kura kwa wagombea wa chama hicho.

Amesema kuwa, wananchi wameyaona makosa walioyafanya uchaguzi wa 2015 kwa kuwachagua viongozi ambao kazi yao ni kukosoa tu na kukimbia vikao bungeni.

Aidha, amesema, wamejipanga vizuri na wapo tayari kupiga kura muda wowote kwani ilani ya uchaguzi 2015 ya CCM imetekelezwa kwa asilimia kubwa, hivyo hana hofu hata ilani ya 2020/2025 itatekelezwa kwa asilimia 100.

Kwa upande wake, Mgombea udiwani wa Viti maalum Kata ya Kimara, Nuru Mbezi amesema kuwa, sasa ni muda wa kuvirejesha viti vyote vilivyokuwa chini ya upinzani.

Amesema kuwa, kwa muda wa miaka 10 Jimbo la Ubungo limekuwa likiongozwa na upinzani,hivyo wamejipanga iwe jua ama mvua watahakikisha jimbo hilo linarudi CCM.

"Viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi mkuu wa 2015 wananchi walifanya makosa sana kwani viongozi hao kutwa ni kususia bunge wakati changamoto za ndani ya kata zikitatuliwa,"amesema Mbezi.

Naye, Katibu wa UVCCM Kata ya Kimara, Ahmedy Mursaly Ahmed amesema kuwa, wamejipanga kuhakikisha kundi lote la vijana linaipigia kura CCM kwa kumchagua Rais John Magufuli, mgombea ubunge Jimbo la Ubungo, Prof. Kitila Mkumbo pamoja na Diwani Kata ya Kimara, Ismail Mvungi.

Amesema kuwa, baada ya mkutano huo wa ndani watakwenda kuwaelezea wananchi jinsi ilani ya CCM ilivyotekelzwa kwa asilimia kubwa, ikiwemo kujenga miundombinu pamoja na kutatua kero ya maji katika Kata Mavurunza katika jimbo hilo la Ubungo.

No comments

Powered by Blogger.