Vodacom Tanzania yatangaza namna wateja milioni nane watakavyoanza kupokea gawio

ZAIDI ya wateja wa Vodacom M-Pesa milioni nane kuanzia leo watapata sehemu ya faida ya shilingi bilioni 3.5 ikiwa ni gawio kutoka kwenye akaunti ya M-Pesa Trust. 

Kampuni ya Vodacom Tanzania PLC imetangaza kwamba kuanzia sasa wateja wake wa M-Pesa watapata sehemu yao ya gawio hilo lililopatikana kama faida ya matumizi ya huduma hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa M-Commerce, Epimack Mbeteni amesema, “tuna shauku ya kugawana faida hii na wateja wetu kwani wao ndio sababu ya mafanikio ya huduma ya M-Pesa. "Huduma ya M-Pesa imechangia maendeleo lukuki ya Watanzania na mpango huu umedhamiria kuendelea kuwapa wateja wetu faida zaidi. Wateja wote wa Vodacom ambao wamekuwa wakitumia M-Pesa kuanzia Januari Mosi hadi Machi 31, mwaka huu watafaidika na bonasi hii ya shilingi bilioni 3.5 ambayo itagawiwa moja kwa moja kupitia M-Pesa,”amesema.

Amesema, kuanzia sasa wateja wa Vodacom wanaweza kutuma SMS ya neno KIASI kwenda namba 15300 ili kujua kiwango gani cha faida watapokea.  

Baada ya kupata gawio hilo, wateja wa M-Pesa wanaweza kukomboa faida hiyo kwa kuitoa kama fedha taslimu, kununua muda wa maongezi, vifurushi au kulipia bili.

“Kiasi ambacho mtu atapokea kama sehemu ya faida hiyo itategemea na idadi ya miamala aliyokuwa akifanya kwa kipindi nilichotaja hapo juu. Shughuli hizo ni kama miamala ya kuhamisha fedha, malipo ya bili mbalimbali au manunuzi ya muda wa maongezi. 

"Napenda kuwahimiza wateja wetu kutuma SMS ili kujua ni kiasi gani cha gawio hili wanastahili kupokea,”amesisitiza Mbeteni huku akiongeza kwamba mpaka sasa Vodacom Tanzania PLC imeshagawa faida ya jumla ya shilingi bilioni 133 kwa wateja wa M-Pesa.

M-Pesa ina umiliki wa soko wa asilimia 39 na inaongoza kwa kuwa huduma ya fedha za mkononi inayotumiwa na Watanzania wengi zaidi ambao wanafanya miamala ya hadi shilingi bilioni 100 kwa siku. 

“Tumewekeza vilivyo katika M-Pesa ndani ya miaka kumi na mbili iliyopita na sasa huduma imekuwa na ufumbuzi wa kibunifu unaokidhi mahitaji ya watanzania kupitia bidhaa mbalimbali kama vile M-Koba, M-Pawa, Halal Pesa M-Pesa MasterCard na nyingine nyingi. Tunaendelea kuwa na nia ya kuboresha huduma hii kwa njia ya ubunifu huku tukishirikiana na makampuni pamoja na wavumbuzi mbalimbali ili kuendesha ajenda ya ujumuishwaji wa kifedha nchini,”amefafanua Mbeteni.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news